Waziri wa Mambo ya Ndani, Matthias Chikawe ©Mwananchi |
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe ametishia kulifuta Kanisa la
Moravian kutokana na migogoro ya mara kwa mara inayolikumba.
Chikawe pia ametangaza kuyafutia usajili madhehebu na makanisa mengine
yenye migogoro ya ndani, hali inayohatarisha amani ya nchi.
Waziri Chikawe alisema hayo jana wakati wa maombezi maalumu ya kuliombea
taifa yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Karismatiki Katoliki, Jimbo Kuu la
Dar es Salaam.
Alisema Kanisa la Moravian limekuwa katika migogoro kiasi cha waumini wake kupigana hadharani tena kanisani wakati wa ibada.
“Ninawataka viongozi wa kanisa hili kumaliza tofauti zao kupitia
mabaraza yao ya ndani badala ya kufikishana katika vituo vya polisi,
vinginevyo nitachukua hatua za kuyafuta kwa kuwa yanahatarisha amani ya
nchi,” alisema na kuongeza:
“Moja ya majukumu ya wizara yangu ni pamoja na kusajili madhehebu na
vikundi vya kidini chini ya Sheria ya Vyama Sura 337. Sitasita kuyafutia
usajili madhehebu yoyote yanayotawaliwa na migogoro ili kuepusha
shari.”
Chikawe aliwataka viongozi kuwa mfano wa kuigwa kwa kutumia fursa
walizonazo kuwakumbusha waumini wao kuwa na hofu ya Mungu, pia kujenga
umoja, amani na mshikamano miongoni mwao.
“Niwatake viongozi wa Kanisa la Moravian nchini kumaliza mgogoro wao kwa
busara na kwa kutumia vitabu vya Mungu badala ya kupishana katika vituo
vya polisi wakishtakiana,” alisema.
Kauli ya Chikawe inakuja ikiwa ni siku chache baada ya Askofu Kiongozi
wa Kanisa la Moravian Tanzania, Alinikisa Cheyo kusema migogoro
iliyolikumba kanisa lake inachangiwa na utovu wa nidhamu pamoja na
kutojua taratibu za uongozi ndani ya kanisa.
Akizungumza mjini Mbeya, Makao Makuu ya kanisa hilo, Cheyo alisema utovu
wa nidhamu unaambatana na ubinafsi na kutaka kufanya kazi kwa manufaa
binafsi. Hivi karibuni, waumini na wachungaji wa Jimbo la Kusini
Magharibi walifunga kwa makufuli na minyororo, ofisi ya askofu huyo
Mtaa wa Jakaranda, Mbeya, wakimshinikiza ajiuzulu. Waumini hao walidai
kuwa Askofu huyo amemfukuza Mwenyekiti wa jimbo hilo, Nosigwe Buya bila
kufuata taratibu.
Mbali ya tukio hilo la hivi karibuni, kanisa hilo limekuwa na migogoro
ya mara kwa mara mkoani Dar es Salaam katika mazingira tofauti. Pia
limekuwa katika migogoro mingi ya uongozi tangu mwaka 2012, baada ya
kuondolewa nyadhifa na kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa
Jimbo la Misheni ya Mashariki, Clement Fumbo.
Chanzo: Mwananchi
Comments