TUNDU BOVU

Na Frank Philip


“Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji” (Waebrania 4: 14-16).

Nimesikia habari ya watu ambao wanadhani majaribu yanachagua watu; hawa kuwaogopa na wale kuwajaribu. Mtu yeyote anajaribiwa katika jambo LOLOTE na hakuna cha ajabu hapo. Wengine kwa UJINGA wao, huku wakijidhani ni wenye HEKIMA na NGUVU, wamesema “nitakwenda, ila sitafanya”, lo! Tazama, wameanguka kama kuku wa kitoweo, bila kujitetea.

Nimesikia watu wenye hekima walisema “ndege mjanja hunaswa na tundu bovu”, nami nikaona hakika hapo kuna hekima, tena nikatazama nikaona maonyo ya kufaa kwa wana wa Mungu pia. Ukisikia mtu ameanguka MAJARIBUNI, na kutenda dhambi, angalia tena, utagundua ni katika yale mambo ambayo huyo mtu aliyadharau na kuacha kuchukua hatua za MAKINI za kujiepusha, huku akijidhania ni ndege mjanja, akanasa katika “tundu bovu”; ikafuatia aibu na majuto. Ndio maana tunaonywa kwamba “anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke” (1 Kor. 10:12).

Kama BWANA alijaribiwa KATIKA mambo YOTE, je! wewe na mimi ni nani hata tuheshimiwe sana na Ibilisi na kutujaribu kwa staha? Je! hatukusikia habari za watu wakuu sana, wenye heshima sana, wenye nafasi za juu sana, wemefanya UPUMBAVU katikati ya wana wa Mungu na Ulimwengu unawashangaa? Kama hao wametenda hayo, je! unadhani ni wajinga? La! hasha. Hao ni wajuzi wa ile Kweli, ila hawakujua SAA YA KUJARIBIWA KWAO, wakaanguka katika “tundu bovu”, na sasa fedheha imewakuta; vyombo vya habari vimepambwa kwa majina yao.

Kumbuka siku zote, “pasipo chambo hakuna kitoweo”. Ni mvuvi asiye na akili ataenda kuvua samaki kwa ndoano isiyo na chambo. Kila samaki aliyenasa kwenye ndoano, alifuata chambo akitafuta “mahitaji ya chakula”, kumbe! Kuna mtego hapo. Naam, hata sasa, wengi wamenasa kwenye ndoano za Ibilisi, na bado wako hapo japo wanajiita wana wa Mungu, kumbe walisahu kwamba imetupasa “kukaribia kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji”, kwa sababu hapo kwenye UHITAJI wako, ndipo kulipo na JARIBU lako.

Tukijua kwamba hatushindi kwa nguvu zetu wenyewe, basi na tumkimbilie Mwamba wa wokovu na tumaini letu, Yesu Kristo, Bwana wetu, ambaye “alijaribiwa KATIKA mambo yote na HAKUTENDA dhambi”, ili tupate Neema ya kushinda na kisha kusimama wakati wa kujaribiwa kwetu, tukiisha kujua nyakati na yatupasayo kutenda kwa kila wakati na nyakati.

Bwana humrehemu yeye amtafutaye, na amtafutaye kwa BIDII atamwona.

Frank Philip.

Comments