Wajibu wa Wazazi kwa watoto wao.

Mzazi ni wajibu wako kuwapenda watoto wako wote, kuwafundisha njia ipasayo, kuwatia moyo wanapopitia magumu, na kuhakikisha unakuwa mstari wa mbele kuwajengea self esteem imara. 

Mzazi hupaswi kuwa critic wa mtoto wako, hiyo sio kazi yako. Muongoze katika kweli, mfundishe, muadhibu pale anapokosea na chunga sana usimuadhibu ili kumuaibisha bali kumsaidia. Adhabu ya kumsaidia mtoto unampa kwa kujali utu wake na sio mbele ya kadamnasi na kumuaibisha.

Watoto hawalingani, usifanye kosa la kuwalinganisha watoto, iwe ni watoto wako wote au kumlinganisha wako na wa jirani. Tambua kila mwanadamu ameumbwa tofauti, jitahidi kumfahamu mwanao na kumsaidia kuwa bora kwa jinsi Mungu alivyomuumba ukiangalia zaidi strengths zake kuliko mapungufu. Kosa ambalo wazazi wengi wanafanya ni kuwabagua watoto kulingana na uwezo wao kwa yale ambayo yanaonekana mema katika jamii mfano kumpenda zaidi mtoto anayejituma kuwahi kuamka na kumbeza yule anayependa kulala tena mbele za wengine.
 Ndio, kila mtoto lazima afuate utaratibu lakini usitumie kigezo hiki kupimia upendo, badala ya kumsaidia utakuwa unampoteza kabisa.
Mtoto anayeona anabaguliwa nyumbani atajenga kiburi na ataanza kuwachukia wenzie wanaopendwa zaidi na itampelekea kutafuta upendo nje kwa watu wasiofaa na kujikuta katika matatizo makubwa. Chunga sana maneno unayomwambia mtoto wako, maneno yanaumiza kwa muda mrefu, yanaua kujiamini na yanaumba. 

Mtamkie maneno ya baraka, tumaini na hata pale unapomuonya maneno yako yasiwe ya kumdhalilisha mfano hujui kitu kabisa, sijui wewe ni mtoto wa aina gani, hufai kabisa n.k. Maneno ya aina hiyo hayafai kabisa maana hayajengi bali yanamuondolea kujiamini na kumfanya ajione hana thamani. 

MUNGU akubariki.
By Women of Christ.

Comments