ZAKA YA FUNGU la KUMI - II

Na Frank Philip


“Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la” (Malaki 3:8-10).

“Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba; ili kwamba BWANA, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo” (Kumbukumbu 14:28,29).

Kwenye somo lililotangulia tumeona kwa ufupi kusudi/lengo la kutoa sadaka za zaka (fungu la kumi), na pia tumeona watu wanaostahili KULA hiyo ZAKA.

Kuna maswali mengi ya kujiuliza, kwa mfano, kwanini Mungu ameagiza sisi tutoe zaka au sadaka? Kumbuka, mfumo wa sadaka ulianza kwenye familia ya kwanza ya Adam na Hawa. Tunajifunza jinsi Kaini na Abeli walivyotoa sadaka zao mbele za Bwana, na matokeo ya utoaji wao. Sasa nataka uone kwamba wakati huo hapakuwa na WALAWI, HEKALU, KUHANI wala HUDUMA, ila Mungu alikuwepo kupokea SADAKA za wanadamu na kuwabariki BILA kuwepo na “mtu wa kati” wa kuwawekea mikono watu wengine (makuhani/viongozi wa kidini). Ukitaka kuona hili jambo, angalia sadaka za Ibrahim, Isaka na Yakobo; ilikuwa ni mtu na Mungu wake (soma kitabu cha Mwanzo). Kwa upana zaidi, angalia sadaka za Korinelio kwenye Agano jipya (Matendo ya Mitume mlango wa 10), hapakuwa na “mtu wa kati”; Korinelio aliwapa watu “vitu vingi”, Mungu akapokea.

Nisikilize kwa makini. Sisemi kuwekewa mikono au kuombewa baraka ni vibaya, ila HAKUNA namna mtu atatoa sadaka zake kwa MOYO MBOVU kama wa Kaini, halafu akawekewa mikono, ikamsaidia kupokea baraka, hakuna! Kwa upande wa pili, hakuna mtu atatoa sadaka zake “kwa SIRI”, bila kuwekewa mikono na mtumishi yeyote, ila ametoa sadaka zake kwa MOYO MZURI kama wa Abeli, asipokee baraka zake kwa kipimo cha kujaa, kusukwa-sukwa, na kufurika. Thamani ya sadaka yako ni MOYO wa sukrani, uelekevu na ibada mbele za Mungu wako. Usisahau hata siku moja, baraka za Mungu hazinunuliwi kwa sadaka, ila kwa “moyo wa uelekevu” mbele za Mungu wako.

Sasa, nataka uone kwa undani kidogo habari ya sadaka/zaka, ili usijivune sana utoapo. Kwanza, imekupasa kujua kwamba Mungu hana shida na hiyo pesa yako, ila HALI ya moyo wako utoapo hizo sadaka zako. Angalia hapa, “Nimkaribie BWANA na kitu gani, na kuinama mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimkaribie na sadaka za kuteketezwa, na ndama za umri wa mwaka mmoja? Je! BWANA atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzao wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu? Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!” (Mika 6:6-8).

Mungu anasema lengo sio kukusanya sadaka zako, hakuna kitu cha thamani mtu anaweza kuleta mbele za Bwana, kikawa kikubwa kama MALIPO ya WEMA wake, au FIDIA ya dhambi zetu mbele zake. Angalia tena hapa, “BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako”. Bwana Yesu akiona shida iliyoko kati ya taratibu za KIDINI, akasema maneno haya, ambayo nabii Mika alisema pia, “Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia” (Mathayo 12:6,7). Yesu anasema, kuna mmoja aliye mkuu zaidi kuliko hekalu lako, naye ni Mungu; na anachotaka kwako sio SADAKA ila REHEMA. Sasa usisahau kwamba Rehema ni “hali ya moyo inayompelekea mtu kutenda/kuenenda kwa namna fulani”; sasa ukiwa na MOYO wa REHEMA, kisha ukatoa sadaka zako, umefanya jambo jema sana. Ukisukumwa kutoa ILI ubarikiwe, jua umepoteza lengo la MSINGI la utoaji wako, japo tukitoa tunabarikiwa; chunguza moyo wako na uhusiano wako na Mungu.

Sababu za Kutoa Sadaka/Zaka Zako

Pamoja na sababu BINAFSI za utoaji, ambazo msingi wake uko katika KUMCHA Mungu na KUMWABUDU, kuna mambo ya msingi ya kuangalia hapa. Kwanza, imekupasa kujua kwamba mfumo wa sadaka uliwekwa ili kuwepo na CHAKULA katika nyumba ya Mungu, au katikati ya watu wa Mungu. Angalia hapa, “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu”. Hili neno “ghalani” limekuwa na tafsiri kwamba (ghala ni kanisani ambapo mtu anaabudu). Lakini nakwambia leo, hili neno “ghalani” ni zaidi ya kanisani kwako (Kumb. 14:28,29). Sasa tafsiri ya Chakula ni Chakula, yaani hiki chakula cha kujenga mwili na sio cha roho (Neno). Hata kama itakuwa sadaka ya pesa, lengo ni kiwemo “chakula” na sio tafsiri ya “Neno” au “mahubiri”.

Watu wengi wamejaribu kubadili hili neno “chakula”, na kusema ni “mahubiri”, sawa, Neno la Mungu ni chakula, ila hapa kwenye Malaki, hasemi habari ya mahubiri (Neno), anasema habari ya chakula cha mwilini kabisa (ugali, mchele, nyama, nk.) Lengo la Mungu kusema watu “walete chakula (zaka)” ni hili hapa, “Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba”. Hapo hakuna kitu kama mahubiri, ni chakula kabisa cha damu na nyama. Je! Masikini, wajane, na yatima wako wapi wakila na kushiba katikati yetu?

Angalia tena, Mungu aliweka mfumo wa kutoa sadaka kwa ajili ya watu wasio na KIPATO au URITHI katika jamii husika. Ndipo tunaona WALAWI (watumishi wa Mungu) wanatajwa hapa, wakichanganywa na MGENI, YATIMA, WAJANE, nk., yaani watu wenye UHITAJI katika jamii (Kumbukumbu 14:28,29). Hawa wote hawakuwa na chakula cha kutosha, kwa sababu hawakuwa na urithi (Mlawi na mgeni) AU mtu waliyemtegemea amekufa (yatima na mjane), na kupitia ZAKA, wanapaswa wale na kushiba. Sasa ukiangalia “ghala” kwenye kitabu cha Kumbukumbu la Torati, utaona unaagizwa “uliweke ndani ya malango yako”. Sasa sisemi kupeleka kanisani kwako ni makosa, ila SIO lazima ufanye hivyo, KAMA Mungu hajakuaagiza kupeleka huko. Kumbuka siku zote, kutoa ni LAZIMA utoe (Kumbukumbu 14:22,23), ILA “utatoa sadaka/zaka zako mahali Mungu alipokuagiza, na sio popote UPAONAPO”.

Ukitaka kuona shida katika mafundisho ya utoaji, jiulize maswali yafuatayo, Je! Mtumishi fulani akipewa ZAKA au SADAKA na kondoo asiye wa kundi lake, anakataa na kumwagiza huyo kondoo apeleke kwa mchungaji wake? Kama anapokea kutoka kwa kondoo wasio wa kundi lake, kwanini anazuia kondoo wake wasiongozwe na Mungu wao kutoa sadaka zao mahali pengine? Jiulize tena swali, Je! Mungu akisema “kuanzia sasa, wanadamu wote wasitoe tena sadaka za fedha na vitu”, Je! Hao watumishi wataendelea na huduma kwa moyo ule ule? Jibu mwenyewe maswali haya kwa nafsi yako, wala usimtazame mwingine.

Umewahi kufikiri watumishi wanasema “leteni zaka yote na sadaka zenu kwa sababu mnakula kiroho hapa kanisani”, na ghafla! Mungu anabadilisha utaratibu na kusema, “wapeni watumishi wangu vitu vya rohoni tu, yaani faraja na maombi, ila msiwape pesa na vitu”. Fikiria mwenyewe ni huduma ngapi zingesimama. Halafu ujiulize kwanini zimesimama? Je! Hawana chakula au hawana faida? Ndipo utagundua tofauti kati ya mchungaji wa halisi na mchungaji wa mshahara, na ndipo utajua lile neno lisemalo, “sisi ni watumishi tusio na faida”. Hebu piga picha uone jinsi wajane, yatima na masikini WANAJIKAMUA kupeleka zaka zao kanisani kwa sababu “wametishiwa maisha” kwamba watalaaniwa wasipofanya hivyo. Kweli imewapasa watu WOTE kutoa zaka na sadaka zao, ila kwa KUMCHA Bwana, na kwa MOYO wa KUPENDA kutoa, sio kwa HOFU na VITISHO. Kama mtumishi angechagua vyema, angewalazimisha watu kwa ukali ZAIDI wasitende dhambi, kuliko kuwalazimisha watu kutoa zaka na sadaka zao wakiwa dhambini; mtumishi wa namna hii angekuwa upande wa Bwana na sio wake mwenyewe.

Kwa habari ya WALAWI nitasema tena. Sio kila mtumishi wa Mungu ni Mlawi. Sifa ya muhimu ya Walawi ilikuwa ni watu wa kutumika HEKALUNI, wao na watoto wao. Hawakuwa na mtu wa kumtegemea kwa ajili ya kujipatia kipato. Walawi hawakuwa na urithi, wala chakula ila kile kilichotolewa sadaka. Hawakuwa na shamba, wala mradi wa kujiingizia kipato, Bwana ndio fungu lao. Je! Watu watajiita Walawi katika jamii zetu za sasa? Je! Walawi hawakuwa kabila mojawapo la wana wa Israel kati ya makabila 12, waliokuwa makuhani mbele za Mungu kwa ajili ya makabila mengine 11? Na Je! Baada ya Kuhani mkuu, Yesu Kristo, kuingia pa Takatifu pa Patakatifu, kwa Damu yake mwenyewe, na kufanya upatanisho kati ya wanadamu na Mungu, je! Bado kuna Walawi na makuhani “katikati yetu na Mungu” ambao pasipo hao hatufiki pa Takatifu pa Patakatifu?

Kwa habari ya Wajane. Kumbuka mjane ni yule aliyefiwa na mumewe, ila kuna sifa za muhimu za kuangalia: Kwanza, hana kipato au watu wa kumsaidia katika watoto au jamii ya karibu. Kwa mfano, mama yangu mzazi ni mjane, ila watoto wake wana kipato cha kutosha kumtunza mama. Mtume Paulo anasema “tujifunze kuwajibika kwa jamaa zetu ili tusielemee kanisa”. Hapa Paulo anajua kwamba wajane wanasaidiwa na kanisa, ila kuna tofauti ya mjane na mjane. Pili, kuna umri wa mtu kuwa mjane “hasa”. Mjane “hasa” umri wake ni miaka 60 au zaidi (hapa inamaanisha mwanamke amepungukiwa na nguvu kimwili, au hakuna uwezekano wa kuolewa tena na hana kipato cha uhakika). Paulo anashauri wasichana waliofiwa na waume zao mapema waolewe tena. Soma maandiko na uongozwe na Roho Mtakatifu kujua mambo haya, kwa maana iko baraka katika KUWATUNZA wajane (hasa), masikini, yatima na wahitaji wengine, bila kuwasahau watumishi wa Mungu aliye hai, ili kazi ya huduma iendelee na mwili wa Kristo ujengwe.

Amani ya Kristo iwe nanyi tangu sasa na hata milele. AMEN.

Frank Philip.

Comments