KANISA KAMA SHAMBA LA MIZABIBU

Leo, tunajifunza Biblia kutoka katika MATHAYO 20:1-16.  Kuna mengi ya kujifunza katika
mistari hii.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele
vitatu:
(1)AJIRA KATIKA SHAMBA LA MIZABIBU (MST. 1-10);
(2) WIVU JUU YA KARAMA WALIZOPEWA WENGINE (MST. 11-15);
(3) WA KWANZA KUWA WA MWISHO, NA WA MWISHO KUWA WA KWANZA (MST. 16).

(1)      AJIRA KATIKA SHAMBA LA MIZABIBU (Mst. 1-10)
Katika mistari hii tunajifunza mengi kuhusu ajira katika shamba la Mizabibu:

1.         MWAJIRI NI MTU MWENYE NYUMBA – Mtu mwenye nyumba anayetajwa hapa ni Mungu mwenyewe (WAEBRANIA 3:6; WAEFESO 2:19).  Mungu ni mmojawapo wa Waajiri wa roho za watu.  Mwajiri mwingine ni Shetani.  Kila mtu ni lazima awe mtumwa wa mmoja wa waajiri hao.  Aidha mtumwa wa haki yaani mtumwa wa Mungu au mtumwa wa dhambi yaani mtumwa wa Shetani (WARUMI 6:17-18).  Ni juu ya kila mtu kuchagua ataajiriwa na nani, na kumtumikia; Mungu au Shetani.    Yoshua alichagua kuajiriwa na kumtumikia Mungu na kuwa mbali na dhambi au Shetani, sisi nasi inatupasa tuwe hivyo daima (YOSHUA 24:1).
2.         MUNGU HUTAFUTA KUWAAJIRI WATU WALIOSIMAMA SOKONI –Sokoni palikuwa ni mahali pa kila namna ya michezo ya wakubwa na watoto (MATHAYO 11:16).  Michezo hii ni pamoja na kamari na bahati nasibu.  Ni kinyume na mapenzi ya Mungu kucheza kamari au bahati nasibu ya AINA YOYOTE.  Iwe ni bahati nasibu ya papo kwa papo au bahati nasibu ya vizibo vya soda.  Tendo lolote lisilotokana katika imani ni dhambi (WARUMI 14:23).  Mambo yote ya kamari na bahati nasibu, yanahusiana na mungu Bahati ambaye watu walimtolea dhabihu ili awape bahati (ISAYA 65:11-12) na ni machukizo mbele za Mungu.  Sokoni pia ni mahali palipojaa mizaha ambayo ni dhambi ya mauti (MITHALI 19:29), uongo (WAKOLOSAI 3:9), wizi (WAEFESO 4:28), matusi na kila namna ya ubaya (WAEFESO 4:31).  Sokoni ni mahali ambapo watu wanakutana na kupanga mambo ya uasherati na uzinzi ambayo hayapaswi kutajwa kwa kila mtakatifu (WAEFESO 5:3).  Vilabu vingi vya pombe pia hujengwa karibu na masoko, sehemu mbalimbali.  Sokoni ni mahali penye watu wengi ambao wameajiriwa na Shetani na kuwa watumwa wa dhambi.  Hapa wanafanya kazi ya dhambi ambayo ni sawasawa na kukosa kazi, maana ni kazi ambayo haina faida yoyote kwa mtu hapa duniani, na zaidi sana katika maisha ya milele (MITHALI 10:2).  Injili ni hekima inayopaza sauti yake na kuwataka watu watoke hapa sokoni na kuajiriwa na Mungu (MITHALI 1:20-21).  Kila mmoja anapaswa kuisikia sauti hii na kukubali ajira ya Mungu na kuokolewa kutoka katika mauti.
3.         KUAJIRIWA SAA MBALIMBALI – Saa za mchana, ni umri wa maisha ya mtu tangu alfajiri hata jioni.  Huu ndiyo wakati anapoweza kuajiriwa na kufanya kazi ya Mungu duniani.  Ni muda ambao mtu anapoweza kuiona nuru ya ulimwengu.  Jioni mtu hufa na kuyakabili maisha baada ya kufa yaani usiku mtu asipoweza tena kufanya kazi ya Mungu (YOHANA 9:4; 11:9).  Wengine wanaajiriwa yaani kuokolewa katika alfajiri ya maisha yao yaani katika utoto, kama Timotheo na Yeremia (2 TIMOTHEO 3:15; YEREMIA 1:4-6).  Wengine wanaokolewa saa tatu yaani katika ujana wao kama Obadia (1 WAFALME 18:7-12).  Wengine saa sita wakiwa nusu ya umri wao.  Wengine saa tisa, wakiwa watu wazima kama Petro aliyeokolewa akiwa ameoa tayari, wengine saa kumi na moja katika uzee au mwishoni mwishoni mwa maisha yao kama mhalifu msalabani.  Wote hawa mshahara wao ni mmoja tu dinari moja, kama wakiwa waaminifu hadi mwisho.  Dinari hiyo ni uzima wa milele.

4.         WITO WA KUFANYA KAZI KATIKA SHAMBA LA MIZABIBU – Baada ya kuokolewa wito wa Mungu kwetu, ni kututaka tufanye kazi katika Shamba la Mizabibu.  Wito huu anaurudia tena na tena kwa kila mtu anayemuajiri au kumuokoa (Mst.1-2,4,7).  Wengine hutii na kwenda kufanya kazi katika Shamba la Mizabibu lakini wengine hawataki kwenda (MATHAYO 21:28-31).  Shamba hili la Mizabibu la Mungu ni KANISA la Mungu (1 WAKORINTHO 3:9).  Kila mtu baada ya kuokolewa, inampasa kujiunga na Kanisa na siyo kukaa mwenyewe tu na kufanya mambo yake mwenyewe.  Ajitengaye  na wenzake, hutafuta matakwa yake mwenyewe na kushindana na shauri jema (MITHALI 18:1).  Kila mtu aliyeokoka ni jiwe moja au tofali ambalo linapaswa kuunganishwa na mengine na kufanywa kuwa Jengo la Mungu au Kanisa.  Ni rahisi kuiba tofali lililotupwa mchangani, kuliko tofali lililounganishwa na wengine katika Jengo.  Shetani ni rahisi kumuiba mtu ambaye hajiungi na Kanisa (1 PETRO 2:5).  Hata hivyo, Shamba kubwa la Mungu duniani kote, limegawanywa na Mungu mwenyewe katika mashamba mengi ya mizabibu kama Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatra, Sardi, Filadelfia, Laodikia, Kolosai, Korintho, Thesalonike n.k.  Kila mtu aliyeokoka, hapaswi kuzungukazunguka tu kila mahali katika kila Kanisa bali achague KANISA MOJA ambalo litakuwa Shamba lake la Mizabibu ambalo atafanya kazi humo tu.  Tuna ruhusa ya kuzungungukazunguka au kutangatanga pale mwanzoni tu kwa kutafuta Kanisa ambalo ni lulu nzuri, penye mafundisho ya Uzima (MATHAYO 13:45-46).  Baada ya kulipata, tunapaswa kufanya kazi katika Shamba hilo tu la Mizabibu.  Katika Shamba la Mizabibu tunalima, kupanda, kupalilia, kutilia Samadi, kutia maji n.k. na siku ya mwisho ya hukumu, Mungu anataka kila mmoja aonyeshe MATUNDA kwake (LUKA 13:6-9).  Ili kupata matunda, mkulima anafanya kazi ya kila siku katika shamba moja.  Siku ya mwisho kila mtu atatoa hesabu ya kazi aliyoifanya katika shamba lake la mizabibu, na kuzungukazunguka katika kila Kanisa na kuacha shamba lako la mizabibu hakutakufaidia siku ya mwisho.  Mtu anayezunguka tu na kufanya kazi kwenye mashamba ya wengine, na kuacha shamba lake la mizabibu atakuwa mweusimweusi tu kutokana na jasho lake, na asipate kitu siku ya mwisho (WIMBO ULIO BORA 1:5-6).  Mtu anayeliacha Shamba lake la Mizabibu limee miiba na viwavi, ni mtu asiye na akili.  Inatupasa leo tujifunze kutoka kwake tusiwe kama yeye (MITHALI 24:30-32).  Baada ya kuokolewa inakubidi  kuchagua Kanisa moja tu ambalo utatoa vyote ulivyo navyo hapo ili upate matunda ya kumwonyesha Mungu.  Iwe ni kushuhudia, kufuatilia, kufundisha, kutoa fedha na mali zako n.k., vyote vihusiane na Shamba lako la Mizabibu.  Hata ukienda nje ya nchi, vyote unavyopata, vitoe kwenye shamba lako la mizabibu!  Mtu yeyote anayezunguka kufanya kazi katika mashamba mengine ya mizabibu, na kuacha la kwake hatachukua matunda kutoka huko! (KUMBUKUMBU 23:24).  Tunaagizwa pia kufanya biashara hata atakapokuja Yesu (LUKA 19:13).  Mfanyabiashara ili ajue faida yake atakuwa na mahali maalum pa kufanyia biashara hiyo na kupiga hesabu zake kila siku.  Yesu atapiga hesabu nasi atakaporudi (LUKA 19:15).  Lazima tuwe na mahali maalum pa kufanyia biashara ambapo tutaliambia Kanisa hilo yote (MATHAYO 18:17).  Kuwa na magari kumi yote mabovu yasiyotembea, ni kuwa tajiri wa vibovu.  Inatupasa kuyakongoroa tisa na kutengeneza MOJA litembee.  Shamba la Mizabibu au mahali pa kufanyia biashara tutakapochagua ni lazima liwe Kanisa lililojaa Utakatifu (WAEBRANIA 12:14) na siyo lolote tu.

5.         SAA YA KUPOKEA UJIRA AU MSHAHARA – Mshahara wa siku wa mwajiriwa unapaswa kutolewa siku ile ile jioni na haupaswi kukaa kwa mwajiri usiku kucha hadi asubuhi (WALAWI 19:13; KUMBUKUMBU 24:14-15).  Vivyo hivyo, mshahara wa mtu ni baada tu ya kufa kwake mwisho wa mchana wake na siyo mpaka asubuhi ya kufufuka!  (WAEBRANIA 9:27).  Mshahara wa dhambi ni mauti ya milele mara tu baada ya kufa na karama ya haki ni uzima wa milele (WARUMI 6:23).  Inatupasa kutenda kazi ya Mungu kwa bidii sana sasa!  Huenda wengine wetu tuko saa ya jioni kabisa na kufa kwetu kunakaribia.  Tukiitenda kazi kwa bidii na kwa uaminifu katika yale tuliyopewa kuyatenda, tutapata thawabu zilezile za watu wa Kanisa la Kwanza walioajiriwa alfajiri na asubuhi.  Vile vile Wayahudi waliajiriwa kwanza, na Wayunani au Mataifa kama sisi Watanzania, tumeajiriwa saa 11 jioni, mwishoni.  Hata hivyo mshahara wetu ni mmoja uzima wa milele, hakuna tofauti ya Wayahudi na Wayunani (WARUMI 1:16; WAGALATIA 3:28).

(2)      WIVU JUU YA KARAMA WALIZOPEWA WENGINE (Mst. 11-15)
Wayahudi au Waisraeli waliitwa kwanza kuwa watoto wa Mungu, miaka mingi sana kabla ya Mataifa.  Mataifa waliajiriwa saa 11 jioni.  Sasa Wayahudi wananung’unika kwa nini Mataifa nao wapewe uzima wa milele kama wao!  (MATENDO 11:1-18).  Hatupaswi kunung’unika na kuona wivu tunapoona fulani amepewa karama fulani na Mungu bali kunyamaza.  Kinyume cha hapo, tunapingana na Mungu.  Je, si halali yake Mungu kutumia vilivyo vyake kama apendavyo?  (MATHAYO 20:15).  Hugawa karama kama apendavyo yeye (1 WAKORINTHO 12:11).  Ni muhimu kutulia na kufahamu kwamba hakuna mtu atakayetoa hesabu kwa karama asiyopewa.  Aliyepewa vingi vitatakwa vingi pia kwake.  Kila mmoja awe mwaminifu tu kuzifanyia kazi zile talanta alizopewa! LUKA 12:48; 19:15-23).  Hatupaswi kuwa na wivu usiokuwa na faida kama Sauli (1 SAMWELI 18:8-9).

(3)      WA KWANZA KUWA WA MWISHO, NA WA MWISHO KUWA WA KWANZA (MST.16)
Mitume walivimba kichwa baada ya kuelezwa yale watakayoyapata kwa kumfuata Yesu (MATHAYO 19:27-29).  Hata hivyo inaelezwa hapa ni kwa kuvumilia hadi mwisho (MATHAYO 24:13).  Aliyeajiriwa alfajiri, saa tatu, saa sita, tisa, kumi na moja, avumilie hadi mwisho au siyo ataachwa na kupitwa (YOHANA 20:3-8).  Paulo alitenda kazi kuliko mitume wote.  Tukazane na kutolegea hadi mwisho au siyo tutapoteza yote (WAEBRANIA 3:14; 2 YOHANA 1:8).
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

 
Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe     tembelea sehemu zifuatazo katika inernet  
Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe



Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Comments