NJIA MBILI ZA KUPITA MWANADAMU AMBAPO KILA MWANADAMU HUPITA MOJAWAPO KATIKA NJIA HIZO.



 
BWANA YESU asifiwe.


Karibu tena katika ujumbe huu ambao MUNGU amenipa kwa ajili ya kila mwanadamu kujua.


Katika maisha ya mwanadamu yeyote kuna njia mbili   ambapo moja kati ya hizo kila mwanadamu anapita.

Kila njia ina matokeo yake na kila  mwisho wa kila mwanadamu  huenda katika hitimisho la mojawapo ya njia hizi mbili.


Kuna njia ya uzima wa milele na kuna njia ya jehanamu ya  milele.

Mathayo 7:13-14 ( Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache. )


Hapa unapata njia mbili.



Kuna njia ya WOKOVU WA MILELE.

                  FURAHA YA MILELE.

                    UTUKUFU WA MILELE.



Pia kuna njia ya MATESO YA MILELE.

UPOTEVU WA MILELE.

KILIO CHA MILELE.



Kila mtu mwisho wake ni katika mojawapo ya njia hizi.


Kama wanadamu wote wangejua maana ya milele hakika wangeokoka wote.


Njia pana ambayo ni njia ya jehanamu ni njia ambayo huonekana kwa urahisi sana, ni njia ya dhambi za kila aina, ni njia ya wazinzi, ni njia ya walevi, ni njia ya waasherati, ni njia ya waongo, ni njia ya waabudu sanamu, ni njia ya freemasoni, ni njia ya wachawi, ni njia ya wala rushwa ni njia ambao hapa duniani inaonekana kama njia ya kuwafanya wanadamu waishi kwa starehe ya muda mfupi sana kama miaka 80 tu lakini wanadamu hawa hawa wanasahau furaha ya milele ambayo inapatikana katika KRISTO YESU pekee.


Njia nyembamba ambayo ni njia ya uzima wanadamu wengi hawaitaki, wanaoiona ni wachache sana, ni njia ambayo ukiiendea haukawii kuambiwa ‘’pole sana kwa kushindwa kuponda raha za dunia’’ ni njia ambayo watu watakusema kila neno baya kwa sababu tu umempokea BWANA YESU, lakini hii ndio njia ya uzima wa milele, duniani unaweza kuwa na dhiki lakini jipe moyo maana ufalme wa MUNGU ni wako, hii ni njia ambayo kuna wakati watenda dhambi watakucheka na kusema umechanganyikiwa, lakini ndio njia ya uzima. MUNGU amewapa urithi huu wa uzima wa milele hao hao ambao wanaonekana ni wanyonge wa duniani.



                                     NJIA YA UZIMA.




Luka 13:24 ( Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. ).

Wengi watataka kukingia lakini hawataweza maana watakuwa wamechelewa sana.

Lango la mbinguni likifungwa wote wali nje watataka kuingia lakini hawataweza.

Ni wachache hata leo wanaoiona njia hii ya uzima Yohana 10:7-9 ( Basi YESU aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo.  Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. ).

Ndugu yangu tunamhitaji YESU ili tupone.

Tunamhitaji BWANA YESU ili tuingie uzimani.

Tunamhitaji YESU KRISTO ili tukafurahi milele.

YESU ndio hiyo njia ya uzima wa milele (Yohana 14:6-YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi. ).

Hakuna mwingine ambaye kupitia kwake tunaweza kuupata uzima wa milele , Matendo 4:12 (Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. )



                 NJIA YA  MOTO WA MILELE.

 Waefeso 2:1-3 (Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;  ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;  ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. )

YESU kuwa BWANA na MWOKOZI wa maisha yako.Wateule wngi ambao kwa sasa wako katika njia ya uzima, zamani wote walikuwa katika njia ya jehanamu, na Biblia inafundisha kwamba ni marufuku kurudi nyuma tena , yaani kataa kurudi kwenye njia pana ,njia ya upotevuni , njia ya maangamizi maana wewe mteule sasa uko mahali salama maana umempokea

Mathao 7:13 ( Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. )

Huu ni upendo wa ajabu ambao MUNGU ametupenda yaani kutuletea ukombozi wa roho na miili yetu kupitia YESU KRISTO BWANA wetu, Ndugu zangu kila mmoja ajitahiti kupita katika mlango mwembamba.

Mathayo 19:24 ( Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa MUNGU).


MUNGU hataki yeyote kati yetu aende njia hii ya jehanamu.

Ndugu yangu unayesoma ujumbe huu, mbele yako kuna UZIMA na MAUTI  nakushauri chagua UZIMA kwa kumpokea BWANA YESU leo. 
Mbele yako kuna BARAKA na LAANA  chagua BARAKA yaani kumpokea BWANA YESU leo.

Kumb 30:19 ( Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; ).


Naamini baada ya kusoma ujumbe huu umechagua kabisa njia ya kupita ukiwa duniani yaani kuishi huku ukiwa na YESU mwenye uzima na kukataa dhambi zote. Mimi naamini umechagua UZIMA. 


Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                 MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments