NI AFADHALI KUPATA MATESO NA WATU WA MUNGU,KULIKO KUJIFURAHISHA KATIKA DHAMBI.

Na mtumishi wa MUNGU Gasper Madumla
Tutafakari kwa ufupi siku ya leo juu ya jambo hili maana imeandikwa;
" Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;
akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;
akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo. " Waebrania 11:24-26

Bwana Yesu asifiwe sana...
Biblia inatuambia;kwa IMANI Musa alikataa kuitwa mtoto wa binti farao.
Sikia;
Pasipo imani Musa asingekubali kuacha vitu vyote vilivyopo kwa farao,sababu ndani ya nyumba ya Farao kulikuwa kuna kila kitu cha kupendeza mwili,mfano palikuwa na chakula N.K sasa si rahisi kuacha vitu vitamu vitamu vipendezavyo mwili na kukimbia katika eneo hilo pasipo IMANI.

Kumbe,imani kwa Kristo Yesu ndio dira yetu,pasipo hiyo hakuna ukristo.Imani hutusukuma kuteswa pamoja na Kristo,tena na kukataa kujifurahisha katika dhambi.
Imani inaweza kukusukuma kuacha mambo yanayoonekana ni mazuri kwa mwili wako,ili kumpata Yesu.

Musa ndani ya nyumba ya farao ni kama wewe ukae ndani ya Ikulu ya nchi yako. Yaani ni sawa na wewe uwe mtoto wa raisi wa nchi yako. Kwamba kila kitu kipo ndani,sababu ndani ya ikulu hakuna shida ya ukame wa chakula,wala hakuna ukame wa mavazi mazuri, wala hakuna ukame wa pesa,ndani ya maisha ya ikulu hakuna kuangaika kutafuta mahospitali pindi uuguapo;
Mfano watu wa nje ya ikulu wakiugua,wewe unaweza kuwatazama jinsi waangaikavyo huko hospitalini Muhimbili,ila wewe aha! Watibiwa nje huko Ulaya katika mahospitali makubwa.
Sasa kwa mambo yote kama hayo,Musa akayakataa kuyapata,sababu alijua akiendelea kuyashikilia atamkosa Mungu wake na atakuwa kama ajifuraishaye katika dhambi.Jambo hili si rahisi kulifanya pasipo IMANI,kwa sababu Musa alipoondoka kwa Farao,ni sawa na kuacha vitu vitamu vitamu na kukimbila katika mateso,jambo hili ni gumu pasipo imani,unajua hakuna mtu apendaye kupata shida.
Biblia imeanza kutuambia kwamba kwa Imani Musa ilipokuwa mtu mzima akakataa kuitwa mtoto wa binti farao...
Sasa unisikilize kwa makini mpendwa;
Ilihitajika Musa awe mtu mzima ili ayajue maovu yaliyopo ndani ya nyumba ya farao. Kuwa mtu mzima ni kuanza kuelewa kweli ya neno la Mungu liletalo imani. Huwezi kujua haki yako ungali u mtoto,ni lazima uwe mtu mzima.

Musa alipokuwa mtu mzima alijua haki yake ipo wapi. Haki ya Musa haikuwa ndani ya nyumba ya farao,bali haki yake ilikuwa kwa ndugu zake waliokuwa wakiteswa huko utumwani. Musa alipoijua kweli,kweli ikamweka huru ( Yoh.8:32 ) Kweli ikamsukuma kutoka kwa farao pasipo kuangalia mali na utajiri uliokuwepo kwa farao.
Leo hii;
Ukitaka kupata mpenyo katika maisha yako kwanza upate ufahamu juu ya tatizo yaani uwe mtu mzima, kisha utoke mahali hapo penye tatizo yaani mahali ambapo penye raha za mwili,ambazo si raha za kufurahisha roho yako. Nasema ni lazima kutoka mahali hapo ambapo hakuna ukuaji wa roho yako,ndiposa ukitoka hapo utairihusu roho yako ikuwe na kusikia nini Mungu akuambiacho.

Ngoja labda nikuulize swali hili,kisha nitajijibu mimi mwenyewe.
* Hivi,unafikiri kwamba Musa alipokuwa mtu mzima kwa nini asingelibakia kwa farao,labda aseme kwamba azidi kumuomba Mungu ili Mungu aziondoe dhambi zilizopo kwa farao ili aendelee kula vinono?
JIBU:
Musa hakuhitajika kuomba kufutwa kwa dhambi za farao,bali alihitajika kuondoka kwa farao. Usalama wa kuacha dhambi ni kuondoka kutoka katika dhambi.
•Hakuna njia nyingine ya kuacha dhambi isipokuwa kuondoka katika dhambi.

Leo,watu wengi wemengangania kubaki mahali ambapo hapana usalama wa roho zao,mahali penye kuifurahisha miili kwa kitambo tu,mtu aweza kubaki akiufurahisha mwili wake hata katika kanisa lisilokuwa la kiroho,au labda hata kungangania dhehebu lake na kushindwa kumpokea Bwana Yesu,Yeye Mungu asiyekuwa na dhehebu lolote.
• Ni bora kuunyima mwili starehe zote zenye kukufanya umkose Mungu kwa kukimbilia haki.
Maana hata biblia inatuambia;
Kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili,twataka kufa ( Warumi 8 : 13 )
Yatupasa kuyafisha matendo ya mwili kwa Roho ili tuishi.

Musa alipokuwa mtu mzima akakataa kuishi kwa kuyafuata mambo ya mwili,bali aliyafisha yote Roho wa Mungu Baba ndio maana aliweza kutoka kwa Farao. Ndiposa akaona ni afadhali kupata mateso na watu wa Mungu.
Hivyo,
• Hata sisi hatutakiwi kubakia mahali penye kuifurahisha miili yetu kwa dhambi,bali yatupasa kuikimbia dhambi kama Musa alivyofanya,na hapo ndipo itakuwa salama yetu.

Ooh,
Kumbe!
Kulikuwa na watu wa Mungu waliokuwa wakipata mateso. Nimelipenda neno hilo " akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko" Waebrania 11:25

Sasa swali la kujiuliza;
Kama kulikuwa na watu wa Mungu waliokuwa nje ya farao ( ndugu zake Musa),Je watu wa farao na farao mwenyewe ni watu wa shetani?

JIBU;
Watu wote ni watu wa Mungu.
Mungu wetu hutupenda sisi sote,wema na wabaya hupokea pendo la Mungu.
Lakini si watu wote ni wana wa Mungu.
Wana wa Mungu ni wale wanaoishi sawa sawa na mapenzi yake Mungu,kwanza wamezaliwa upya kwa Roho mtakatifu,wameokoka lakini pia na kuishi kwa kuyafanya mapenzi ya Baba wa mbinguni. Hata wakati wa Musa hali ni vivyo hivyo.

Imefika wakati sasa wa kukubali kuteswa pamoja na Kristo kwa kuyafanya mapenzi yake Mungu wetu,kuliko kubakia kujifurahisha katika dhambi kwa muda tu.
Maana tukiwa upande wake Mungu,tu kinyume na dunia,na hapo tutaanza kuchukiwa na ulimwengu,lakini tu rafiki wa Mungu.

• Kwa huduma ya maombi na maombezi;nipigie namba hii 0655 111149
UBARIKIWE.

Comments