TENGENEZA UHUSIANO WAKO NA MUNGU

Na Frank Philip


"Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa" (Matendo 19:13-16).

Pamoja na kwamba Jina la Yesu ndio lina tenda KAZI, kuna tofauti kati ya mtu na mtu wakati wakilitumia hilo Jina. Hebu fikiri unakutana na adui yako, halafu unamsihi "atoke" huku unamwogopa, badala ya "kumwamuru" kwa MAMLAKA na UJASIRI, Je! atatoka kiurahisi ilihali ni vita? Je! BWANA hakutufundisha kwamba "tukiuamuru mti/mlima ung'oke......itatokea ILA tusipkuwa na shaka"? Sasa basi, pamoja na kwamba Jina la Yesu ndio linafungua watu, IMETUPASA kujifunza JINSI ya kulitumia kwa usahihi ILI kupata matokeo mazuri zaidi.

Jambo jingine nililojifunza kuhusu Jina la Yesu ni UHUSIANO wako binafsi wewe na Yesu. Huwezi kusimama na kushinda vita yako kwa kutumia uhusiano wa mtu mwingine na Yesu, ila uhusiano wako binafsi na Yesu. Wana wa Skewa walijaribu kutumia uhusiano wa Paulo na Yesu, kukemea pepo wakapata shida (Mdo. 19).

Tengeneza uhusiano wako na Yesu, pata IMANI lakini pia UJASIRI ili uone matokeo mazuri utumiapo Jina la Yesu. IMANI ni muhimu, lakini nakwambia leo, UHUSIANO wako na Yesu ukiwa mzuri utapata UJASIRI wa kusimama na kuamuru mambo yakatokea kama ulivyosema, kwa Jina la Yesu.

Angalia mfano huu, hebu fikiri wewe ni mtoto wa Rais, na kuna jamaa mwingine ambaye hawajuani kabisa na Rais (hawana uhusiano binafsi); halafu hawa watu wawili wanakwenda pale Ikulu, wakitaka kumwona Rais wa nchi. Kumbuka wote wawili hawana appointment ya kumwona rais, ILA wakifika mlangoni, mtoto wa Rais atakuwa na UJASIRI wa juu sana kwa sababu Rais ni baba yake (uhusiano binafsi); walinzi watampisha mlangoni; ila huyu wa pili atajitahidi kujieleza ZAIDI kwa walinzi pale mlangoni, kwa mfano, atasema "mimi nilisoma na mtoto wa Rais", na walinzi watashindwa kumwelewa kwa sababu anatumia "uhusiano wake na mtoto wa Rais (mtumishi mwingine)" WALA sio "uhusiano wake binafsi na Rais", na walinzi wanaweza kumsumbua tu. Hili lilikuwa KOSA la wana wa Skewa.

Mambo machache yanaweza kukusaidia kuongeza ujasiri wako kwa Bwana Yesu:
1. Kaa mbali na dhambi
2. Jifunze Neno ili umjue Mungu wako na NGUVU zake
3. Fanyia imani yako mazoezi, yaani kuwa mtendaji wa Neno. Chukua muda wa kuzungumza na Yesu (kuomba) mara kwa mara, eleza mambo yako na jenga UHUSIANO wenu, kisha TENDA KILA jambo ambalo unadhani litamfurahisha.

Frank Philip.

Comments