NGUVU YA MAZUNGUMZO MABAYA

Na Frank Philip


“Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema. Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe” (1 Wakorontho 15:33, 34).

Kati ya silaha za maangamizi ambazo Ibilisi anatumia kuangamiza watu, mojawapo ni “mazungumzo mabaya”. Mazungumzo mabaya ni mazungumzo yoyote ambayo ndani yake watu wanasema maneno machafu, au maneno yasiyo na madili mazuri, au maneno ya shuhuda mbaya za kazi za Ibilisi, au maneno ambayo ni kinyume na Neno la Mungu, au masengenyo, nk. Kumbuka, kuna mazungumzo mengi sana ya kujenga, japo sio katika Neno la Mungu. Kwa mfano, mazungumzo ambayo yanalenga kumjenga mtu kitaaluma, kiuchumi, maisha bora ya kijamii na kiafya, nk. mazungumzo ya namna hii ni ruksa.

Kuna njia nyingi za kupitisha mazungumzo mabaya, kwa namna ambayo watu wengi hawajajua kwamba wanaathirika, ndio maana Paulo anatutahadharisha kwa kusema “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema”. Watu wengi sana WAMEJIDANGANYA kwamba yale mazungumzo wanayosikia watu wakiongea huwa yanaishia hapo. Kwa mfano, angalia maeneo ya kazini, shuleni, biashara, mitaani, nk. Utagundua kuna mazungumzo mabaya yametapakaa.

Sasa kuna mitego mingine ambayo Ibilisi ameweka katika TV, Sinema, Tamthilia, nk. Unapozama na kuchukua muda mwingi katika kutazama “mazungumzo mabaya”, kidogo kidogo, hayo mazungumzo huanza kuingia na kubaki moyoni, na kuanza kuathiri tabia yako njema bila wewe mwenyewe kujua. Ni kweli hufanyi hayo mambo kwa sasa, ila UNAYATAFAKARI! Sasa kumbuka, imekupasa kutafakari Neno la Mungu au njia za Mungu usiku na mchana, KAMA unataka kufanikiwa katika mambo yako (Zaburi 1). Nitakupa mfano, hebu fikiri mtu ambaye ni mtazamaji mzuri wa tamthilia za mapenzi/usaliti/wivu/ngono, nk. Unapoanza kuangalia, ghafla! Unaanza kuvutiwa na mwigizaji fulani, unaanza kumpenda tu na kumtafakari muda mwingi. Ghafla, unaanza kupenda kila afanyacho, na kuanza kumwonea huruma au kufurahishwa akifanya mambo fulani; nafsi yako inaanza kutekwa taratibu. Ikifikia hapo, unaanza kufuatilia kwa makini kila kitu anachofanya. Ghafla, unaanza kupata uchungu au hasira huyo mwigizaji akipatikana na majanga. Sasa hujui kwamba umeanza kuunganishwa nafsini mwako na huyu mwigizaji. Sasa nisikilize, huyu mwigizaji umpendaye au anayekuvutia, katika kuigiza kwake, akianza kufanya mambo kujitetea, kwa mfano, kufanya usaliti katika ndoa yake au mambo mengine maovu, huku ndani ya moyo wako wakati unatazama, unaanza kuona ni sawa tu kwa sababu unampenda, tena unajikuta unasema “safi sana, huyu mwanaume/mwanamke amemtesa sana, ngoja apate dawa yake”, kumbe hukujua unapokea jambo kwenye ulimwengu wa roho. Sasa nisikilize. Huko mbele sana kama mika 10 ijayo, ukiwa kwenye ndoa yako au mahusiano mengine, usishangae ukajikuta katika mazingira fulani unajikuta unafanya kama “ulivyoona kwenye tamthilia fulani” huko zamani. Tabia imebadilika na hukujua! Kikuingiacho, ndicho kikutokacho! (What goes in, the same will come out!)

Ona mtego huu, Daudi anasema “Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa” (Zaburi 1:1-3). Daudi anaonesha uhusiano kati ya MAFANIKIO katika mambo yako ufanyayo, na mambo au watu wengine unaojihusisha nao, ikiwemo na MAZUNGUMZO (barazani pa wenye mizaha). Sasa hebu fikiri, ile tamthilia iliyokukaa vizuri moyoni, na mwigizaji fulani, Ibilisi anajua hilo, sasa anaanza kukuletea picha za yule mwigizaji na matukio, unaanza kutafakari hapo na kupata hisia kali, umesahau kutafakari Neno muda huo, umezama kwenye matukio au mazungumzo mabaya ya kwenye tamthilia! Kumbe, hukujua lengo la Ibilisi ni usiwe mmojawapo wa hao watu ambao Daudi alisema “Na kila alitendalo litafanikiwa” kwa maana hutafakari Neno, ila habari mbaya tu unazosikia na kuona mitaani na kwenye vyombo ya habari!

Usisahau, mazungumzo mabaya (habari mbaya) yana nguvu ya kukamata hisia na mawazo yako, mara nyingine kuliko hata habari/mazungumzo mazuri. Kwa mfano, siku zote waigizaji wakiwa kazini watakufanya ujue kwamba “mambo ndivyo yalivyo”, kumbe wanaigiza tu na kupandikiza mbegu mbaya kwa watazamaji bila kujua. Hebu fikiri ni mara ngapi umetazama tamthilia/sinema, nk. jamabo likakugusa hadi machozi yakatoka? Je! Si maigizo tu? Umeona nguvu ya haya mambo katika nafsi yako?

Nisikilize vizuri hapa. Sikushauri utupe TV yako. Hapana, ila nataka nikufundishe jambo la kukusaidia. Kuna tofauti kubwa SANA kati ya mtu ambaye ni MSOMAJI wa Neno na MWOMBAJI, na mtu ambaye hasomi Neno wala sio mwombaji; hawa watu wawili wakikutana na mazungumzo mabaya, msomaji wa Neno na mwombaji yuko salama zaidi kwa sababu Neno lina takasa, Neno lina huisha; kila akisoma na kuomba, anatakaswa; mwenzake anabugia tu pumba na hakuna Neno wala maombi hapo. Je! N’nini matokeo baada ya muda mrefu? Usisahau, Daudi alisema “moyoni mwangu nimeliweka Neno lako nisikutende dhambi”, Hebu fikiri kama moyoni ni kutupu inakuwaje? Neno ndani yako lina nguvu ya kumulika na kuona hila za adui na kuipa nafsi yako nguvu ya kushinda. Tunaambiwa “hakuna kilichofichika kwa Neno”.

Kumbuka, ili usikutane na mazungumzo mabaya, imekupasa usikae duniani, lakini jua jambo hili, ukiwa msomaji wa Neno na Mwombaji, utakuwa salama. Mtu asiye soma Neno, wala haombi, ila yuko busy na kazi, shule, nk. kisha anabugia kila takataka, mpe miaka michache tu, atajikuta naye ni mtendaji wa hayo madudu hata kama ni mtoto wa askofu mkuu na amekulia kanisani.

Kuna jambo jingine hapa, Paulo analiita “kuukomboa wakati”. Paulo anasema, “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana” (Waefeso 5:15-17). Kama kuna kitu kitagharimu wengi ni ratiba za kila siku. Fikiri mtu anaamka asubuhi kuwahi kazini. Kwa sababu amechelewa kulala, basi amechelewa kuamka. Akiamka anakimbilia bafuni, kisha kukimbilia usafiri kuwahi kazini, BILA kuomba wala kusoma Neno. Sawa, sio wengi watapata muda wa kusoma Neno asubuhi. Mtu anaingia kwenye daladala, kabla hajakaa sawa, anasikia matusi yakivurumishwa kila kona, redioni kuna habari/mazungumzo mabaya, huku kwa dirishani wauza magazeti wanakuja na magazeti yenye “picha mbaya” ukurasa wa kwanza; kabla hujakaa sawa, macho yananasa kichwa cha habari cha gazeti la udaku, kabla hujagundua kinachoendelea, unajikuta unawaza ile habari mbaya ya udaku njia nzima hadi unafika ofisini.

Unafika ofisini, kabla hujakaa sawa unakutana na mlolongo wa kazi, ukishangaa ni jioni! Ukirudi nyumbani unakutana na tamthilia yako au zile sinema za Kinigeria zilizojaa uasherati na usaliti; kinachofuata unatafuta kitanda kilipo na kulala kama mfu, bila kuomba, bila Neno kwa sababu umejichokea. Mzunguko unaendela mwaka mzima. Sasa nisikilize vizuri, kama ukidumu namna hii, NAFSI yako umeilisha mazungumzo mabaya, mbinu za kumsaliti mpenzi wako, sinema za Kinigeria zimekufundisha jinsi watu wavyozini maofisini, maneno ya ngono kule ofisini, nk. Kabla hujakaa sawa, unaanza kuona hayo “mazungumo mabaya” ni vitu vya kawaida. Kidogo kidogo, na wewe unaanza kuchangia watu wakiongea hayo mazungumzo mabaya. Baada ya muda, “hao” watu unaoongea nao wanakuona “wewe ni mwenzao”, wanakurushia “neno”. Hujakaa sawa unaanza kufanya uchafu kama wao! Hapo ni wewe umejiachia kwa kutojua KUUKOMBOA wakati, ukajiweka kwenye mazingira mabaya, hukumtafuta Mungu wako katika maombi na Neno, ukawa dhaifu kabisa. Ghafla, unakuwa na wewe ni mwabudu sanamu, japo unajiita umeokoka. Kichwani yamejaa masinema ya Kinigeria na mbinu za kuiba wake/waume za watu!

Ibilisi anajua akikwambia uzini utamkemea, ila anakufundisha taratibu kwa kupitia mazungumzo mabaya, na kupitia “vitu vya kuvutia” kwenye vyombo vya habari (muziki, matangazo, nk.), na wewe unamsikiliza tu, bila kujua tabia yako anaathirika; baada ya miaka michache, jina lako linabadilika kutoka binti sayuni kuwa kahaba! Kumbe hukujua ni mazungumzo tu yamekubadili tabia yako.

Moja wapo wa namna ya kuukomboa wakati, ni kusoma Neno ukiwa mahali pa kusubiri kama kituoni, ukiwa kwenye usafiri, au muda wa mapumziko mafupi kazini, nk. Jiwekee malengo ya kusoma Neno kila siku, na utaona Mungu akikusaidia [kama unaona AIBU kusoma biblia hadharani, angalau basi weka biblia yako kwenye simu, ili ukisoma watu wasijue unafanya nini; japo hilo ni tatizo ambalo unahitaji kulishinda pia]. Jaribu kupata muda wa kuomba katikati ya ratiba ya siku. Kwa mfano, gawa muda wako wa lunch, jipatie dakika angalau 20 za kuomba tu, nk. Kama unapata muda wa kukandamiza ugali, au kuongea kwenye simu na “jamaa” zako, kwanini unakosa muda wa kuongea na Mungu? Tafakari, chukua hatua.

Mungu saidia kanisa lako.

Frank Philip.

Comments