 |
Na Mch. Maximillian Machumu |
Waamuzi
15:9-16: Samson alikuwa mnadhiri wa Mungu na aliwekwa kuwaangamiza
wafilisti, kwasababu ya kuwaangamiza Wafilisti ndugu zake wakaamua
kumfunga na kumkabidhi kwa wafilisti ili wasije kulipa kisasi kwa wao.
Katika kumfunga Samsoni, ndugu zake wapatao elfu tatu walitumia kamba
mbili; kuna mambo mengi ya kujifunza kupitia habari hii
KWANINI
NDUGU WALIMFUNGA: kama tulivyosoma katika kitabu cha Waamuzi 15:9-16,
ndugu zake ndio waliohusika kumfunga Samsoni. Hapa tunajifunza kuwa mara
nyingi adui (shetani) anapotaka kumfunga mtu hupitia kwa watu wake au
wanaomjua mtu huyo vizuri. Kifungo kinachotokana na watu wako wa karibu
ni kibaya zaidi kwasababu wanaujua udhaifu wako; muda gani unaomba na
muda gani huombi.
Ndio maana hata Mtume Paulo aliwahi
kutegeshewa nyoka kwenye kuni (Matendo ya Mitume 28:3). Nyoka ni yule
mtu wa karibu anayejua siri na mambo unayoyafanya, kwasababu hiyo
inakuwa rahisi kwa shetani kuwatumia kukuangamiza. Nyoka hakuonekana
mwanzoni kwa Paulo kwasababu alijifanya kama kuni, na watu wa karibu ni
vivyohivyo huwezi kuwatambua kwa urahisi. Furaha ni kuwa Mungu
hakuruhusu yule nyoka kumwangamiza Mtume Paulo.
KWANINI
WALITUMIA KAMBA MBILI: Ndugu wa Samsoni walikuwa elfu tatu lakini jambo
la ajabu ni kuwa walibeba kamba mbili tu; Utajiuliza nini siri ya hizi
kamba mbili?. Yesu mwenyewe aliainisha kamba mbili kuu ambazo shetani
anazitumia kuwaangamiza na kuwafunga watu duniani. Ukisoma katika Ufunuo
1:18 “na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata
milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.” Kumbe zile
kamba mbili zina maana ya mauti na kuzimu. Kuzimu inaleta magonjwa na
matatizo mbalimbali lakini mauti inaleta kifo. Kamba mbili mpya ni mauti
na kuzimu. Kwa kuzimu na mauti shetani amekuwa akiwaangamiza na
kuwatesa watu wa Mungu. Inawezekana na wewe ni mmoja wa watu wanaoteseka
kwasababu ya kamba hizi leo kuna habari njema kuwa Yesu aweza kukata
kamba hizo.
MATOKEO YA KIFUNGO CHA SAMSONI: baada ya
kumfunga, ndugu zake wakamkabidhisha kwa wafilisti yaani adui zake.
Jambo la ajabu likatokea, mara baada ya kukabidhiwa. Imeandikwa,
“Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho
ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake
zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake
vikaanguka mikononi mwake.” Waamuzi 15:14 kupitia kifungo kile Mungu
akamtumia Samsoni kuwaangamiza wafilisti wote. Kumbe waweza upo katika
kifungo ambacho Mungu alikiruhusu ili upate ushindi ulio mkamilifu.
MUNGU
ANAWEZA KUKATA KAMBA ZILIZO KATIKA MAISHA YAKO: Wachawi na waganga
wanaweza kuwa wajanja mbele ya macho yetu lakini Bwana anawaona, na
kamba zao zinaonekana mbele ya macho ya BWANA. Hata mfalme Daudi aliwahi
kuwa katika kamba hizo ukisoma katika Zaburi 119:61 “Kamba za wasio
haki zimenifunga, Sikuisahau sheria yako.” Upo uwezekano wa mtu
kufungwa, Mwilini unajiona ni mtu asiye na mafanikio au asiye na
mwelekeo lakini rohoni unakuwa umefungwa na kamba kabisa. Zaburi
18:1->… “…Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia
hofu. Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili. Katika
shida yangu nalimwita Bwana, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia
sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake…”
Mungu anaweza kukutoa katika kamba za matatizo unayopitia. Daudi
alipokuwa katika kamba hizo aliliitia jina la BWANA.
Yesu
alipofufuka akatangaza kuwa anazo funguo za mauti na kuzimu, Hata kama
aliyekufunga awe mtu wa karibu kiasi gani lakini zipo funguo za kufungua
kamba zilizokufunga. Kama alivyofanya kwa Samsoni; baada ya kukufungua
kinachofuata ni kipigo kwa wale wote walioshiriki kukufunga. Mungu
anaweza kukutofautisha; shida na mateso yote unayopitia si kitu mbele za
Mungu wetu kwasababu yeye anaweza kukuweka huru. Mpokee Yesu upate
uhuru mkamilifu, kwasababu dunia ya leo haipo salama kama haupo ndani ya
Yesu.
Comments