JE, MUOTA NDOTO ANAWEZA KUFA KABLA YA NDOTO YAKE KUTIMIA?

 Na AP Hosea Shaban, Ufufuo na Uzima Moshi
 Mwanzo->45:1-9
 Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze. Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia.

Majeshi ya bwana wakisiliza neno
Yusufu akawaambia ndugu zake, “Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake.
Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri.

Basi sasa, msihuzunike, wala msihudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna.

Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu. Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri.

Fanyeni haraka, mmwendee baba yangu, mkamwambie, Hivi ndivyo asemavyo mwanao Yusufu, Mungu ameniweka kuwa bwana katika Misri yote, basi unishukie, usikawie.”
AP Hosea akimwombea huyu mama

Kila mtu anayo ndoto kwa habari ya maisha yake. Lakini wapo wajanja wa mjini ambao ni wajumbe/watumishi wa shetani huku duniani wenye uwezo wa kufunika ndoto ya mtu. Pia ni muhimu kufahamu ya kwamba humu duniani kuna watu wasiofaa kwenye maisha ya mtu.

Tunaona ya kuwa ndugu zake Yusuph walimtenda mabaya ili wamwuangamize, lakini ashukuriwe Mungu  nduguze na Yusuph walikuwa daraja la yeye kupanda juu kupitia nyota yake.

Yamkini umekuja leo kwenye nyumba ya Ufufuo na Uzima na umeshindwa kupiga hatua kwa sababu ya ndugu, mchumba, mume au mke amekuacha wala usiwe na wasi wasi kwa maana inakuja siku ambayo Mungu atasababisha ndoto yako itimie kwa namna yeyote,


Tena usiogope kwa maana lile jaribu au pito unalopitia ni la muda tu kwa sababu hakika halitakuangamiza na ni Mungu ameruhusu usiangamie  ili adui/watesi wako washuhudie na kuliona lile jambo jipya litakalotokea kwa maana historia ya maisha yako itabadilika.

Ni kweli yawezekana sasa hivi watu wanakudharau kulingana na hali ngumu ya maisha unayopitia, Ila usiogope kwa maana lipo jambo ambalo Mungu atalifanya maishani mwako litakalowasababishia adui na watesi wako wanapenda au wasipende!!!

Historia ya maisha yako ni lazima itabadilika acha waendelee kijivuna wanachojivunia ila wewe mkamate Yesu Kristo pekee ili ujivunie yeye.


Pia tunaona mfano mzuri kwenye biblia wa Gidioni alikuwa anajiona ya kuwa hafai kama wewe unavyojidharau na kujiona ya kuwa haufai. Mungu anasema unafaa. Nakutangazia hautakufa kabla ndoto zako kutimia katika jina la Yesu Kristo wa nazaret. 

Comments