ASILIMIA MIA

Na Frank Philip

[Wewe ni 100% Tangu Kuzaliwa, Je! Umeweza Kufikia Ngapi hadi sasa?]

“Neno la BWANA lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto” (Yeremia 1:4-6).

Mara nyingi watu wanadhani wanatengeneza “future” (hatima) zao, nakupa habari mpya kama hujajua, hakuna mtu anaweza kuumba jambo ambalo halikuumbwa tangu mwanzo; KILA uonacho, kiwe ni kitu, nafasi, makazi au nyakati, vilikwisha-umbwa na kuamriwa tangu zamani.

Ona jambo hili, wakati Yeremia anakua, hakujua kwamba Mungu alimjua kwa jina lake; hakujua kwamba Mungu alikuwa anamwona kama nabii, japo yeye anajiona ni mtoto tu; hakujua kwamba ni mtu mkuu sana, hadi siku Mungu alipomwambia, Yeremia hakujua. Hata sasa wapo watu wengi sana, hawajui MIISHO yao; wanajua kueleza HISTORIA zao, na mambo yanayotokea sasa, ila Mungu anajua MIISHO kabla ya mianzo, huko mbele sana kwenye hatma (future) yako; huwezi kujua miisho yako kama huna connection (mawasiliano mazuri) na huyu Mungu.

Nitakuonesha jambo, BWANA anasema kwa kinywa cha nabii Isaya, “Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima” (Isaya 49:15-16). Kama unadhani umesahulika, au Mungu hakuoni unachofanya, jua kwamba UNAJIDANGANYA, Mungu anakufuatilia kuliko ambavyo “mama yako mzazi aanafanya”.

Angalia tena, “Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu” (Matendo 17:24-27).

Mtume Paulo akijua siri hii, anasema, Mungu alifanya ulimwengu na VITU VYOTE (yaani wewe na kila udhanicho kimo duniani), akafanya KILA taifa, na kutuwekea MIPAKA ya MAKAZI, na kuweka NYAKATI (yaani, mambo yanayotokea kwa wakati fulani. Ukisikia Nyakati ni matukio na muda/wakati kwa pamoja).

Sasa ngoja tutumie mfano rahisi kujifunza hili somo. Mungu alipowatoa wana wa Israel kule Misri, Aliwaambia MWISHO wa safari yao, na MALENGO yake, na BARAKA zote alizoamuru juu yao. Safari ya kutoka Misri kwenda Kaanani ni takriban siku chache tu kwa njia ya miguu. Sasa ona jambo hili, ni kweli walipewa AHADI zilizo bora, ni kweli walijua MWISHO wao ulivyo mwema (nchi iliyojaa asali na maziwa); ILA ni Joshua na Kalebu tu, kati ya watu zaidi ya MILIONI moja waliotoka Misri, walionja hiyo asali na maziwa waliyoahidiwa.

Tazama jambo hili, Mungu HAKUPI kitu kilichokuzidi UFAHAMU na IMANI yako. Iko hii shida chini ya jua, naam, inaumiza sana, MWANA awapo MJINGA, biblia inasema huyo hana tofauti na MTUMWA, kwa maana HAJUI mambo ya BABA yake, wala mambo ya NYUMBANI! Sasa ona tena, wana wa Israel hawakuwa TAYARI kuvuka Yordan, kuingia Kaanani kwa sababu hawakumpendeza Mungu katika njia zao. Ghafla tu wametengeneza SANANU, na kuanza kuiabudu, eti, kisa wako peke yao na Musa hayupo, hawakujua ile DHAMBI yao ya SIRI (wakati kiongozi wao au mtu hawaoni) ingeweza kuwanyima kufikilia asilimia mia (100%) ya ahadi (MAONO) Mungu aliyowaahidi.

Nasikitika kusema kwamba, hata leo, Mungu akitazama BARAKA na NAFASI za watu wengi kati yetu, anaoona mambo makubwa, ILA sio wote watafikia 100% ya hizo ahadi/nafasi Mungu alizoweka maishani mwao; wengi sana watafia jangwani kabla ya kufikia 100% ya makusudi ya Mungu. Kwa mfano, ukiona mtu anazini, eti, kwa sababu mumewe/mkewe amemuudhi, hana tofauti na wana wa Israeli, walivyokuwa wanamtenda Mungu dhambi kwa kuabudu SANAMU, nk. (usisahau kwamba imeandikwa UZINZI ni ibada ya sanamu!); ona hapa “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu” (Wakolosai 3:5,6). Sasa, wakati unadhani unamkomoa mwenzako, kumbe! Hujui kwamba unarefusha safari yako ya kuzunguka jangwani kama wale wana wa Israel! Mungu anakuona unavyabudu sanamu, hata kama una majina matakatifu sana kama KUHANI Haruni, haijalishi; ibada ya sanamu itakugaharimu kufikilia hatma (future) yako. Wana wa Israel wakatembea jangwani miaka 40, wakafa bila kufikia 100% ya lile kusudi la Mungu.

Nataka ujue jambo hili, iko MIPAKA ya makazi (Mdo. 17); huwezi kuishi kokote tu utakapo ukawa na amani. Jua kwamba kuna NYAKATI (matukio na muda) zimeamuriwa juu yako, huwezi kuziepuka, ila utazipita kwa ushindi na amani kulingana na IMANI yako na KIWANGO chako cha kumjua Mungu wako. Kumbuka siku zote, ukimjua SANA Mungu, utakuwa na amani, na NDIPO mema yatakapokujilia (Ayubu 22:21). Katika safari ya kufikilia 100% ya hatma yako, kuna magumu mengi na shida nyingi; BWANA anatutia moyo kwa kusema “ulimwenguni mnayo dhiki nyingi lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu”. Dhiki, shida na mateso yatakuwepo tu madamu upo njiani, na mateso hutokezea kwa wale watu wa karibu nawe kabisa, jichunge nafsi yako; jua nyakati/saa ya kujaribiwa kwako, usimtende Mungu dhambi ukaharibu hatma yako kwa sababu ya mtu mwingine. Kukasirika ni ruksa, ila USITENDE dhambi.

Watu wengi wanadhani nafasi, na hatua walizofikia ni kwa nguvu zao; kweli wametumia nguvu, akili, na jitihada, ila HAKUNA uumbaji zaidi ya ule wa Mungu; njia zako ZIMECHORWA vitangani mwa mikono ya Mungu tangu zamani; na sio kuchorwa tu, kuna MIPAKA (Mdo. 17), huvuki hapo, kazi yako ni KUTOKUWA mlegevu katika kumtafuta Mungu, na kumshukuru kwa hapo ulipofika, ila jiulize, Je! Umefika asilimia ngapi kati ya zile 100% alizoziamuru Mungu juu yako? Unaweza kudhani umefika mbali; hutaamini ukijua, kumbe! ULIKOTOKA ni KARIBU kuliko UNAKOKWENDA. Janga kubwa juu ya nchi, ni pale unapozunguka miaka 40, ukidhani uko KAZINI, kumbe uko jangwani tu, unakula mana/chakula cha njiani tu; kumbe kinachokuweka hapo NJIANI ni kale ka-kahaba kanakokuzuzua, ile rushwa pale kazini kwako, nk. VUKA hapo mahali, GEUKA, mrudie Mungu, HARIBU “yule ndama wako wa dhahabu” unayemwabudu SIRINI, utaona ukivuka hatua za Baraka zako.

Mungu anakujua kwa jina lako; Mungu anajua cheo chako; Mungu anajua kiwango cha baraka zako; huna jambo jipya unafanya zaidi ya KUMTAFUTA hata kwa kupapasa-papasa, ili umuone! Yuko hapo karibu na wewe kuliko unavyodhani; kuna MIISHO yako myema sana, je! Unijua? Hadi sasa umefikia asilimia ngapi kati ya zile 100 Mungu alizokwisha kupa?

Frank Philip

Comments