uwe wa ndani
kuliko dhati yangu yenyewe.
Wewe, kielelezo cha uzuri
wowote na asili ya utakatifu wote,
uchonge moyo
wangu kadiri ya sura yako;
uuchonge kwa nyundo ya huruma yako, Mungu wa moyo wangu
na urithi wangu, Ee
Mungu, heri yangu ya milele. Amina.
MT. YOHANE WA DAMASKO (645-750)
|
Wewe, Bwana, ulinitoa katika viuno vya baba yangu;
|
Nakusihi, Bwana, nguvu
yenye moto na tamu ya upendo wako
iondoe akili yangu mbali na vitu vyote vilivyopo chini ya
mbingu,
ili nife kwa kupenda upendo wako,
wewe uliyeona inafaa
ufe kwa kupenda upendo wangu.
|
MT. FRANSISKO WA ASIZI (1181-1226)
|
BABA YETU mtakatifu kabisa:
muumba,
mkombozi, mfariji na mwokozi wetu.
ULIYE MBINGUNI:
katika malaika na katika watakatifu,
ukiwaangazia wawe na
ufahamu, kwa sababu wewe Bwana ni mwanga;
ukiwawasha wawe na
upendo, kwa sababu wewe Bwana ni upendo;
ukikaa ndani mwao na
kuwajaza furaha, kwa sababu wewe Bwana
ni wema mkuu kabisa, wema wa milele,
ambaye kwako hutoka
mema yote, na bila yako hakuna jema.
JINA LAKO LITUKUZWE:
ujuzi wetu juu yako uwe wazi zaidi na zaidi,
tuweze kujua
upana wa baraka zako, urefu wa ahadi zako,
kimo cha ukuu wako, kina cha hukumu zako.
UFALME WAKO UFIKE:
utawale ndani yetu kwa njia ya neema yako
na kutuwezesha
kuingia katika ufalme wako ambapo
unaonekana
kama ulivyo, unapendwa kikamilifu,
unatia heri ya kukaa
nawe, unatia raha ya kukufurahia milele.
UTAKALO LIFANYIKE
DUNIANI KAMA MBINGUNI: tuweze kukupenda
kwa moyo wetu
wote, kwa kukuwaza wewe daima;
kwa roho yetu
yote, kwa kukutamani wewe daima;
kwa akili yetu
yote, kwa kuelekeza nia zetu zote kwako
na kwa
kutafuta utukufu wako katika yote;
kwa nguvu zetu
zote pia, kwa kutumia uwezo na hisia zote
za roho na mwili katika
kuhudumia upendo wako na si chochote kingine;
na tuweze
kuwapenda majirani wetu kama tunavyojipenda,
kwa kuwavuta wote
kwa nguvu zetu zote kwenye upendo wako,
tukifurahia mema ya
wengine kama tunavyofurahia ya kwetu,
na tukihuzunika
pamoja na wengine kwa mabaya yanayowafikia,
bila ya kumuudhi yeyote.
MKATE WETU WA KILA SIKU: Mwanao mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo.
UTUPE LEO:
kwa ukumbusho, ufahamu na heshima
ya
upendo ule aliokuwanao kwetu sisi
na ya mambo yale ambayo alisema na kutenda na kuteseka kwa ajili
yetu.
|
ONGEA NA MUNGU
WAKO.
UTUSAMEHE MAKOSA
YETU: kwa huruma yako isiyosemeka,
kwa nguvu ya
mateso ya Mwanao mpendwa,
pamoja na stahili
na maombezi ya Bikira mbarikiwa daima
na ya wateule wako wote.
KAMA
TUNAVYOWASAMEHE NA SISI WALIOTUKOSEA:
na
lolote tusilosamehe kikamilifu,
wewe Bwana
utuwezeshe kulisamehe kabisa,
tuwapende
kweli maadui wetu kwa ajili yako,
na tuwaombee kwa bidii mbele zako, bila ya kumlipa yeyote ovu
kwa ovu,
bali
tukijitahidi kumsaidia kila mmoja katika wewe.
NA USITUTIE KATIKA
VISHAWISHI: kilichofichika au cha wazi,
cha
ghafla au cha muda mrefu.
LAKINI UTUOPOE
MAOVUNI: yaliyopita, ya sasa na yajayo.
ATUKUZWE BABA
NA MWANA NA ROHO MTAKATIFU
KAMA MWANZO,
NA SASA NA MILELE. AMINA.
|
Ndiwe Bwana Mungu
mtakatifu unayetenda maajabu.
Wewe una nguvu. Wewe
ni mkuu. Wewe ndiwe mkuu kabisa.
Wewe
ndiwe mfalme mwenyezi.
Wewe, Baba
mtakatifu, mfalme wa mbingu na nchi.
Wewe ni utatu na
umoja, Bwana Mungu wa miungu;
ndiwe wema, wema wote, wema mkuu, Bwana Mungu hai na wa kweli.
Wewe ni pendo, upendo;
wewe ni hekima, wewe ni unyenyekevu,
wewe ni uvumilivu, wewe
ni uzuri, wewe ni upole, wewe ni usalama,
wewe ni utulivu, wewe
ni furaha na heri, wewe ni tumaini letu,
wewe ni haki, wewe ni
kiasi, wewe ni mali yetu yote ya kututosha.
Wewe ni uzuri, wewe
ni upole, wewe ndiwe msimamizi,
wewe ni mlinzi na mtetezi
wetu, wewe ni nguvu, wewe ni burudisho.
Wewe ni tumaini letu,
wewe ni imani yetu, wewe ni upendo wetu,
wewe ni utamu wetu
wote, wewe ni uzima wetu wa milele:
Bwana mkuu na wa ajabu, Mwenyezi Mungu, Mwokozi mwenye huruma.
|
MT. ELIZABETI WA HUNGARIA (1207-1231)
|
Bwana, ukitaka kuwa pamoja nami,
mimi nataka kuwa pamoja
nawe,
nisitake kutengana nawe
kamwe.
|
Asante kwako, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa fadhili zote
ulizonistahilia.
Kwa mateso na matusi
yote uliyoyavumilia kwa ajili yangu.
Mkombozi, rafiki
na kaka mwenye huruma nyingi,
naomba niweze kukufahamu
wazi zaidi, kukupenda kwa hisani zaidi,
kukufuata
kwa karibu zaidi, siku kwa siku.
|
MT. BONAVENTURA (1217-1274)
|
Lo, uzuri usiosemeka wa
Mungu mkuu,
lo, mng’ao safi kabisa wa nuru ya milele!
Wewe ni uhai
unaohuisha kila uhai,
mwanga unaoangaza kila
mwanga!
|
Bwana Yesu Kristo,
unichome mpaka kiini cha moyo wangu
kwa donda lile
tamu la kuletea wokovu la upendo wako.
Unijaze kwa ule
upendo motomoto, mnyofu na mtulivu
uliomfanya
mtume wako mtakatifu Paulo
atamani
kutengwa na mwili wake awe nawe.
Roho yangu ikuonee shauku, ikijaa daima hamu ya makao yako ya
milele.
|
MT. THOMA WA AKWINO (1225-1274)
|
Mungu wa wema wote, utujalie tutamani motomoto, tutafute kwa
busara,
tujue kwa hakika na
kutekeleza kikamilifu matakwa yako matakatifu
kwa utukufu wa jina lako.
|
M.H. ANJELA WA FOLIGNO (1248-1309)
|
Mungu
wangu, unijalie kujua fumbo kuu
linalotokana
na moto wa upendo wako usiosemeka
na wa Nafsi tatu za Utatu,
yaani
fumbo la umwilisho wako mtakatifu
uliotaka kutekeleza kwa ajili yetu.
Ndio mwanzo wa wokovu wetu
nao
unatenda mambo mawili ndani mwetu:
kutujaza
upendo na kutuhakikishia ukombozi wetu.
Lo, upendo
usioweza kueleweka kwa yeyote!
Hakuna upendo mkuu kuliko huo:
Mungu wangu
amejifanya mtu anifanye niwe Mungu!
Lo, upendo la kupita kiasi:
umejiharibu ili
kunitengeneza wakati ulipotwaa mwili wetu.
Si kwamba wewe au
umungu wako umekuja kupungukiwa kitu,
ila kina cha umwilisho wako kinanitoa midomoni maneno yenye
hisia kali!
Wewe,
usiyeeleweka, umejifanya wa kueleweka;
wewe
usiyeumbwa umejifanya kiumbe;
wewe
usiyefikirika, umekuja kufikirika;
wewe Roho tupu
umekubali kuguswa na mikono ya watu!...
Ee Mkuu kabisa, uniwezeshe kuelewa zawadi hiyo ipitayo nyingine
yoyote:
malaika
na watakatifu wote heri yao pekee
ni
kukuona, kukupenda na kukutazama!
Ee
zawadi ya juu kuliko yoyote,
kwa kuwa wewe
ndiwe zawadi yenyewe, ndiwe Upendo!
|
Ee Wema mkuu, umekubali kujulikana kama Upendo,
na unatufanya
tuupende Upendo huo.
Wale wote watakaofika
mbele yako watapata raha
kadiri ya upendo
waliokuwanao kwako.
|
Mungu, unayestahili
upendo usio na mipaka,
sina chochote cha kupimia
vema ukuu wako,
lakini hamu yangu kwako
ni hivi kwamba,
kama ningekuwa na yale yote uliyonayo wewe,
ningekupa yote kwa
furaha na shukrani.
|
Kwa ajili ya
uongofu nakutolea, Baba mpenzi sana,
mateso yote ya Mwanao
mpendwa sana tangu wakati ule ambapo,
akilazwa horini juu
ya nyasi, alianza kulia, halafu akavumilia
mahitaji ya utoto,
mapungufu ya ubalehe, mateso ya ujana,
hadi alipoinamisha
kichwa akafa msalabani kwa mlio mkubwa.
Vilevile, kwa
kufidia makosa yangu ya uzembe, nakutolea,
Baba mpenzi sana,
mwendo wote wa maisha matakatifu sana
ambayo Mwanao
pekee aliyaishi kikamilifu kabisa
katika
mawazo, maneno na matendo yake
tangu atumwe kutoka ukuu wa kiti chako cha enzi kuja katika
dunia yetu,
hadi
alipouonyesha mtazamo wako wa Kibaba
utukufu wa mwili wake mshindi.
Kama shukrani nazama
katika kilindi kirefu sana cha unyenyekevu,
na
pamoja na huruma yako isiyolipika,
nasifu na kuabudu wema wako mtamu
sana.
Wewe, Baba wa huruma,
nilipokuwa ninapoteza maisha yangu hivyo,
ulikuza
kwangu mawazo ya amani, si ya mabaya,
ukaamua
kuniinua kwa wingi na ukuu wa fadhili zako.
Kati ya mengine, ulitaka
kunijalia ujirani usiothaminika wa urafiki wako
kwa kunifungulia kwa namna mbalimbali hazina ile azizi sana ya
umungu,
ambayo
ni moyo wako wa Kimungu,
na kwa kunitolea kwa
wingi mkubwa kila utajiri wa furaha ndani yake.
|
Usifiwe, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kuwahi kutabiri kifo
chako,
kwa kugeuza kwa namna ya
ajabu, katika karamu ya mwisho,
mkate wa
kawaida uwe mwili wako mtukufu,
kwa
kuwagawia mitume kwa upendo
kama ukumbusho
wa mateso yako mastahivu,
kwa kuwaosha miguu kwa
mikono yako mitakatifu na azizi,
ukionyesha hivyo ukuu
usio na mipaka wa unyenyekevu wako.
Heshima kwako,
Bwana wangu Yesu Kristo,
|
kwa kutoka jasho la
damu katika mwili wako usio na kosa
kwa hofu ya mateso na kifo,
na kwa kutekeleza hata
hivyo ukombozi wetu uliotamani kuutimiza,
ukionyesha
hivyo wazi upendo wako kwa binadamu.
Usifiwe, Bwana wangu
Yesu Kristo, kwa kupelekwa kwa Kayafa
na kuruhusu kwa
unyenyekevu wako uhukumiwe na Pilato,
wewe uliye hakimu wa wote.
Utukufu kwako, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kudhihakiwa pale
ambapo,
kisha kuvikwa nguo ya
zambarau, ulitiwa taji la miba mikali sana,
na kwa
kuvumilia kwa subira isiyo na mipaka kwamba
uso wako
mtukufu ujae mate, macho yako yafunikwe,
mashavu yako yapigwe kwa
nguvu na mikono ya kikafiri ya watu waovu.
Sifa
kwako, Bwana wangu Yesu Kristo,
kwa kuruhusu kwa
uvumilivu mkubwa ufungwe kwenye nguzo,
upigwe mijeledi kinyama,
upelekwe
mahakamani kwa Pilato umejaa damu,
uonekane kama mwanakondoo
asiye na kosa anayepelekwa machinjoni.
Heshima
kwako, Bwana wangu Yesu Kristo,
kwa kukubali
kuhukumiwa katika mwili wako mtakatifu,
uliojaa tayari damu, ufe msalabani;
kwa kubeba kwa uchungu
msalaba juu ya mabega yako matakatifu,
na kwa kutaka
kupigiliwa misumari katika mbao za adhabu,
kisha kuburutwa kikatili
hadi mahali pa mateso na kuvuliwa nguo zako.
Heshima kwako, Bwana Yesu Kristo,
kwa kuelekeza
kwa unyenyekevu, kati ya mateso hayo,
macho yako yaliyojaa
upendo na wema kwa Mama yako mstahivu sana,
ambaye
hajawahi kupatwa na dhambi
wala
kukubali kosa dogo namna gani,
na kwa kumfariji ukimkabidhi kwa ulinzi mwaminifu wa mwanafunzi
wako.
Uhimidiwe
milele, Bwana wangu Yesu Kristo,
kwa kuwapa
wakosefu wote, wakati wa kihoro chako,
tumaini la
msamaha ulipomuahidia kwa huruma
utukufu wa
paradiso mhalifu aliyekukimbilia.
Sifa ya
milele kwako, Bwana wangu Yesu Kristo,
kwa kila saa
uliyovumilia msalabani kwa ajili yetu wakosefu
machungu na mateso makubwa kabisa;
kwa kuwa
uchungu mkali sana wa majeraha yako
ulikuwa
ukipenya vibaya mno roho yako yenye heri
na kuchoma
kikatili moyo wako mtakatifu sana,
mpaka pale ambapo, moyo
ukishindwa kazi, ulitoa kwa heri roho yako
na, kisha kuinamisha kichwa,
uliikabidhi kwa
unyenyekevu wote mikononi mwa Mungu Baba,
ukabaki mfu, ukiwa na mwili
baridi.
Usifiwe, Bwana wangu Yesu Kristo,
kwa kukomboa
roho za watu kwa damu yako azizi
na
kwa kifo chako kitakatifu sana,
|
na kwa kuzirudisha kwa huruma katika uzima wa milele toka
uhamishoni.
Usifiwe, Bwana wangu Yesu Kristo,
kwa kukubali mkuki
ukuchome ubavu na moyo kwa wokovu wetu,
na kwa damu azizi na maji
vilivyobubujika
kutoka ubavu huo kwa ukombozi wetu.
Utukufu
kwako, Bwana wangu Yesu Kristo,
kwa kutaka mwili
wako mbarikiwa ushushwe toka msalabani
kwa
mikono ya marafiki wako,
ukabidhiwe mikononi mwa
Mama mwenye huzuni na kuvikwa naye,
halafu ufungwe
katika kaburi na kulindwa na askari.
Heshima ya
milele kwako, Bwana wangu Yesu Kristo,
kwa
kufufuka kutoka wafu siku ya tatu
na kwa
kukutana hai na wale uliowachagua;
kwa kupaa mbinguni,
siku arubaini baadaye, ukitazamwa na wengi
na kwa kutawaza huko juu kwa heshima marafiki wako uliowatoa
kuzimu.
Shangwe na sifa
ya milele kwako, Bwana Yesu Kristo,
kwa kumtuma Roho
Mtakatifu mioyoni mwa wanafunzi
na kwa
kushirikisha roho zao upendo mkuu wa Kimungu.
Uhimidiwe, usifiwe
na kutukuzwa milele, Bwana wangu Yesu,
uliyeketi katika kiti
che enzi kwenye ufalme wako wa mbinguni,
katika utukufu wa enzi yako,
mwenye mwili hai
pamoja na viungo vyako vitakatifu vyote,
ulivyovitwaa kutoka mwilini mwa Bikira.
Hivyo utakuja siku ya hukumu
uhukumu
roho za wote walio hai na waliokufa:
wewe unayeishi na kutawala pamoja na Baba
na Roho Mtakatifu
daima na milele. Amina.
|
SALA KUTOKA ASSISI (Karne
XIV)
|
Salamu, Bwana Yesu
Kristo, Neno wa Baba, Mwana wa Bikira,
Mwanakondoo wa Mungu,
wokovu wa ulimwengu, Hostia takatifu,
Neno
uliyefanyika mwili, chemchemi ya wema.
Salamu, Bwana Yesu
Kristo, sifa za malaika, utukufu wa watakatifu,
mandhari ya
amani, Mungu mzima, mtu kweli,
chipukizi na tunda la Mama Bikira.
Salamu, Bwana Yesu Kristo, mng’ao wa Baba,
mfalme wa amani,
mlango wa
mbingu, utukufu wa ufalme, mkate hai,
uliyezaliwa
na Bikira, chombo cha Umungu.
Salamu, Bwana Yesu Kristo, mwanga wa mbingu, msingi wa
ulimwengu,
furaha yetu, mkate wa malaika,
furaha ya moyo,
mfalme na bwanaarusi wa ubikira.
Salamu, Bwana Yesu
Kristo, njia tamu, ukweli safi, upendo mkuu,
tuzo letu, chemchemi ya
upendo, amani ya wema, pumziko halisi,
uzima wa milele,
ambapo baada ya unyonge wa sasa
wewe utujalie
kutuburudisha kwa uso wako, Mungu wa miungu,
|
mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana, daima na milele. Amina.
|
SALA NYINGINE YA KARNE XIV
|
Roho ya Kristo,
unitakase.
Mwili wa Kristo,
uniokoe.
Damu ya Kristo,
unilevye.
Maji ya ubavu wa
Kristo, unioshe.
Mateso ya Kristo,
yanitie nguvu.
Ee Yesu mwema,
unisikilize.
Katika madonda yako
unifiche.
Usikubali nitengane
nawe.
Na adui mwovu unikinge.
Saa ya kufa kwangu
uniite.
Uniamuru nije
kwako,
nikutukuze pamoja na Watakatifu wako,
milele na milele.
Amina.
|
MT. KATERINA WA SIENA (1347-1380)
|
Mungu wa
milele, Utatu wa milele,
umefanya damu ya Kristo iwe azizi kabisa kwa kushiriki umungu
wako.
Wewe ni
fumbo la kina kuliko bahari;
kadiri ninavyotafuta
naona; na kadiri ninavyoona nakutafuta.
Siwezi kamwe kushiba; ninachopokea kitanifanya daima nitamani
zaidi.
Unapojaza roho yangu nazidi
kuonea njaa na shauku mwanga wako.
Hasa natamani
kukuona wewe, mwanga halisi, jinsi ulivyo.
Ndiwe muumba wangu,
Utatu wa milele, nami ni kiumbe chako.
Umenifanya
kiumbe kipya katika damu ya Mwanao,
nami najua unavutwa na
uzuri wa kiumbe chako kutokana na upendo.
|
Bwana wangu, elekeza
jicho la huruma yako juu ya taifa lako
na juu ya
mwili wa fumbo wa Kanisa takatifu.
Wewe utatukuzwa zaidi sana kwa kusamehe na kuwaangazia akili
wengi,
kuliko kwa kupokea
heshima toka kwa kiumbe mmoja duni,
kama nilivyo
mimi, ambaye nilikukosea sana
na kuwa sababu
na chombo cha maovu mengi.
Ingenitokea nini kama ningeona mimi ni hai, na watu wako
wamekufa?
Ingekuwaje kama ningeliona gizani,
kutokana na
dhambi zangu na za viumbe wengine,
Kanisa lako, Bibiarusi
wako mpenzi, lililozaliwa liwe mwanga?
Basi,
nakuomba huruma kwa taifa lako
kwa ajili ya ya
upendo usioumbwa uliokusukuma wewe
umuumbe mtu kwa sura na mfano wako.
Sababu gani ilikufanya
umweke mtu katika heshima kubwa hivyo?
Bila ya shaka
ni upendo ule usiothaminika ambao
|
ulimuangalia kiumbe
chako ndani mwako ukachanganyikiwa naye.
Lakini baadaye kwa dhambi aliyoitenda akapoteza ukuu huo
uliomuinulia.
Ukisukumwa
na moto huohuo ambao ulituumba,
ulipenda
kuwatolea binadamu njia ya kupatanishwa nawe.
Ndiyo
sababu umetupatia Neno, Mwanao pekee.
Amekuwa mshenga kati yako na sisi,
amekuwa haki
yetu aliyeadhibu ndani mwake maovu yetu.
Alitii agizo ambalo
wewe, Baba wa milele, ulimpa ulipomvika utu wetu.
Lo, kilindi cha upendo!
Moyo upi hautajaa mhemko kwa kuona ukuu huo
kushukia unyonge mkubwa kama huu, yaani
ubinadamu wetu?
Sisi
ni mfano wako, nawe mfano wetu
kutokana na
muungano uliouanzisha kati yako na binadamu,
ukifunika umungu wa milele
kwa wingu
maskini la utu ulioharibika wa Adamu.
Kwa
sababu gani? Bila ya shaka kwa upendo.
Kwa upendo huo
usiosemeka nakuomba na kukuhimiza
uwawie huruma viumbe wako.
|
JULIANA WA NORWICH (1342-1413)
|
Ee Mungu wa wema
wako, unipatie wewe mwenyewe,
kwa kuwa
wewe unanitosha.
Siwezi kuomba vema
chochote kingine ili nikustahili wewe.
Ningeomba chochote kidogo kuliko wewe ningekuwa mhitaji daima,
kwa sababu
ndani mwako tu nina kila kitu.
|
THOMAS WA KEMPIS (1379-1471)
|
Ee Bwana,
unangurumisha hukumu zako juu yangu,
na kutikisa
mifupa yangu yote kwa hofu na tetemeko.
Roho
yangu imeshtuka sana.
Nabaki nimeduwaa na kuzingatia mbingu zenyewe si safi machoni
pako.
Kama uliona kasoro katika
malaika usiwaachilie, itakuwaje kwangu?
Nyota za mbinguni
zilianguka, nami, mavumbi, natarajia nini?
Watu kadhaa
walioonekana wenye mwenendo bora
walianguka chini kabisa;
na mtu aliyekula mkate wa
malaika,
baadaye nikamuona
kufurahia vyakula vya nguruwe.
Basi, hakuna utakatifu
wowote, ukiondoa mkono wako, Bwana.
Hakuna hekima
inayofaa, ukiacha kutawala wewe.
Hakuna nguvu inayosaidia,
ukiacha kutegemeza.
Tukiachwa, tunazama na kufa.
Kumbe
tukitembelewa, tunainuka na kuishi.
Hatuna
msimamo, lakini wewe unatuimarisha.
Tunapoa,
lakini wewe unatuwasha tena.
Majivuno yoyote yanamezwa
na kilindi cha hukumu zako juu yangu.
|
Mwili
wowote ni nini mbele yako?
Je, udongo
utajivuna dhidi ya mfinyanzi?
Anawezaje kupotea katika majivuno mtu ambaye anahisi sana ukweli
na
kukaa chini ya Mungu?
Ulimwengu wote
hauwezi kumtia kiburi mtu
anayejiona
kutawaliwa na sheria ya ukweli,
wala midomo ya
walaghai wote haitamsogeza mtu
aliyeweka
tumaini lake lote kwa Mungu.
Wale wenyewe
wanaosema si kitu vilevile;
Watatoweka
pamoja na sauti ya maneno yao:
kumbe,
“Uaminifu wa Bwana ni wa milele”.
|
Bwana Yesu, kadiri maisha yako yalivyodharauliwa na ulimwengu,
utujalie
tukuige hivi kwamba,
tukiwa na picha yako
daima mbele ya macho yetu,
hata kama
ulimwengu unatudharau,
tujifunze kwamba
watumishi wa msalaba tu
wanaweza kuona njia ya
heri halisi na mwanga wa kweli.
|
MT. NIKOLA WA FLUE (1417-1487)
|
Bwana, uniondolee yale yote yanayonizuia nisifike kwako;
unijalie yale yote
yanayoweza kunifikisha kwako;
ujichukulie nafsi yangu,
na kujipatia kabisa mwenyewe.
|
MT. THOMAS MORE (1478-1535)
|
Bwana mwema, utujalie neema ya kuyafanyia kazi yale
tunayokuomba.
|
MT. INYASYO WA LOYOLA (1491-1556)
|
Pokea,
Bwana, hiari yangu yote.
Pokea
kumbukumbu, akili na utashi wote.
Vyovyote
nilivyonavyo au kuvimiliki nimejaliwa na wewe:
nakurudishia vyote
na kuukabidhi utashi wako uvitawale.
Unijalie tu upendo wako na neema yako, nami nitakuwa tajiri
kutosha,
nisitamani kitu kingine chochote.
|
M.H. PETRO FAVRE (1506-1546)
|
Ee Yesu Kristo, kifo
chako kiwe uhai wangu;
nijifunze kuona
uhai katika kifo chako.
Uchovu wako
uwe pumziko langu,
udhaifu wako wa
kibinadamu uwe nguvu yangu.
Kudhalilishwa kwako kuwe chemchemi ya utukufu wangu,
mateso yako raha yangu,
huzuni yako furaha yangu.
|
Kujishusha
kwako kuniinue:
kwa ufupi, machungu yako yawe yote nilivyonavyo.
|
MT. FRANSISKO SAVERI (1506-1552)
|
Ee Mungu
wa mataifa yote ya dunia,
uukumbuke
umati wa Wapagani ambao,
ingawa
waliumbwa kwa sura yako,
hawajakufahamu wewe wala kifo cha Mwanao Yesu Kristo, mwokozi
wao.
Fanya kwamba, kwa
sala na kazi za Kanisa lako takatifu,
wakombolewe kutoka
ushirikina wote na utovu wa imani
wakaletwe kwenye ibada zako.
Kwa njia ya yule
uliyemtuma awe ufufuo na uzima wa watu wote,
huyo
Mwanao Yesu Kristo, Bwana wetu.
|
MT. LUDOVIKO BERTRANDO (1526-1581)
|
Bwana, unichome moto hapa duniani, na kunikausha hapa duniani,
ili
unihurumie milele.
|
MT. TERESA WA YESU (1515-1582)
|
Bwana wangu, je,
hukuweza kujumlisha yote katika neno moja
na kusema,
“Baba, utupe yote tunayoyahitaji”?
Kwa yule anayejua yote
vizuri kabisa, inaonekana haihitajiki zaidi.
Lo, hekima ya milele!
Kwako na kwa Baba yako hiyo ingetosha,
na kweli ndivyo
ulivyosali katika bustani la Getsemane:
ulionyesha matakwa na hofu yako, lakini ukajiachilia kwa matakwa
yake.
Hata hivyo kwa kuwa
unajua hatuko tayari kama wewe, Bwana wangu,
kutii matakwa ya Baba
yako, ilikubidi ubainishe vizuri maombi,
tuweze kuona
kama tunayoyaomba yanatufaa,
na
tujizuie kuomba tukiona haitufai.
Kwa sababu ndivyo
tulivyo kwamba, tusipopewa tunayotamani,
kwa hiari yetu
tunayakataa tunayopewa na Bwana,
hata yakiwa mambo bora.
Kwa kuwa hatujioni
matajiri mpaka tushike fedha mikononi.
|
Bwana wangu, kwa hakika saa niliyoitamani sana hatimaye imefika.
Kwa hakika
wakati wa sisi kuonana umefika.
Bwana na mwokozi wangu, kwa hakika huu
ni wakati
wa mimi kuchukuliwa
kutoka uhamisho huu niwe nawe milele.
Dhabihu za
Mungu ni roho iliyovunjika;
moyo uliovunjika na
kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.
Usinitenge na uso wako,
wala roho yako
mtakatifu usiniondolee.
Ee Mungu,
uniumbie moyo safi.
|
MT. YOHANE WA MSALABA (1542-1591)
|
Roho yangu ni kavu ndani mwangu kwa sababu imesahau kujilisha
wewe.
|
MT. MARIA MAGDALENA WA PAZZI (1566-1607)
|
Neno, wewe ni
wa ajabu katika Roho Mtakatifu pia,
ukimfanya
ajimimine katika roho hivi kwamba
roho inakuja kuungana na
Mungu, inamjua Mungu, inamuonja Mungu,
haifurahii chochote isipokuwa Mungu.
Na
Roho Mtakatifu anakuja rohoni
imetiwa daima mhuri azizi ya Damu ya Neno, Mwanakondoo
aliyechinjwa;
tena
damu ndiyo inayomsukuma aje,
ingawa
mwenyewe anakuja kwa kutaka…
Roho
Mtakatifu, huishii katika Baba asiyebadilika,
wala huishii katika Neno;
ingawa umo
daima ndani ya Baba, ndani ya Neno,
ndani mwako na
ndani ya roho zote zenye heri mbinguni
na ndani ya viumbe.
Unahitajiwa na kiumbe
kutokana na damu iliyomwagwa na Neno,
Mwana
pekee, ambaye kwa ari ya upendo
amejifanya ahitahiwe na kiumbe chake.
Unapumzika katika
viumbe vilivyojiandaa kupokea ndani mwao,
kwa
kushirikishwa vipaji vyako, mfano wako kwa usafi.
Unapumzika ndani ya
wale wanaopokea tunda la damu ya Neno
na
kujifanya maskani ya kukufaa.
Njoo, Roho Mtakatifu.
Uje muungano
na Baba, faraja ya Neno.
Roho wa ukweli,
ndiwe tuzo la watakatifu, burudisho la roho,
mwanga wa giza,
utajiri wa mafukara, hazina ya wenye upendo,
shibe ya
wenye njaa, faraja ya wanaohiji;
basi ndiwe mwenye hazina zote.
Njoo wewe ambaye, kwa
kumshukia Maria, ulimfanya Neno awe mwili,
fanya
tena ndani mwetu kwa neema
kile
ulichomfanyia Maria kwa neema na maumbile.
Njoo, uliye lishe
ya kila wazo safi, chemchemi ya kila wema
na fungu la usafi wote.
Njoo, uteketeze
ndani mwetu yale yote yanayotufanya
tusiweze kuteketea ndani mwako.
|
MT. FRANSISKO SOLANO (1549-1610)
|
Yesu mwema,
mkombozi na rafiki yangu!
Nina kitu gani usichonipa wewe? Najua nini usiyonifundisha wewe?
Nina
thamani gani usipokuwa nami?...
|
Ndiwe uliyeniumba, tena bila ya kuniuliza. Wewe umeniumba.
Elekeza macho yako
kwangu, Bwana, na unihurumie,
kwa kuwa mimi
ni mkiwa na maskini…
Kwa nini, Bwana Yesu
wangu, wewe umesulubiwa,
nami
nasaidiwa na watumishi wako?
Kwa nini wewe
uchi, nami nina vazi?
Kwa nini wewe umepigwa
makofi na kutiwa taji la miba,
nami nimepewa vitu vyema
na kufarijiwa na fadhili nyingi?...
Mungu wa roho yangu,
utukuzwe kwa yale uliyonijalia!
Bwana wangu, nafurahi kwamba u Mungu; jinsi hilo lilivyo zuri!
|
MT. ROBERTO BELLARMINO (1542-1621)
|
Wewe, Bwana, u
mwema, umekuwa tayari kusamehe,
na mwingi wa
fadhili, kwa watu wote wakuitao;
nani hatakutumikia kwa moyo wote baada ya kuanza kuonja walau
kidogo
utamu
wa mamlaka yako ya Kibaba?
Unawaagiza nini watumishi wako, Bwana?
Unasema,
Jitieni nira yangu. Na nira yako ikoje?
Unasema, Nira
yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.
Nani hatabeba kwa moyo
radhi kabisa nira isiyobana bali inapendeza,
na
mzigo usiolemea, bali unainua?
Kwa hiyo umeongeza kwa
haki, Nanyi mtapata raha nafsini mwenu.
Na ikoje nira yako
hiyo ambayo haichoshi, bali inapumzisha?
Kwa hakika
ndiyo amri ya kwanza tena kuu,
Mpende Bwana
Mungu wako kwa moyo wako wote.
Nini ni rahisi, nono na
tamu kuliko kupenda wema, uzuri na upendo?
Na hayo yote
ndiwe wewe, Bwana Mungu wangu.
Nawe unafikia hatua ya
kuahidi tuzo kwa wale wanaoshika sheria zako,
ingawa tayari
zenyewe ni za thamani kuliko dhahabu nyingi,
na
tamu kuliko sega la asali?
Ndiyo,
unaahidi kweli tuzo, tena tuzo kubwa mno.
|
MT. FRANSISKO WA SAL (1567-1622)
|
Ee
Mungu wangu, nakutolea siku hii.
Nakutolea
sasa mema yote nitakayotenda
na ninakuahidi nitapokea kwa upendo wako magumu yote
yanayonikabili.
Unisaidie
kuenenda siku hii namna inayokupendeza.
|
Ee Bwana, mimi ni
wako, tena natakiwa kuwa wako tu,
si wa
mwingine yeyote.
Roho yangu ni wako, nayo
inatakiwa iishi kwa njia yako tu.
Utashi wangu ni wako,
nao unatakiwa kupenda kwa ajili yako tu.
Napaswa kukupenda kama asili yangu kuu, kwa kuwa natoka kwako.
Napaswa kukupenda
kama lengo na pumziko langu,
|
kwa kuwa nipo
kwa ajili yako.
Napaswa kukupenda
kuliko nafsi yangu,
kwa kuwa nafsi
yangu inatoka kwako.
Napaswa kukupenda
kuliko mimi mwenyewe,
kwa kuwa mimi mzima ni wako na ndani yako. Amina.
|
MT. YOHANE WA BREBEUF (1593-1649)
|
Ee Mungu wangu,
jinsi ninavyosikitika kwamba hujajulikana,
na kwamba
katika makabila haya yasiyostaarabika
wachache tu
wameikumbatia imani yako!
Dhambi
haijatoweka, nawe hujapendwa!
Naam, Mungu wangu,
ikiwa mateso yote ambayo katika nchi hizi
mateka wanaweza
kupatwa nayo, pamoja na ukatili wa adhabu,
zitatakiwa kumwagika juu yangu,
niko tayari kwa moyo wote kuyapokea na kuyavumilia hata peke
yangu.
|
SALA ILIYOSAMBAZWA KWA JINA LA KLEMENTI XI
|
Nasadiki, Bwana, lakini nisadiki
kwa imara zaidi;
natumaini, lakini nitumaini kwa hakika zaidi;
napenda, lakini nipende kwa ari zaidi;
nasikitika, lakini nisikitike kwa nguvu zaidi.
Nakuabudu kama asili
ya vyote; nakutamani kama lengo kuu;
nakusifu kama mfadhili
wa kudumu; nakulilia kama mtetezi wa kufaa.
Uniongoze kwa
hekima yako, unidhibiti kwa haki yako,
unifariji kwa
wema wako, unilinde kwa uwezo wako.
Bwana, nakutolea ya kuwaza ili
yakuelekee wewe,
ya kusema yakuhusu wewe,
ya kufanya yawe kadiri yako,
ya
kuvumilia yake kwa ajili yako.
Nataka chochote
unachotaka, nataka kwa sababu unataka,
nataka jinsi
unavyotaka, nataka mpaka utakapotaka.
Naomba,
Bwana: angaza akili, washa utashi,
safisha moyo, takasa roho.
Nilie juu ya maovu
yaliyopita, nifukuze vishawishi vijavyo,
nirekebishe
maelekeo mabaya, nistawishe maadili ya kufaa.
Mungu mwema,
unipatie upendo kwako, chuki kwangu,
ari
kwa jirani, dharau kwa ulimwengu.
Nijitahidi
kutii wakubwa, kusaidia walio chini yangu,
nishauri marafiki, nisamehe maadui.
Nishinde tamaa kwa
maisha magumu, uroho kwa ukarimu,
hasira kwa
upole, uvuguvugu kwa umotomoto.
Unifanye niwe na busara katika maamuzi, niwe na msimamo katika
hatari,
niwe mvumilivu katika
matatizo, na mnyenyekevu katika mafanikio.
Ee Bwana, fanya niwe
mwangalifu katika sala, niwe na kiasi katika mali,
|
niwe na bidii katika majukumu, niwe imara katika nia.
Nijitahidi kuwa na usafi
wa ndani, utaratibu wa nje,
maongezi bora, maisha
yanayofuata mipango.
Nikeshe kwa bidii kutawala umbile, kustawisha neema,
kufuata
sheria, kustahili wokovu.
Nijifunze kwako
yalivyo duni mambo ya dunia,
yalivyo makuu
mambo ya Kimungu,
yalivyo
mafupi mambo yapitayo,
yanavyodumu
yale ya milele.
Unijalie nijiandae
kwa kifo, niogope hukumu,
nikimbie
moto, nipate paradiso.
Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.
|
M.H. MARIA MAGDALENA MARTINENGO (1687-1737)
|
Kwa kweli,
Mungu wangu, wewe tu ni mtakatifu!
Utufanye
wote watakatifu, Bwana,
ukiteketeza kwanza ndani mwetu yale yote yanayopinga utakatifu
wako.
|
MT. LEONARDO WA PORTOMAURIZIO (1676-1751)
|
Yesu wangu, kwa haki tu na kwa
shukrani
napaswa kujitoa kabisa kwako, baada ya wewe kujitoa kabisa
kwangu…
Wewe umetakasa
hisi zangu zote; fanya ziwe zako,
zisifurahie tena
kilicho kinyume cha sheria yako ya Kimungu.
Umetakasa kumbukumbu
yangu; iwe inakukumbuka mfululizo.
Umetakasa
utashi wangu; usigeuke kamwe
kupenda chochote kuliko wewe.
Basi, kutoka
dhati ya moyo wangu nakutolea
kama sadaka
kamili ya kudumu, kadiri ninavyoweza,
mwili wangu na roho
yangu, hisi zangu na vipawa vyangu,
nilichonacho na jinsi nilivyo.
Ee
moto wa Kimungu, choma,
Ee Upendo wa
Mwenyezi, choma na kuteketeza
yale yote
yasiyo yako ndani mwangu! Amina.
|
MT. ALFONSO MARIA WA LIGUORI (1696-1787)
|
Yesu wangu, nasadiki kuwa umo katika sakramenti takatifu.
Nakupenda kuliko vyote
na kukutamani rohoni mwangu.
Kwa kuwa sasa siwezi
kukupokea katika sakramenti,
njoo moyoni
mwangu walau kiroho.
Kama umeshafika
nakukumbatia na kujiunga nawe kabisa.
Usiruhusu
nitengane nawe kamwe.
|
MT. YOHANE MARIA VIANNEY(1786-1859)
|
Nakupenda, Bwana,
na neema pekee
ninayokuomba, ni kwamba nikupende milele…
Mungu wangu,
ikiwa ulimi wangu hauwezi kukariri kila nukta kwamba nakupenda,
nataka moyo wangu
ukuambie tena na tena kila ninapopumua.
|
Yesu wangu, jinsi
inavyopendeza kukupenda!
Unijalie niwe kama wanafunzi wako juu ya mlima Tabori,
nikikuona wewe
tu, Mwokozi wangu.
Tuwe kama marafiki
wawili ambao hata mmojawao
hawezi kukubali
kumchukiza mwingine. Amina.
|
MT. KATERINA LABOURE’ (1806-1876)
|
Bwana, nipo hapa, nipe chochote unachotaka.
|
JOHN HENRY NEWMAN (1801-1890)
|
Mungu wangu uliyetuumba,
ulijua kwamba
wewe tu unaweza kutushibisha;
basi umeamua
kujifanya chakula na kinywaji chetu.
Fumbo abudiwa
kuliko yote! Huruma ya ajabu kuliko zote!
Wewe mwenye
utukufu, uzuri, nguvu na utamu kuliko wote
ulijua
fika kwamba chochote kingine
kisingeweza kutegemeza
umbile letu lisilokoma, mioyo yetu dhaifu;
kwa hiyo ulitwaa
mwili na damu ya kibinadamu, hivi kwamba,
vikiwa mwili na
damu ya Mungu, viweze kuwa uhai wetu…
Naja kwako, Bwana,
sio tu kwa sababu pasipo wewe sina raha,
sio tu kwa
sababu najitambua ninakuhitaji,
bali kwa
sababu neema yako inanivuta
nikutafute kwa ajili yako mwenyewe, kwa jinsi ulivyo mtukufu na
mzuri.
Naja kwa uchaji
mkubwa, lakini kwa upendo mkubwa zaidi.
|
MT. TERESA WA MTOTO YESU (1873-1897)
|
Ee Mungu
wangu! Utatu mtakatifu!
Natamani tu
kukupenda na kukufanya upendwe…
Ili maisha yangu yaweze
kuwa tendo moja tu la upendo kamili:
Ninajitoa mhanga
kama kitambiko cha kuteketezwa kabisa na upendo wako rahimu.
Nakusihi
uniteketeze bila ya kukoma,
ukiyaruhusu yale
mawimbi ya upendo wako usiopimika,
yanayojazana ndani
yako, yafurike rohoni mwangu:
hivyo nami niweze kuwa shahidi wa upendo wako, Mungu wangu!
Unijalie kifodini hicho baada ya kunitayarisha kutokea mbele
yako,
|
hatimaye unisababishe
kufa:
na roho yangu iruke moja
kwa moja, bila ya kuchelewa popote pale,
ifikie
kukumbatiana milele na upendo wako rahimu.
Ee mpenzi wangu, mimi napenda,
katika kila pigo la moyo wangu,
kurudia
upya, mara nyingi zisizohesabika,
hili
tendo langu la kujitoa kwako.
Mpaka
hapo vivuli vitakapotoweka,
nami nikaweza kukuambia milele, uso kwa uso, jinsi ninavyokupenda.
|
Ee Yesu, upendo wangu, hatimaye nimegundua wito wangu.
Wito
wangu ni kupenda!
Ndiyo, nimeona
nafasi yangu ndani ya Kanisa,
na nafasi hiyo
umenipatia wewe, Mungu wangu.
Katika moyo wa Kanisa,
mama yangu, nitakuwa upendo:
hivyo nitakuwa yote
na hamu yangu itatimia.
|
Ee Bwana Yesu, mimi si
tai, ila nina macho na moyo wake.
Ingawa ni mdogo, nathubutu kulikazia macho jua la upendo,
na kutamani
kurukia kwake.
|
M.H. ELIZABETI WA UTATU (1880-1906)
|
Ee Mungu wangu, Utatu, ninayekuabudu, unisaidie nijisahau kabisa
ili nikukazie
wewe bila ya kubadilika na kwa utulivu,
kama kwamba roho yangu
ingekuwa tayari katika uzima wa milele.
Kisiwepo
chochote cha kuvuruga amani yangu
wala cha kunitoa nje yako, wewe
usiyebadilika, uliye wangu;
bali kila nukta
nizidi kuzama katika vilindi vya fumbo lako!
Tuliza
roho yangu; uifanye iwe uwingu wako,
makao yako
unayoyapenda zaidi na mahali pa pumziko lako.
Humo nisikuache
kamwe peke yako; bali niwemo mzima,
mwenye
kukesha na kutenda kwa imani yangu,
mwenye kuzama katika kuabudu,
mwenye kujiachilia
kikamilifu kwa utendaji wako Muumba.
Ee Kristo mpendwa
wangu, uliyesulubiwa kwa upendo,
nataka
kuwa bibiarusi wa moyo wako,
nataka kukujaza utukufu,
nataka
kukupenda hadi kufa kwa upendo!
Lakini nahisi unyonge
wangu wote: hivyo nakuomba uwe vazi langu,
ulinganishe matendo
yote ya roho yangu na yale ya roho yako,
unizamishe
ndani mwako, uenee ndani yangu,
ushike nafasi yangu, ili
maisha yangu yake kioo cha maisha yako tu.
Njoo ndani
mwangu ili uabudu, ufidie, uokoe.
Ee Neno
wa milele, Neno wa Mungu wangu,
nataka
kutumia maisha yangu kukusikiliza,
nataka kuwa
msikivu kabisa kwa mafundisho yako,
|
nijifunze yote kwako,
halafu katika usiku wa
roho, katika utupu, katika unyonge
nataka
kukukazia macho daima
na kubaki
chini ya uangavu wako mkuu.
Ee nyota
yangu ninayoiabudu,
unichanganye hata
nisiweze tena kukwepa mng’ao wako.
Ee moto unaoteketeza, Roho wa upendo, ushuke ndani yangu
ili katika roho yangu
itokee aina ya umwilisho wa Neno!
Niwe kwake
mwendelezo wa ubinadamu wake
ambapo aweze
kutekeleza upya fumbo lake.
Nawe Baba uniinamie
mimi kiumbe chako maskini,
unifunike kwa kivuli
chako, usione ndani yangu kitu kingine
isipokuwa mpenzi
wako uliyependezwa naye sana.
Enyi watatu
wangu, yote yangu, heri yangu,
upweke usio na mipaka,
upana ambao napotea ndani yake,
najiachilia kwenu kama mateka.
Mzame ndani mwangu
ili nami nizame ndani mwenu,
wakati ninapongojea kuja
kutazama katika mwanga wenu
kilindi cha ukuu wenu.
|
M.H. CHARLES DE FOUCALD (1858-1916)
|
Baba yangu, najiaminisha
kwako; unifanyie unavyopenda wewe;
kwa chochote
utakachonitendea, nakushukuru tu.
Niko tayari
kwa lolote; nakubali yoyote,
mradi matakwa
yako yatimizwe ndani yangu
na
katika viumbe vyako vyote.
Sitamani
kitu kingine, Mungu wangu.
Naweka roho yangu mikononi mwako; naitoa kwako, Mungu wangu,
kwa upendo wote wa
moyo wangu, kwa kuwa nakupenda.
Basi, kwangu ni
sharti la upendo kujitolea,
kujitia mikononi mwako, pasipo kipimo,
ila kwa
tumaini lisilo na mipaka,
kwa sababu
wewe ndiwe Baba yangu.
|
MT. MASIMILIANO MARIA KOLBE (1894-1941)
|
Wewe umenipenda
milele, tangu u Mungu;
hivyo umenipenda na
utanipenda milele!...
Upendo wako kwangu
ulikuwepo hata kabla sijakuwepo,
na ni kwa sababu ya kunipenda, Mungu mwema, kwamba
umeniita kutoka utovu
wa vyote nianze kuwepo!
|
M.H. TERESA WA KOLKATA (1910-1997)
|
Baba yetu, mwanao nipo hapa, tayari kwako
|
unitumie ili kuendelea
kupenda ulimwengu kwa kuupatia Yesu
na, kwa njia yangu, kumtoa kwa kila mmoja na kwa ulimwengu.
|
Ee Bwana, utufanye
tustahili kutumikia watu wenzetu
ambao ulimwenguni kote wanaishi na kufa kwa ufukara na njaa.
Kwa mikono yetu uwape
leo mkate wao wa kila siku;
na kwa upendo wetu wenye
kuelewa uwape amani na furaha.
|
Ee Bwana wangu,
nakupenda,
Mungu wangu,
najuta,
Mungu wangu,
nakuamini,
Mungu wangu,
nakutumainia.
Utusaidie kupendana unavyotupenda.
|
Bwana Yesu, wewe
ambaye uliumba kwa upendo,
ulizaliwa kwa upendo, ulitumikia kwa upendo, ulitenda kwa
upendo,
uliheshimiwa kwa
upendo, uliteseka kwa upendo,
ulikufa kwa
upendo, ulifufuka kwa upendo,
nakushukuru kwa upendo
wako kwangu na kwa ulimwengu wote,
na kila siku
nakuomba: unifundishe mimi pia kupenda!
Amina.
|
YOHANE PAULO II (1920-2005)
|
Ee Kristo,
kichwa na mwokozi pekee,
uvute kwako
viungo vyako vyote.
Uwaunganishe na
kuwageuza katika upendo wako,
ili Kanisa ling’ae kwa
ule uzuri upitao maumbile
unaodhihirishwa katika watakatifu wa kila wakati na taifa,
katika wafiadini,
waungamadini, mabikira
na mashahidi
wasiohesabika wa Injili!
Ee Yesu
mtamu, Yesu mwema,
Yesu,
mwana wa Maria!
Amina!
ITAENDELEA...............
|
|
Comments