KUTAFAKARI UZIMA.

Na Frank Philip


“Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana” (Joshua 1:8).

“Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa” (Zaburi 1:1-3).

Kutafakari (meditation) sio jambo rahisi, hasa kutafakari kwa utulivu na kwa “kuzama”. Kutafakari ni KITENDO cha kupitisha jambo fulani katika nafsi yako, na kulitazama kwa namna ambayo unaweza kuliona kama picha ndani yako, au mara nyingine kusikia sauti ndani yako.

Katika kutafakari, mtu anaruhusu NGUVU fulani iachiliwe kupitia lile jambo analolitafakari ndani yake. Sasa, mtu akitafakari jambo jingine lolote ambalo sio Neno la Mungu, pia iko nguvu inaachiliwa. Kwa mfano, wale watu wafanyao “yoga meditation” hupokea nguvu fulani ambayo wao wanaiita “chi” au “qi” energy. Mfano mwingine, ukitafakari sana mambo ya kuumiza na kuudhi, utasikia maumivu ya moyo, hasira na hata mara nyingine ugonjwa wa moyo unaweza kuachiliwa mwilini mwako. Jua nguvu ya kutafakari na ujifunze kutafakari mambo ya kujenga, nawe utafanikiwa sana.

Kwa bahati mbaya sana, Wana wa Mungu hawajui siri katika kutafakari Neno. Shida nyingine inakuja pale ambapo watu hawajui JINSI ya kutafakari. Kuna tofauti ya KUKUMBUKA jambo na KULITAFAKARI hilo jambo. Kukumbuka ni kitendo cha kurudisha jambo katika fahamu zako kama picha tu, ILA kutafakari ni mchakato ambao mtu atawaza na kufikiri juu ya jambo fulani, huku akilitazama kwa makini, tena kwa msisitizo bila kuingiliwa na kuvurugwa na mawazo au mambo mengine yanayoendelea katika mazingira yanayomzunguka. Najua sio mara nyingi mtu ataweza KUZAMA katika kutafakari Neno kwa muda mrefu, ila imekupasa kujitahidi “kutafakari Neno mchana na usiku”.

Umewahi kujiuliza ni kwanini watu wanabeba shanga mkononi, na wanazihesabu kwa vidole kila mahali wanapokaa au kutembea, bila kujali kama kuna mtu anawaona? Unadhani ni urembo? Hapana! Wako kazini. Ukiwaruhusu waseme kwa sauti, utasikia maneno wanayotamka ndani ya mioyo/nafsi zao. Sasa, mara nyingi wanajitahidi “kutafakari” au “kusali”, na katika hayo wanapata nguvu fulani. Sasa, kutumia shanga ni kusaidia akili isihame (concentration) hapo anapotafakari ili waweze kuzama katika hilo jambo wanalotafakari bila kuvurugwa.

Joshua aliambiwa hii siri mapema; kwamba akitaka “kufanikiwa na kusitawi sana”, asiache kutafakari Neno usiku na mchana. Ona jambo ambalo Daudi anasema juu ya mtu anayetafakari Neno usiku na mchana, huyo “amefananishwa na mti uliopandwa kando kando ya vijito vya maji, uzaao matunda yake kwa majira yake, na kila atendalo litafanikiwa”.

Nataka uone jambo jingine. Ukiangalia katika Joshua 1, utaona kuna “kunena”, “kutafakari” na kisha “kutenda” Neno. Ukiangalia kwenye Zaburi 1, utaona huyu mtu aliyefananishwa na mti, “anaendenda” kwa namna fulani, “kupendezwa” na sheria ya Bwana (Neno), kisha “kutafarari” juu ya hilo Neno mchana na usiku. Sasa ninachotaka kukuonyesha hapa ni uhusiano wa kuweza “kunena”, “kutenda” na “kutafakari” Neno. Mtu hunena mambo yaujazayo moyo wake; kadri unavyolijaza Neno, na kulitafakari sana, utagundua maneno yako yanabadilika kwa sababu mawazo yako yamebadilishwa na hilo Neno ndani ya moyo wako.

Moyo uliojaa Neno, una tabia ya kuhusianisha mambo na Neno la Mungu. Ukiona au ukisikia jambo, ghafla! Unasikia mstari fulani wa biblia unaibuka ndani yako kuhusiana na hilo jambo. Sasa ukikaa katika hali hiyo ya kutafakari na kutazama mambo kwa kioo cha Neno la Mungu, unaanza kuwa mtendaji wa Neno kwa wepesi zaidi, kwa sababu lile Neno linaloibuka ndani yako lina kupa NGUVU. Hii “nguvu” ya kuwa mtendaji wa Neno unaipata katika KUTAFAKARI, naam, ndipo unaweza kumpendeza Mungu na kufanikiwa katika njia zako ZOTE.

Kumbuka, Mungu huchunguza mioyo na viuno; kila Anapochungulia ndani yako, Anaona mawazo yako. Kama wewe ni mtu wa kutafakari Neno, unakuwa mtu wa kumpendeza Mungu muda wote kwa sababu moyo wako hauna muda na nafasi ya kutafakari mambo machafu. Ndipo utajua maana ya maombi ya Daudi aliposema, “mawazo za moyo wangu, na maneno ya kinywa changu yapate kibali mbele zako ee Bwana”.

Angalia jambo jingine. Imani huja kwa kusikia, na kusikia huja kwa Neno la Kristo (Warumi 10:17). Kuna tofauti kubwa kati ya mtu “anayesikia” Neno kwa masikio ya nje, kisha hilo Neno likaishia katika kumbukumbu zake kama kitu kilichohifadhiwa ghalani; na mtu ambaye anasikia Neno kwa masikio ya nje, LAKINI anaendelea kulisika lile Neno ndani yake (akitafakari) usiku na mchana. Japo wote wawili wamesikia Neno lile lile, imani za hawa watu ni tofauti; pia NGUVU ya kupambana na dhambi au hali fulani za kimaisha ni tofauti pia. Kama Neno linakaa tofauti ndani ya watu (kwa kutafakariwa au kutotafakariwa), basi tarajia na KUFANIKIWA kwa hawa watu ni tofauti pia, kwa sababu kwa kupitia Neno lile lile hawa watu wawili wamepokea NGUVU tofauti.

Daudi aliposema “moyoni mwangu nimeliweka Neno lako, nisije nikakutenda dhambi” alimaanisha kitu zaidi ya kukumbuka mistari ya biblia. Kuna uhusiano wa “mawazo” na “nafsi/moyo”, kisha “matendo” yako. Kutafakari kunatokea kwenye moyo/nafsi. Unapotafakari Neno, lile Neno linakuwa na nguvu maishani mwako nawe unakuwa mshindi dhidi ya dhambi, na kukewezesha kuishi maisha ya utauwa. Kumbuka siku zote, Neno lililopo akilini mwako halina tofauti na “mbegu iliyoko ghalani”; usitarajie itaota na kuzaa; Bali Neno linalotafakariwa moyoni mwako ni kama “mbegu iliyoko shambani”, tarajia itaota na kuzaa matunda maishani mwako.

Frank Philip.

Comments