KUMTUMIKIA MUNGU KWA MOYO NA NAFSI YAKO.

Na Frank Philip


“Lakini mjibidiishe sana kuzifanya amri na sheria, ambazo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwaamuru, kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kwenenda katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na kushikamana na yeye, na kumtumikia kwa moyo wenu wote na nafsi yenu yote” (Yoshua 22:5).

Kuna jambo hili juu ya nchi, je! Umewahi kujiuliza tofauti ya mtu AJIZUIAYE kufanya jambo kwa KUOGOPA adhabu, na AJIZUIAYE kwa KUMPENDA au KUMHESHIMU aliye mkataza kufanya jambo hilo? Wote wawili WAMEJIZUIA, tena kwa bidii, mmoja kwa kuogopa adhabu, na mwingine kwa kutaka KUMPENDEZA aliyeagiza/amuru (kwa sababu ya upendo na heshima kwa Bwana aliyeagiza). Je! Watu hawa wawili wako sawa?

Hata siku moja, hawa watu wawili hawako fungu moja, japo wote kwa jinsi ya NJE wako sawa, ndani yao ni watu tofauti mbele za BWANA wao. Nikitazama jambo hili, ndipo nikajua ni kwanini Mungu huchunguza MIOYO na VIUNO. Nikatazama tena nikaona jambo hili, “haijalishi sana UNASEMA nini kwa kinywa chako, au KUTENDA nini, ila unawaza nini moyoni mwako”. Ni kweli kabisa kwamba huwezi kunena au kutenda bila kuwaza, ila unaweza kuwaza kingine na ukatenda kingine, sio kama uwazavyo ila kama MAZINGIRA yalivyo; nidhamu ya uoga, ili kuwapendeza watu fulani.

BWANA akiona jambo hili akakemea wale waliokuwa wakijiita “watu wa Mungu”, yaani Mafarisayo na viongozi wengine wa dini. Ona hapa, “Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu” (Mathayo 15:7-9). Ni rahisi sana kunyooshea MAFARISAYO vidole, kumbuka siku zote, Bwana YESU hakupambana na vyeo vyao, wala nafasi zao, ila namna walivyokuwa mbele za Mungu (mioyo na nafsi zao). Matendo yao yalikuwa SAFI, tena watii wa SHERIA, ila mioyo yao ilikuwa mbali na Mungu. Je! Hata leo si wapo wengi wa namna hii? Je! Itamsaidia nini mtu kuwa mkamilifu kwa matendo (kwa sababu ya kuogopa sheria au watu) kisha Mungu akichunguza moyoni anaona uozo tu? Umesahu BWANA alipowafananisha watu na makaburi yaliyopambwa nje huku ndani kuna mifupa tu?

Joshua alijua jambo hili na kuwaonya wana wa Israel, kwamba waangalie, “KUMPENDA Bwana Mungu, na kumtumikia kwa moyo WOTE na nafsi YOTE”. Kati ya wana na Israel, wapo ambao waliogopa kutenda dhambi kwa sababu walijua WATAPIGWA (kama wenzao walivyomkasirisha Mungu wakaangamia), sasa wamekuwa wapole; na kuna wengine waliogopa kutenda dhambi kwa sababu ya KUMCHA MUNGU. Ona tofauti ya makundi haya mawili, na ujichagulie mwenyewe; ukitaka kutenda kwa namna ya kuwapendeza wanadamu, na sio Mungu ni juu yako, jua humdanganyi Mungu, unajidanganya mwenyewe na kujilisha upepo. Nakupa shauri, jifunze kumtumikia Mungu kwa MOYO na NAFSI safi, kabla ya huduma na matendo yako mbele za watu, nawe utakuwa umechagua fungu jema.

Frank Philip.

Comments