KILA ATENDAYE DHAMBI NI MTUMWA WA DHAMBI.

Na mtumishi wa MUNGU Gasper Madumla
Imeandikwa;
" Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi" Yoh.8:34

Bwana Yesu asifiwe...
Awali ya yote nikuambie kwamba yeyote atendaye dhambi hupendezwa nayo na kuifurahia,na kuiona kama ni kitu kitamu.Hivyo yeye atendaye dhambi hufanya kazi ya kuitumikia kwa kujua au hata kwa kutokujua.
Siku ya leo Bwana anatuambia kwamba kama tunahitaji kuwa huru basi hatuna budi kuacha kutenda dhambi.

Kwa lugha nyingine kupitia andiko lilo hilo ( Yoh.8:34) ni sawa na kusema;
" Kila asiyetenda dhambi yupo huru."

Jambo moja ninalolijua kwa uhakika wote ni kwamba,hakuna mtu chini ya jua hili awezaye kuacha dhambi kwa kutumia akili zake au ujanja wake yeye mwenyewe. Hata mimi mwenyewe jinsi nilivyo hivi sasa sio kwa sababu ni mjanja sana au sababu nina akili. Bali sote tunao uwezo wa kucha kutumikia dhambi kwa kuwezeshwa na Roho mtakatifu baada ya kuokoka. Bila Roho wa Bwana hakuna awezaye kuacha kutenda dhambi.
Kwa lugha nyepesi ni hii;
•Tusipookoka tu watumwa wa dhambi.
Maana kamwe hatuwezi kuwa huru mbali na dhambi pasipo kuokoka na kuishi kama Bwana atakavyo.

Bwana Yesu asifiwe...
Kumbuka leo,Bwana Yesu anatuambia;
" Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi" Yoh.8:34

Labda kabla sijakusogeza mbele kidogo katika fundisho hili,ngoja nikupe mfano huu;
Mfano;
Palikuwa na watoto wawili wa baba na mama mmoja,watoto hawa walifunga safari hadi kwa bibi yao huko kijijini. Bibi yao alikuwa ni mfugaji.
Siku moja watoto hawa wakiwa shambani wakicheza pamoja,gafla mtoto aliyekuwa mkubwa alimrushia jiwe bata wa bibi yake na hapo hapo yule bata akaanguka na kufa.

Wakati mtoto huyo alipokuwa amempiga bata kwa jiwe kumbe mdogo wake alikuwa akimuangalia,sasa mdogo wake akaja na kumwambia " Aaha! Umemuua bata wa bibi kwa jiwe,naenda kumwambia bibi,utakoma leo..." yule dada mtu akasema usimwambie mdogo wangu. Kisha yule dada akamfukia bata kimya kimya wala hakuna ajuaye ila mdogo wake tu aliyekuwa naye shambani.
Sasa ;
Waliporudi kutoka shambani wote wawili,yule mdogo mtu akakataa kufanya kazi yoyote ile,kisha kila kazi iliyokuja mbele yake aliisukumia kwa dada yake,na kumwambia;
" Nifanyie kazi zangu,na ole wako usipofanya kazi zangu zote,maana ntamwambia bibi jinsi ulivyomuua bata wake na kumfukia chini kimya kimya !"

Basi hatimaye dada mtu akawa mtumwa wa dhambi,maana alifanya kazi nyingi sana akiogopa kusemewa dhambi yake. Akawa mtumwa wa dhambi. Akapelekeshwa na dhambi pasipo hata kupenda.
Ndivyo ilivyo hali ilivyo sasa,watu wengi hujikuta tukitumikia mambo mengi tusiyoyapenda sababu ya DHAMBI kwamba tumekataa kurejea kwa BWANA MUNGU kwa toba,tuokoke na kuanza maisha mapya ya wokovu.Eeh MUNGU akusaidie sana wewe ikiwa kama ni mmoja wa watu walio wafungwa kwa habari ya dhambi.
Mimi nimeona jambo hili chini ya jua likichukua nafasi kubwa sana. Utakuta mtu akiikimbilia dhambi na ikiwa ameikosa dhambi hiyo kuifanya,basi hujutia kwa nini ameikosa dhambi hiyo kwa muda hule. Yaani badala ya kushukuru kwamba ameepushwa na dhambi,badala yake huchukia eti kwa nini hakufanya dhambi?
Mfano;
Mtu mwenye " kideti" na binti kwamba wamepanga wakazini,kisha ikatokea huyo binti hakutokea siku hiyo,hapo mtu huyo hujilaani vikali kwamba kwa nini kamkosa kwa muda huo! Maana anachokisiktikia ni kwamba kwa nini kaikosa dhambi ya uzinzi?
Mtu wa namba hii ni mtumwa wa dhambi!

Au
Mtu huacha maombi kanisani,na kukimbilia kuangalia matamthilia kwenye luninga.Huo nao ni utumwa wa dhambi.

Bwana Yesu alipowaambia wale Wayahudi ya kwamba ninyi ni watumwa wa dhambi,wao Wayahudi wakambishia na kumwambia;
" Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru? " Yoh.8:33
Mara nyingi mtumwa wa dhambi hajitambui kwamba ni mtumwa. Maana huzani kwamba yote ayafanyayo yapo sawa wakati si sawa.
Na wala mtumwa wa dhambi hawezi kumgundua mtumwa mwezake maana wote hufanana,ndio maana hata Waswahili wakasema ;
" huwezi kuuona msitu ukiwa ndani ya msitu,bali ukitaka kuuona msitu sharti uwe nje ya msitu "

Huwezi ukamuona mwenzako kwamba ni mtumwa ukiwa na wewe ni mtumwa,sharti kwanza wewe uwe safi ndipo uweze kuona.
Dawa ya kuwa huru ni kujisalimisha kwa Bwana Yesu kwa kuokoka na kisha Roho mtakatifu Yeye mwenyewe atakata kila kiu ya dhambi ndani yako na hatimaye hutakuwa mtumwa wa dhambi maana dhambi haitakuweza shauli ya uwepo wa Roho mtakatifu ndani yako.
Wakati uliokusudiwa ndio sasa,
Wakati wa kurejea kwa Bwana kwa toba.
Wakati wa kumpa Yesu maisha yako,wakati wa kuokoka ndio sasa.

Sikia;
Yawezekana umeokoka lakini bado U mtumwa wa dhambi,sababu ndani yako hakuna KWELI.
KWELI ni neno la Mungu ( Yoh.17:17 )
KWELI ikijaa kwa wingi ndani yako,basi kamwe huwezi kuwa mtumwa wa dhambi.

Nahitaji niombe na wewe siku ya leo,
Usisite kunipigia simu yangu hii hapa chini;
0655-111149.

UBARIKIWE.

Comments