KIZAZI CHA ZINAA

Na Frank Philip


“Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kando-kando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu. Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa. Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa” (Ufunuo 15:2-4).

“Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaonyeshe ishara itokayo mbinguni. Akajibu, akawaambia, [Kukiwa jioni, mwasema, Kutakuwa na kianga; kwa maana mbingu ni nyekundu. Na asubuhi, mwasema, Leo kutakuwa na dhoruba; kwa maana mbingu ni nyekundu, tena kumetanda. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa mbingu; lakini, je! Ishara za zamani hizi hamwezi kuzitambua?] Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake” (Mathayo 16:1-4).

Umewahi kujiuliza ni kwanini watumishi wengi wa Mungu wanatafuta kuwa WAFANYAJI wa ishara na miujiza? Umewahi kujiuliza ni kwanini watu wengi wanavutwa na ishara na miujiza? Je! Unadhani hili ni jambo jipya? La! Hasha, hili jambo sio jipya, lilikuwepo tangu zamani za Musa, na zamani Bwana akifanya huduma miaka takriban 2000 iliyopita.

Nitakuonyesha jambo. Musa alikuwa nabii ambaye hapana kama yeye kabla yake na baada yake, yeye aliongea na Mungu uso kwa uso. Mungu alimpa uwezo wa miujiza, lakini hakufanya miujiza kama APENDAVYO, ila kwa maagizo ya Mungu pekee. Musa hakufanya miujiza ILI ajulikane naye ni nabii, hakuliinua jina lake mwenyewe ila Jina la Bwana. Ona tena, Bwana Yesu, anasema “hakufanya jambo ambalo hakumwona Baba yake akifanya”. Mapenzi ya Mungu ilikuwa ndio chakula chake. Jiulize tena, unataka ufanye miujiza na ishara ili nini? Kisha jiulize tena, ukiisha kufanya ishara na miujiza, unataka watu waone ili nini? Je! Wewe si udongo tu mikononi mwa mfinyanzi? Iweje leo unataka kujipangia uwe chambo tofauti, kinyume na mfinyanzi?

Angalia wale watakaoingia Mbinguni watakachoimba, “wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo” na kisha watauliza “Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa. Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako?” Umejiuliza kuna manabii wangapi wakubwa, ila wataimbwa wawili tu? Musa na Yesu! Musa hakutafuta mambo yake ila ya Bwana aliyemtuma, jina lake ni “MTUMWA wa MUNGU”, je! Leo tunaona “watumwa wa Mungu” au “viji-mungu mtu”? Nataka uone ALAMA za hatari na ujihadhari, maana sio kila mtu atendaye miujiza kwa Jina la Bwana amekubalika. Wapo wengi wataambiwa “kwanza sikuwajua”, yaani huko duniani wajapokuwa na majina yao “mahali pa juu sana”, kumbe! Bwana hawajui! Basi nitatazama neno hili Mtume Paulo alilotufundisha, “pamoja na unabii, imani timilifu, miujiza, kutoa sadaka kubwa kubwa, nk. Kama sina UPENDO, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao”.

Jifunze kujinyenyekesha na kumtafuta Mungu kama Bwana, na wewe kama “mtumwa wa Mungu”, japo unakibali kama mwana. Hakuna mahali mtumwa anajipangia cha kufanya, ila kile bwana wake atakacho. Mtumwa hana fahari yake mwenyewe kwa chochote, kwa maana yeye ni mtumwa tu, mtumishi asiye na faida, ila kila jambo afanyalo litaitwa kwa “jina la bwana wake”. Kwa mfano, hebu fikiria kiwanda cha magari cha Suzuki. Huyu ndugu Suzuki alikuwa Mjapani huko, maelfu na maelfu ya watu wamefanya kazi kuunda magari ya Suzuki, ila kwa jina la bwana wao. Ndio maana kila ukiangalia utaona jina Suzuki, na sio majina ya hao watenda kazi waliounda hayo magari. Mbona sisi tunamtenda Bwana wetu kinyume? Mbona tunainua majina yetu na huduma zetu, na kutafuta kuonekana wakati kazi ni yake?

Najua wengi wameanza kukodolea macho watumishi wa Mungu. Watumishi wa Mungu watajibu kwa Mungu wao, haikuhusu wewe. Huu ujumbe ni wako na si wa mwingine. Angalia mambo yako hayo hayo madogo, je! Umemwinua Bwana kwa kiwango gani? Angalia tena hapa, wale watu wakasema mbele za Bwana huko Mbinguni, Je! “Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako?” Hapa sio habari ya WATUMISHI wa Mungu, ni suala la KILA mtu, mkubwa kwa mdogo, kwa maana “aliyepewa vingi, kwake vitatakiwa vingi, na aliyepewa vichache, kwake vitadaiwa vichache”. Je! Kwenye vichache vyako, umemcha Mungu? Umelitukuza jina la Mungu?

Frank Philip.

Comments