UNYENYEKEVU WA MOYO.




BWANA YESU asifiwe ndugu.


Neno la MUNGU ni chakula cha uzima, Tamani sana kula chakula hiki maana ndani ya chakula hiki umo uzima.


Leo  ninazungumzia kitu cha muhimu sana yaani UNYENYEKEVU WA MOYO.


Mathayo 11:29 BWANA YESU anasema (Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; )

Tuna mengi sana ya kujifunza kwa BWANA YESU  na hili la unyenyekevu wa moyo ni moja kati ya mambo ya kujifunza kwake.

Kama ukiushika unyenyekevu wa moyo kinachofuata ni Raha.

Kuna raha ya dunia hii na kuna raha ya milele ambayo tutaipata mbinguni. Waebrania 4:1,3,11 ( Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile; kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu: Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi. )

Tufanye bidii ili tuweze kuingia rahani mwake BWANA YESU .

MUNGU aliahidi tangu zamani kwamba waasi na wasio wanyenyekevu wa moyo, hawataweza kuingia rahani mwake.

Biblia inaendelea kusema maneno haya Ufunuo 14:11 ( Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na kila aipokeaye chapa ya jina lake. )


           JINSI YA KUIPATA RAHA YA MILELE.


Bila upole na unyenyekevu hatuwezi kuipata raha hii ya milele. Mathayo 5:5 (Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. ).


BWANA YESU asifiwe.

Unajua kwanini nasisitiza sana unyenyekevu wa moyo?

Ni kwa sababu kinyume cha  upole na unyenyekevu ni ujeuri na kiburi Zaburi 147:6 (BWANA huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri. ) na pia andiko hili ni la muhimu sana katika hili 1 Petro 5:5 ( Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu MUNGU huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. ).


Kinyume cha unyenyekevu ni kiburi  na MUNGU huwashusha wenye kiburi.


Ndugu yangu nyenyekea kwa MUNGU ili akuinue.


Kiburi ni kibaya sana .


Kiburi kilimwangusha shetani kutoka kwenye uzima wa milele mbinguni na kwenda kwenye jehanamu ya milele.


Unyenyekevu ni syllabus nzuri ya maisha.


Shetani ni chanzo cha kiburi na jeuri na vitu hivi viwili yaani kiburi na jeuri humpata mtu baada tu ya kuondoka unyenyekevu na upole wa moyo.


Isaya 14:12-15 inazungumzia kilichomwangusha shetani inasema ( Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za MUNGU; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu. Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo. ).

Kiburi na jeuri ni vitu vibaya sana, vinashusha watu wengi shimoni yaani kuzimu kama vile shetani na malaika zake walivyoshushwa.

Wengi kwa kujawa na kiburi na jeuri hawahitaji kujifunza neno la MUNGU, kwa sababu ya kiburi na jeuri hawamhitaji BWANA YESU mwenye uzima wao wa milele.
Biblia inaendelea kuzungumza kuhusu shetani 
Ezekieli 28:13-17 (Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya MUNGU; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa MUNGU, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa MUNGU, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama. )


Ndugu yangu ukiona umeishiwa unyenyekevu wa moyo na upole kwa MUNGU basi tambua kabisa ndani yako kumeingia kiburi na jeuri ambavyo ni mapando ya shetani na tambua kabisa mapando hayo shetani ameyapanda ndani yako ili tu kukushusha shimoni yaani kuzimu.


Ukiwa na kiburi hutahitaji kuchukua muda wako kujifunza neno la uzima.

Kiburi na jeuri vinawafanya wengi kudharau ibada kanisani.

Ufunuo 12:7-9 ( Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake;  nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. )

Kiburi kilimshusha shetani na malaika zake.

MUNGU huwashusha wenye kiburi.

Nyenyekea kwa MUNGU wako ili MUNGU akuinue.

Hata kama wewe umeokoka ukiona unapungukiwa na unyenyekevu wa moyo basi kiburi kimekuvaa. Kataa kiburi kwa maombi na utafunguliwa.

Biblia katika Yakobo 4:7 Inasema tumtii MUNGU na tumpinge shetani naye atatukimbia.

Mwenye utii hawezi kuwa na kiburi.

Mwenye utii hawezi kuwa na jeuri.

Ndugu mtii MUNGU siku zote za maisha yako  na nyenyekea chini ya mkono wake wenye nguvu naye atakuinua tu.
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292
                 MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
 MUNGU Akubariki.


Comments