UKARIBU NA MUNGU v/s MAFANIKIO

Na Frank Philip


“BWANA peke yake alimwongoza, Wala hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye. Alimpandisha mahali pa nchi palipoinuka, Naye akala mazao ya mashamba; Akamnyonyesha asali iliyotoka jabalini, Na mafuta yaliyotoka katika mwamba wa gumegume; Siagi ya ng’ombe, na maziwa ya kondoo, Pamoja na mafuta ya wana-kondoo, Kondoo waume wa Kibashani, na mbuzi, Na unono wa ngano iliyo nzuri; Ukanywa divai, damu ya mizabibu. Lakini Yeshuruni alinenepa, akapiga teke; Umenenepa, umekuwa mnene, umewanda; Ndipo akamwacha Mungu aliyemfanya, Akamdharau Mwamba wa wokovu wake” (Kumbukumbu la Totari 32:12-15).

Zamani nilisikia kwamba “watu waliookoka” ni watu wenye matatizo fulani katika maisha yao. Mwingine akasema, “ukiona mtu ameokoka, jua kuna kitu anatafuta huko na sio kwamba anampenda Mungu”, na mwingine tena akasema, “hawa walokole wakipata pesa, wakifanikiwa, huanza kurudi nyuma na kumwacha Mungu”.

Nikatazama jambo hili na kugundua sio jambo geni. Alikuwepo Yeshuruni, alipofanikiwa baada ya Mungu kumpitisha mengi, akamdharau Mungu kwa kugeukia kufanya machukizo mbele za Bwana. Yeshuruni alipokuwa nyikani, mahali pa gumu, alimlilia Mungu, sasa Mwamba wa wokovu wake amemwokoa, amembariki, natazama! Yeshuruni amepiga teke, eti kwa sababu amenenepa kwa mafanikio, sasa amegeukia njia za udhalimu, uzinzi na uasherati. Mafanikio!

Je! unaona uhusiano gani kati ya MAFANIKIO yako na UKARIBU wako na Mungu? Je! Mafanikio yamekuvuruga ukawa mbali na Mungu? Kumbuka, sio kila aliyeko mbali na Mungu, au aliyegeukia sanamu atasema “sasa nimemwacha Mungu”, ila utaona akisema “niko busy, sina muda kabisa wa maombi wala Neno”, lakini utamkuta anasoma magazeti, kucheza games kwenye simu yake ya kiganjani, kuangalia senema, ku-chart na watu mtandaoni, nk. Ewe Eshuruni, umesahau fadhili za Bwana Mungu wako, hata sasa unamkasirisha na kumtia wivu na vinyago vyako?

Sawa, hukujua habari za Mungu hadi ulipofikwa na shida fulani, ndipo ukakimbilia kupata msaada. Sasa angalia hekima yako isipungue, ikawa ndogo kuliko ya yule kahaba kule Yeriko, jina lake Rahabu. Rahabu aliposikia matendo makuu ya Mungu, alipata hekima na kujua ukuu wa Mungu asiyemjua zamani; akafanya maamuzi ya kujisalimisha yeye na nyumba yake yote; wote WAKAOKOKA, wakapata msaada, hawakuangamia. Angalia tena, Rahabu hakubaki hapo, alienda na watu wa Mungu hata leo. Kupitia tumbo la Rahabu, walizaliwa wafalme wakuu wa Israel, ikiwemo na Bwana pia. Rahabu alikuwa kahaba, ila alipata moyo wa hekima na kumjua Mungu aliye hai na kumkimbilia.

Frank Philip.

Comments