PIMA UKARIBU WAKO NA BWANA

Na Frank Philip


“Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano? Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa” (Mathayo 13:10-13).

Haya ni mazungumzo baina ya Bwana na wanafunzi wake, wakiwa peke yao (faragha) baada ya mahubiri ambapo Bwana alifundisha kwa mfano wa Mpanzi.

Kuna tofauti kubwa kati ya mtu asomaye Neno au kusikiliza mahubiri tu, na mtu aombaye na kujifunza Neno au kusikiliza mahubiri. Neno bila maombi ni kitu chema ila hufiki mbali; Neno na Maombi ni jambo jema na utafika mbali sana katika imani yako. Ukisoma na kuomba, utaona unavyokua katika hilo Neno na matunda yake ni dhahiri.

Bwana alisema ataleta “Msaidizi mwingine”, ambaye ATATUFUNDISHA na KUTUKUMBUSHA. Yesu alijua sio rahisi kujifunza bila msaada, tunamhitaji Roho Mtakatifu 100% ili kuelewa Neno na hilo Neno litusaide katika maisha yetu kama mtu binafsi. Hebu fikiri Bwana anahubiri maelfu-elfu ya watu, halafu baadae wanafunzi wake 12 wanamfuata na kumwambia, “Mwalimu, hatukuelewa kitu pale”, Bwana anaanza tena kuwaambia tafsiri na maana ya lile Neno alilofundisha, kwa KUTUMIA MANENO MENGINE ya ziada.

Sasa kumbuka, ILE mikutano mikubwa ambayo Bwana Yesu alihubiri, watu walipata somo, ila PART 1 tu. Baadae wanafunzi waliokaa tena FARAGHA na Bwana, na kuuliza tena walipata PART 2 ya somo lile lile. Nisikilize, ukitaka kupata part 1 na part 2 ya Neno, jifunze kwenda FARAGHANI na Bwana. Ukiishia kusoma Maandiko kwa sababu umeambiwa na mchungaji wako usome biblia, utaishia na part 1 tu, ila wapo wengine ambao watachukua hatua ya ziada, watajifungia huko ndani na Bwana, wanasoma na Kuomba, huko faraghani, hao watapata Part 1&2 ya Neno.

Hebu fikiri, wakati ule Bwana akiwa duniani, watu 12 tu ndio walipata part 1&2 ya Neno alilosema Bwana kwa sababu walichukua muda wa ziada wa kukaa na Bwana na KUOMBA awafundishe zaidi maana ya walichosikia. Mara nyingine, Bwana alikaa na wanafunzi 3 tu kati ya hao 12! Je! Umetafuta kuwa KARIBU na Bwana kama mkutano wote ulivyokuwa, au wale wanafunzi 12 au wale wanafunzi 3? Je! kwenye makanisa yetu ya nyakati hizi, ni wangapi wanapata part 1&2 ya Neno?

Frank Philip.

Comments