KAMANDA KOVA: TUMEKAMATA WAWILI KWA MAUAJI YA SISTA DAR ES SALAAM

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova

 
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imewakamata watu wanane na kati ya hao, wawili wakidaiwa kuhusika na mauaji ya Sista wa Kanisa Katoliki, Cresencia Kapuri na wengine, uporaji wa Benki ya Barclays, Tawi la Kinondoni.
Watuhumiwa hao wawili wanadaiwa kuwa, Juni 23, mwaka huu walifanya mauaji ya Sista huyo eneo la Riverside, Ubungo, Dar es Salaam na kupora kiasi cha Sh20 milioni na nyaraka mbalimbali.
Katika tukio jingine la Aprili 15, mwaka huu watuhumiwa wengine wanadaiwa kupora Sh500 milioni za benki ya Barclays.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema majambazi hao walikamatwa kutokana na operesheni kali inayoendelea jijini hasa baada ya kifo cha sista huyo.
Kamanda Kova alisema watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na mauaji ya mtawa huyo wa Kanisa Katoliki, mmoja alikuwa akiendesha bodaboda na alimbeba jambazi mwenzake akiwa na fuko la mamilioni ya fedha na kutoroka nalo wakati mtuhumiwa wa pili aliyekamatwa ambaye ni mfanyabiashara, ndiye aliyekuwa kiongozi katika tukio hilo.
Kova alisema polisi bado inawatafuta watuhumiwa wengine wawili.

Comments