MUNGU ANASEMA: BALI MTU HUYU NDIYE NITAKAYE MWANGALIA


Isaya 66:1-2
“Bwana asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzika ni mahali gani? Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema BWANA; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu”.

Isa 66:2 “All these things my hand has made, and so all these things came to be, declares the LORD. But this is the one to whom I will look: he who is humble and contrite in spirit and trembles at my word”
Ukisoma mstari huu vizuri kuna mambo mengi unaweza kujifunza lakini kile tunachotaka tukiangaalie ni sifa/tabia ambazo kama mtu akiwa nazo zitamfanya Mungu amtazame/ajifunue kwake na amsikilize mtu huyo. Naam sifa ambazo zitavuta uwepo wa Bwana ukae naye daima. Ni imani yetu kwamba kama ukiliweka jambo hili kwenye matendo lazima Bwana awe upande wako.


Sifa hizo ni;


• Mtu aliye mnyonge 


Kwa tafsiri ya kawaida, Mnyonge ni mtu mwenye kustahili huruma/msaada, mtu asiyejiweza, mnyenyekevu, aliye duni, dhaifu, mwenye upungufu, muhitaji nk. Naam kwa maana ya mafundisho ya kiroho, Mnyonge ni yule mwenye kuhitaji msaada wa Mungu siku zote za Maisha yake kwa kuwa yeye pekee hawezi jambo lolote bila Bwana. Mungu yupo tayari kumsaidia kila anayehitaji msaada wake.
Biblia inaposeama mtu aliye mnyonge maana mwenye kuhitaji msaada/huruma toka kwa Mungu. Usijaribu kufikiri mtu anaweza kufanya jambo lolote bila Bwana, jifunze kuishi maisha ambayo Bwana mwenyewe ataona na kujua kwamba mwanangu huyu ametambua kwamba mimi ndiyo nguzo yake, naam bila mimi yeye hawezi jambo lolote. Hivyo katika maisha yako yote jifunze kutafuta msaada wa Mungu kwa kila jambo ulifanyalo ndivyo utakavyofanikiwa.


• Mwenye roho iliyo pondeka


Huyu ni mtu mwenye toba au roho ya toba, naam aliye mwepesi kutubu mbele za Mungu pale anapokosea. Zaburi ya 51, ni mfano sahihi wa mtu mwenye roho ya toba. Hii ni Zaburi aliyoimba na kuomba mfalme Daudi mbele za Mungu kama toba kwa sababu ya dhambi aliyotenda kwa kulala na Bathsheba mke wa Uria na kisha kumuua Uria. Mungu aliangalia toba ya Daudi na kujua kwamba ni toba ya kumaanisha na kisha akamsamehe, maana roho yake ilidhihirisha kupondeka, hebu tusome mistari kadhaa ya Zaburi 51 .
Mstari wa 1 – Ee Mungu unirehemu sawasawa na fadhili zako, kiasi cha wingi wa rehema zako uyafute makosa yangu
3 – Maana nimejua mimi makosa yangu, Na dhambi yangu i mbele yangu daima
10 – Ee Mungu uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu
11 – Usinitenge na uso wako, wala roho yako Mtakatifu usiniondolee
17 – Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika na kupondeka, Ee Mungu hutaudharau.

Biblia imeweka wazi kwamba afichaye dhambi zake hatafanikiwa, Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema (Mithali 28:12). Angalia maisha unayoishi sasa, je ndani yako unajisikia uhuru wa kumtumikia Mungu, au unahukumiwa lakini wewe unajitia tu moyo kwa sababu ya uongozi, huduma heshima au ukaribu ulionao na watumishi wa Mungu kanisani nk. Mpendwa dawa ya dhambi si kuficha bali ni kutubu.
Ushuhuda;
Nikiwa mkoa fulani, Mungu alinisemesha kuhusu dada mmoja Mwimbaji wa nyimbo za Injili ambaye alikuwa ametengwa kanisani kwao kwa sababu ya dhambi ya uasherati. Dada huyo alipoulizwa na uongozi husika kama ametenda dhambi, alikana kuhusika na dhambi hiyo na kudai anaonewa. Vikao vingi vilifanyika ili kumuhoji aseme ukweli lakini yeye alisema ukweli ni kwamba sijaanguka dhambini bali nasingiziwa tu.
Siku moja jioni dada huyo alinitumia sms akisema mtumishi jaribu la kutengwa limekuwa zito natamani hata kujiua. Baada ya kupata sms hiyo niliitafakari sana kimaandiko na kujua kwamba, lazima huyu dada kuna kitu ameficha kwa sababu kama kweli hakutenda dhambi roho ya kujiua ingetoka wapi? roho hiyo ilimjia kwa sababu ametenda dhambi na imeandikwa wazi kwamba mshahara wa dhambi ni mauti.
Usiku nikamuomba Mungu anijulishe ukweli juu ya hali ya yule dada, ndipo nikasikia sauti ikisema ‘afichaye dhambi zake hatafanikiwa’. Nikaelewa kwamba yule dada kuna dhambi amefanya na yeye ameficha. Ndipo nikamuita na kisha kumuelezea picha yote na baadaye akakiri kwamba kweli alianguka dhambini na hakutaka watu wajue kwa sababu ingemuondolea heshima aliyonayo. Nikamsaidia kiroho na sasa anaendelea vema katika Bwana.

 
Fundisho tunalotaka ujue katika ushuhuda huu ni; kwa ile miezi karibu mitano ambayo yule dada alikuwa ametengwa, maisha yake yalikuwa kama ya mtumwa, kila alichojaribu kufanya hakikuweza kufanikiwa, maisha yake yalijaa huzuni muda wote, akamuona Mungu kuwa dhalimu, kumbe yeye ndiye alikuwa dhalimu. Naam usifiche dhambi, bali tubu, Mungu yuko tayari kukusamehe usjijaribu kujitia moyo tokana na heshima au kibali ulichonacho kwa watu, mbele za Bwana ni machukizo makubwa, kuficha dhambi halafu ukaendelea kutumika. Naam tubu kabla roho ya kutokufanikiwa haijakuvamia na laana zake.


• Atetemekaye asikiapo neno langu

Huyu ni mtu mwenye kulipokea neno la Mungu kwa hofu na si mazoea. Mungu anataka watu wake wasilizoee neno lake, bali iwepo tofauti kati ya neno lake na kauli za watu wengine, watu wasilipokee neno lake kama vile taarifa ya habari za kila siku. Jifunze kutoka kwa wandugu wa Beroya, ambao walikaa chini na kuchunguza kile walichokisikia na kisha kukiweka kwenye Matendo (Matendo 17:10-12). kwenye ule mstari wa 11 Biblia inasema ‘Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo’. Je nini matokeo ya jambo hili? Ule mstari wa 13 unasema ‘Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini, na wanawake wa kiyunani wenye cheo na wanaume si wachache’.
Maandiko haya yanatusaidia kujua kwamba mtu atetemekaye asikiapo neno la Mungu ni yule ambaye anapolisikia neno la Mungu moja halipuuzii, pili analipokeea kwa uelekevu wa moyo, tatu analichunguza(kwa kutafakari) na kisha anachukua hatua ya kuliweka kwenye matendo. Naam fanya hivyo nawe utaishi.
Ni imani yetu kwamba ukiyaweka mambo haya matatu kwenye matendo basi utavuta uwepo wa Mungu kwenye maisha yako siku zote.
Mungu akubariki

Comments