USIKUBALI KUFA KIMYA KIMYA,PAZA SAUTI YAKO KWA BWANA,UOKOLEWE.

Na mtumishi wa MUNGU Gasper Madumla
" Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.
Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu.
Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.
Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?" Mathayo 14:28-31

Bwana Yesu asifiwe...
Nakusalimu mpendwa katika Kristo Yesu,na karibu katika fundisho hili zuri usomalo mahali hapa ambapo pamefanyika baraka kwa watu wengi,watu walio ndani ya Tanzania hata wale walio nje ya nchi ya Tanzania maana kupitia mahali hapa nimepata simu za watu wengi,na wengine wameokoka kwa kufuatilia mafundisho haya nikupayo,nami najua ya kwamba siku ya leo ni siku yako ya kumgeukia Mungu kwa moyo mmoja,kwa kuziacha dhambi zako,kisha Bwana awe mwokozi wa maisha yako,ukaokoke.

Katika maandiko hayo hapo juu tuliyoyasoma,tunaona kwanza
Ingawa Petro aliona shaka hata kuzama ,lakini alikuwa na kiwango kikubwa cha imani kwa sababu aliweza kupiga hatua kadhaa kwenye maji. Biblia haikutuambia ni hatua ngapi ambazo Petro alizopiga juu ya maji. Zipo baadhi ya hatua alizozipiga juu ya maji ndipo baadae alipoona shaka akaanza kuzama. Hivyo Petro alikuwa na imani kubwa sana ingawa aliona shaka.

Kutembea juu ya maji si mchezo!
Ukitaka kuamini kwamba kutembea juu ya maji ni kiwango kikubwa cha imani,basi nenda kajaribu wewe.
Ngoja nikupe zoezi la kufanya siku ya leo,ili kuhakikisha hiki ninachokuambia kwamba kutembea juu ya maji ni kiwango kikubwa.

Zoezi lenyewe ndio hili:
MAHITAJI YA ZOEZI.
01. Mtumbwi.
02.Bahari

Hakikisha unakuwa ndani ya mtumbwi na pia uhakikishe huo mtumbwi upo baharini,mfano bahari ya hindi hivi. Alafu kwa kiwango chako cha imani utoke katika mtumbwi na ujitupe baharini uanze kutembea juu ya maji ya bahari. Ukishajitupa juu ya maji kwa lengo la kutembea,hapo ndipo utajipima imani yako,kwamba utatembea juu ya maji au la!
Bwana Yesu asifiwe...
Biblia inasema Petro alipoanza kuzama alipaza sauti yake,akapiga yowe, akisema, " Bwana, niokoe. " ndiposa Bwana Yesu akamuokoa,ndio maana neno la Mungu kupitia kitabu cha Warumi linasema;
" kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. " Warumi 10:13.
Bwana Yesu pia alikuwa akimfundisha Petro pamoja nasi neno lilo hilo,kwamba yatupasa kuliitia jina la Bwana ili tuokolewe. Tazama kwa habari ya Petro,Bwana Yesu si kana kwamba alikuwa hamuoni Petro akizama,bali Bwana alimuhitaji Petro ampazie sauti ili amuokoe,maana yake kama uombi basi hakuna msaada.
Katika mazingira hayo,Patro aliokoka baada ya kuliitia jina la Bwana, " Bwana uniokoe " laiti kama asingeliitia jina la Bwana,angelikufa kimya kimya lakini Petro hakukubali afe kimya kimya. Uzima wa Petro ulikuwa ni kuliitia jina la Bwana.
Alikadhalika uzima wako leo ni kuliitia jina la Bwana. Nje ya macho ya Bwana hakuna kitakachofanyika kikafanikiwa.
Hivi,..
Ngoja nikuulize swali;
Tuwe wawazi kabisa siku ya leo,yaani tusifichane.
Unafikiri;
Petro asingelipaza sauti yake,je angepona na yale maji?

Kama jibu ni hapana asingepona,basi ndivyo hali ilivyo katika maisha yetu. Kama hatutapaza sauti kwa Bwana basi ni dhahili tutakufa kimya kimya huku tukiwa tunazama.
Leo hii,Petro anatufundisha fundisho kubwa sana mahali hapa kwamba;
Pasipo kuliitia jina la Bwana,twataka kufa kimya kimya. Mtunga Zaburi naye hutuambia hivi;

"Katika shida yangu nalimwita Bwana; Bwana akanijibu akaniweka panapo nafasi. " Zaburi 118:15
Yawezekana ipo shida kwako,
Yawezakana unaangamia kwa mateso ya magonjwa,
Yawezekana unazama katika dimbwi la shida kimya kimya.
Yawezekana unazama taratibu taratibu katika dimbwi la dhambi,
LAKINI LEO USIKUBALI UFE KIMYA KIMYA,LIITIE JINA LA BWANA,UOKOKE.

Sasa unisikilize sana;
Petro hakuweza kujiokoa yeye mwenyewe katika yale maji hata kama angefanyaje! Ilimbidi Bwana Yesu amuokoe.
Nami ninakuambia kwamba:
Hakuna mtu awezae kujisaidia mwenyewe pasipo kusaidiwa. Narudia tena;

•Hakuna awezae kujisaidia pasipo kusaidiwa.
• Hata kama U mjanja kiasi gani,Lakini bado unamuhitaji Bwana Yesu akuokoe.
Sasa;
Watu wengi hujidanganya kwa msemo huu; " jisadie ili Mungu akusaidie " msemo huu ni msemo wa kuzuka,usio na mantiki ya kimaandiko mahali popote pale . Mungu yupo wa kutusaidia,sisi wenyewe hatuna uwezo wa kujisaidia. Tunapokuwa na shida kimbilio letu ni Bwana.

Haleluya...
Watu wengi leo wamekubali kufa kimya kimya kwa magonjwa yao. Wakidhani kuwa Mungu anawaona hivyo magonjwa na mabalaa yataondolewa pasipo kupaza sauti kwa Bwana. Mimi nakutangazia kuwa ukinyamaza kimya pasipo kumpazia sauti Bwana;utakufa huku unajion mwenyewe. Sasa umefika wakati wa kupaza sauti kwake yeye Bwana illi atuokoe.
Bwana Yesu asifiwe...
Lakini pia kupitia maandiko hayo ( Mathayo 14:28-31) tunajifunza kwamba;
• Tunapomfuata Bwana Yesu hatutakiwi kuona shaka mioyoni mwetu,tukiona shaka kamwe hatuwezi kufikia lengo.
Tena ikiwa unamfuata Bwana Yesu huku una shaka moyoni mwako,basi ni afadhali sana usimame kwanza,kisha ukishaondoa shaka ndiposa umfuate.

Siku ya leo,kataa kufa kimya kimya shout to the Lord,omba msaada wa Bwana. Misingi ya dini yako isikufanye ufe kimya kimya,wala dhehebu lako lisikufanye ufe kimya kimya.
Wala hata wazazi wako wasikufanye ufe kimya kimya. Ikiwa umenielewa basi unipigie simu yangu hapo chini tuombe kwa pamoja katika tatizo au shida unayoipitia wewe au hata wazazi wako,au ndugu zako.
Piga;
0655-111149.

UBARIKIWE.

Comments