KWA NENO LA MUNGU,NITAZISHUSHA NYAVU *sehemu ya mwisho *

Na mtumishi wa MUNGU Gasper Madumla


" Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.

Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;
wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. " Luka 5:5-7

Hata walipofanikiwa kuvua samaki wengi kwa uweza wa jina la Bwana,wahawakusita kuwapungia washirika wenzao walio chombo cha pili. Huu ni moyo wa shirika,moyo wa upendo ndani ya mafanikio yaliyopatikana.

Moyo wa shirika ni ile hali ya kutokukumbatia mafanikio yote apatayo mtu mmoja au kikundi kimoja,bali kuwashirikisha ndugu wengine katika roho,kwamba kilichopatikana kitumiwe kwa wote na sio mtu mmoja.Wakina Simoni hawakuona kitu cha kuchukuliana nacho,kuyakumbatia mafanikio yote wao pasipo kuwashirikisha washirika wenzao.

Jambo hili lina asili tangia hapo awali kwa kanisa la kwanza,maana ndivyo lilivyokuwa likitenda kwa moyo mmoja wa shirika. Na huu ulikuwa ni moyo wa Bwana Yesu Kristo,tazama tunasoma;

" Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika,
wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja " Matendo 2:44-45.

Wote walioamini walikuwa mahali pamoja na kuwa vitu vyote shirika,hii inamaanisha kwamba Mungu anapoachilia mbaraka kwa mmoja,basi mbaraka huo unakuwa ni wa faida kwa wote.

Na hapo ndipo tunaambiwa kwamba Mungu akalizidisha kanisa.
Nami nasema hivi;
Ukitaka kanisa lako lizidi,basi iweni shirika ninyi nyote mnaoamini.

Ahaa!,
Hali hii ilikuwa nzuri sana,maana hakuna cha nani wala nani,bali wote walikuwa ni sawa mbele za Bwana.
Swali langu kwako;
Je hali hii ikoje sasa?

Jibu unalo mwenyewe ndugu mpendwa katika Bwana.Ukweli ni kwamba;
Hali ya kanisa la leo limekosa MOYO WA SHIRIKA.
Mara nyingi,mali ipatikanayo hushikiliwa na mtu mmoja au na watu wachache.

Mfano;
Mtumishi anaye hudumu anaweza akawa na mali nyingi za thamani hali waamini wake wanakufa njaa. Anaweza kumiliki magari ya kifahali,magari yaliyopatikana kwa njia ya huduma,wala si kwa jasho lake,lakini waamini hata lifti hawapati,tena nini lifti! Hata kulisogelea gari la mtumishi ni mwiko!

Mbaya zaidi, mara nyingine mtumishi wa Mungu hula vyakula vya bei ya juu mno,wakati wapo baadhi ya waamini wake wakihitaji pesa kidogo tu kwa ajili ya kuwezesha mlo mmoja tu.

Zaidi ya yote hali ya sasa imepelekea hadi baadhi ya makanisa ya kiroho kutenga baadhi ya watu na watu fulani ndani ya kanisa wakati wa ibada. Wengi hutengwa mahali pa kukaa siku zote sababu ya position ya pesa zao,na wengine ni MARUFUKU kuonekana wamekaa katika siti za wenye nazo.
Lakini neno la Mungu halisemi hivyo,bali Neno linatutaka tuwe shirika,pasiwepo na matabaka kanisani. Hali hii ya matabaka,hakika huzuilia matendo makuu ya Bwana,na huwa hakuna ibada halisi ya namna hiyo,tulitizame neno la Mungu linatuambiaje;

" Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, " Matendo 2:44

Katika Luka 5:5-7,tumesoma hapo juu ile namna ya wandugu hawa walivyogawana mafanikio yaliyopatikana. Lazima ifike wakati ambapo tutashirikiana chochote kinachopatikana kwa kazi ya Bwana,sababu hiyo sio kazi yetu bali ni ya BWANA Mungu,na tushirikiane kwa pamoja,kisha tumrudishie vyote BWANA Mungu.

Haleluya....
Nasema Haleluya..,Haleluya...
Blessed be the name of Jesus,
Say Amen,...

Vitendea kazi tulivyo navyo,hujulikana kama NYAVU. Nyavu hazina maana pasipo Neno la Mungu. Kwa neno la Bwana; Nyavu huwa na thamani. Nami nasema kwako jambo hili wazi wazi ya kwamba;
Heri mtu yule mwenye nyavu,ategaye kwa neno la Bwana. Nisemapo " heri " maana yake " amebarikiwa"

Haleluya...

Lakini pia tunasoma tena ;

" Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata. " Luka 5:11

Zingatia hapo " Waakacha vyote wakamfuata" Unisikilize mpendwa;
Hawa watu walioacha vyote ni watu waliofanikiwa tayari kwa mafanikio makubwa sana,ila wakaona mafanikio ya kupata samaki si chochote,ni kama mavi ili wampate Kristo. Watu hawa wanatufundisha leo , MAFANIKIO YOYOTE HAYANA MAANA KAMA KUMPATA KRISTO.

Hata Paulo,ilifika wakati akayaona mambo yote nje ya Kristo ni kama mavi shauli la kumpata Kristo,anasema;

" Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; "Wafilipi 3:8

Andiko hili;
" Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata. " Luka 5:11

Nalifananisha na andiko hili;
"...akamwambia,Nifuate.Akaondoka,akamfuata." Mathayo 9:9

Umeona hayo maandiko,yanafanana fanana sababu huoni shauri lolote la kumfuata Yesu likifanywa. Baada ya kusikia,WAKAACHA VYOTE,WAKAMFUATA.

Unaposikia habari za Yesu,ni kuacha vyote na kumfuata pasipo kujiuliza uliza,nasema KUACHA VYOTE NA KUMFUATA maana Yeye Yesu ndie njia kweli na uzima (Yoh.14:6)

Haleluya...

Sijui kama unapata picha yoyote ile,kwamba kile ulichokuwa ukikitafuta kwa muda mrefu bila mafanikio,alafu gafla ukakipata na kuamua kukiacha chote kwa ajili ya Bwana Mungu,kama vile wakina Simoni walivyofanya.

Mafanikio yoyote ya kidunia hayana maana kama kumpata Yesu Kristo,maana ndani yake Bwana mna kila kitu. Unajua wakina Simoni laiti kama wange'ambatana na mafanikio waliyoyapata,inge'likuwa ni vigumu kumkufuta BWANA Yesu.

Je unahitaji umfuate Bwana Yesu Kristo sasa?..
Je unaamini kwa neno lake Mungu,utafanikiwa katika biashara yako uifanyayo sasa?
Ikiwa jibu ni NDIO,basi usisite kunipigia simu yangu tuombe kwa pamoja juu ya hitaji ulilo nalo.
Piga namba hii;
0655-111149.

MWISHO.

UBARIKIWE

Comments