TOKENI MKATENGWE NAO.





BWANA YESU asifiwe ndugu yangu.

Siku za karibuni nikiwa kazini kuna mkubwa wangu mmoja wa kazi ambaye ni mgeni kwangu alinishangaza sana maana aliniita na kuniambia ‘’Peter Kaninunulie sigara 2’’ 

Moyo wangu ulilipuka na kukaja hasira ya rohoni kubwa sana, Nikamjibu kwa nguvu kwamba haiwezekani na MUNGU hapendi ujinga huo, Yule mzee  uoga wa ghafla ukampata, akaanza kuongea kama ana kigugumizi, akawa mpole sana na hakutoa amri tena bali akaniuliza ‘’Samahani je umeokoka?’ Nikasema ‘’Ndio nimeokoka kwa neema ya BWANA YESU’’ Akasema ‘’Samahani sana mtumishi,  akaondoka na kuelekea kwingine ndipo nikakumbuka Neno la MUNGU katika 2 Kor 6:17-18 Linasema ‘’Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, ‘’.

Kumbe kuna haja ya kutoka kati yao.

Hatutoki yaani hatuhami nyumba zetu ambazo tunakaa na wasioamini au walikamatwa na dhambi mbaya ila  tunatoka kwa jinsi ya kutokushirikiana nao katika uovu wao.

Wewe mama ambaye mmeo ni mlevi na wewe umeokoka hakikisha unatengwa naye kwa jinsi ya matendo yake yaani usishiriki uovu wake, Isitokee kwa sababu unaenda sokoni harafu akakuambia ‘’Hiyo chenji itakayobaki niletee bia 2 za kopo’’ Mkatalie maana hapo utakuwa umeshiriki uovu wake. NI BORA KUMTII MUNGU NA SIO KUWATII WANADAMU AMBAO HAWANA MBINGU YA KUKUPELEKA. Na kama una ndoa ya aina hii maombi kwako itakuwa ni silaha namba moja na kuhakikisha mpaka kati yako na mmeo mlevi  ni mkubwa sana kiasi kwamba hawezi kukushirikisha uovu wake.

Hiyo ni mifano miwili tu katika makumi elfu ya mambo kama hayo yanayowapata watu wengi  lakini Biblia inatuambia tokeni mkatengwe nao kwa habari ya matendo yao maovu.

Ni marufuku kuchangia uovu wa mtu mwovu.

Vijana wengi wa kiume huwatongozea marafiki zao mabinti wakidhani wako salama na dhambi, kumbe hata wao wanachukua ujira wa wazinzi.

Unabuniwa uongo  mahali Fulani na wewe unashirikishwa ili tu umwambie uongo mtu mwingine ukidhani kwamba dhambi yako ni ndogo kumbe umebeba kapu zima la dhambi hiyo.

Wengi wanawaficha wezi wakidhani kwamba wao wako salama kumbe hata wao wametabeba dhambi ya wezi vilele na kwa kiwango kile kile cha mwizi halisi.

Tunatakiwa tume makini sana, tunatakiwa tukatengwe nao waovu kwa habari ya kuzishiriki dhambi zao.

Nikiwa Zanzibar miaka michache iliyopita, yaani miezi kadhaa baada ya kuokoka, marafiki zangu wengi kama sio wote kabisa walikuwa na tabia ya kuongea matusi, lakini namshukuru MUNGU kwa msimamo wangu wa kiroho ulipelekea kila nikifika tu wanaacha mada ya matusi na kuanza kuongea yasiyo matusi,  unashangaa ukitokea tu kazini unasikia ‘’mtu wa MUNGU amefika hivyo tuache matusi’’, mwanzoni niliona kama wananikebehi lakini nilikuja kugundua kwamba walikuwa wananisaidia sana ili siku zote niwe mbali na baraza la wenye mizaha. Na pia msimamo wangu ulisaidia kuwafanya wasiongee uovu mbele yangu. Kumbe kuwa na msimamo ni jambo jema sana.

Hata wewe ndugu yangu tambua kwamba msimamo wako kiroho utasababisha  mtu yeyote asikushirikishe uovu wake. Dhihirisha imani yako hadharani, na kila mtu ajue kwamba umeokoka, linda imani yako ya uzima, wala sio kila siku ukienda kanisani unaficha Biblia hadi ukifika kanisani ndio unaitoa hiyo ni imani haba zaidi. Onyesha msimamo wako na onyesha kwamba YESU uliyempokea hafananishwi na chochote na hakuna wa kumwondoa ndani yako.

Waefeso 5:7-12 (Basi msishirikiane nao.  Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika BWANA; enendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo BWANA. Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee; kwa kuwa yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu hata kuyanena. )

-Msishirikiane nao katika uovu.

-Mlikuwa hivyo zamani lakini sasa hivi  mko na YESU.

-Enendeni kama watoto wa MUNGU wanaokataa kila dhambi iwe ya kutenda au kushawishiwa kutenda.

-Kwa kila jambo mkihakiki kama mnampendeza MUNGU.

-Msifanye matendo yasiyofaa yaani matendo ya giza bali myakemee siku zote.

Tusiichezee neema kuu namna hii maana ‘’Wema wake Mwokozi wetu MUNGU na upendo wake kwa wanadamu ulipofunuliwa, ALITUOKOA-Tito 3:4.

Hakuna siri kwa MUNGU.

Mathayo 12:36(Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. ).

Usikubali kushiriki uovu wa waovu, Biblia katika Ufunuo 18:1,4  inatuonya kwamba ‘’Baada ya hayo naliona malaika mwingine, akishuka kutoka mbinguni, mwenye mamlaka kuu; na nchi ikaangazwa kwa utukufu wake.  Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza; kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake. Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, TOKENI KWAKE, ENYI WATU WANGU, MSISHIRIKI DHAMBI YAKE, WALA MSIPOKEE MAPIGO YAKE . ‘’

Wafanye uzinzi wengine harafu uende moyoni na wewe kwa sababu tu ulitoa chumba chako ili wafanyie uovu wao, kataa leo kama neno linavyokuonya katika Isaya 52:11 ‘’ Nendeni zenu, nendeni zenu, tokeni huko, msiguse kitu kichafu; tokeni kati yake; iweni safi ninyi mnaochukua vyombo vya BWANA. ‘’.

Toka kati wa waovu wanaokushawishi uovu, Yeremia 51:45 ‘’Enyi watu wangu; tokeni katikati yake, mkajiokoe nafsi zenu na hasira kali ya BWANA, kila mmoja wenu. ‘’

MUNGU hadhihakikiwi milele Hivyo ‘’APANDACHO MTU NDICHO ATAKACHOVUA- Wagalatia 6:7.’’

Usipande uovu kwa watu bali panda mema, panda uzima kwa watoto wako, panda uzima kwa mke wako, panda uzima kwa mme wako, usimtendeshe dhambi maana dhambi ni mbaya , dhambi inaua na dhambi inapeleka watu kwenye mateso ya milele.

BWANA MUNGU anasema hivi katika Kutoka 32:33 ‘’ Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. ‘’

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292
                 MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
 MUNGU Akubariki.

Comments