ITA UWEPO UKIWEPO

Na Frank Philip


“Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua” (Yeremiah 33:3).

KUITA na KUTUMA, ni maneno mawili ambayo yanatumika kueleza mahali (location), na pande mbili za watu/vitu vinavyowasiliana. Kwa mfano, mtu akisema KUITA inamaana ANAYEITWA aje kumfuata huyu aitaye; na KUTUMA ina maana MMOJA amemwagiza mwingine AENDE mahali tofauti na alipo.

Yeremiah 33:3 ni msitari maarufu sana vinywani mwa wengi. Je! Umewahi kujiuliza ni watu wangapi WANAMWITA Mungu wakati wao wenyewe hawapo? Yaani utasikia mtu anamwambia Mungu “shuka Bwana ukashughuluke na adui zangu au na hali fulani”, sawa, Bwana anashuka, ila akija anakuta HAUPO! Sasa usisahau kwamba “Mungu anatenda kazi pamoja na wanadamu ili kuwapatia mema”, Anapokuja kufanya kazi na wewe, Anakuta HAUPO! Uko busy na Ibilisi katika miradi yake ya kumuudhi Mungu. Kwa lugha nyingine, badala ya KUMWITA inakuwa kama UMEMTUMA Mungu akashughulike huko, huku wewe uko MAHALI pengine (ulimwinguni), yaani nje ya KUSUDI la Mungu.

Ukitaka kujifunza kwa mfano rahisi, fikiri mtu hamtaki Yesu, lakini anataka UPONYAJI au anataka Yesu ampiganie katika mambo yake ya kila siku! Mtu anataka USHINDI, ila hajampokea huyo MSHINDAJI! Sasa unaweza ukafikiri nazungumza na watu ambao hawamjui Mungu; hapana! Nazungumza na watu ambao wanamjua Mungu, ila wameamua kuishi maisha ambayo WANAJUA sio MPANGO wa Mungu, sasa wanakutana na mambo magumu huko njiani, Ghafla! Wanaanza kusimama na Yeremia 33:3, huku bado HAWAJATUBU (kugeuka na kuacha njia zao mbaya!), WANAITA UWEPO WA MUNGU, WAKATI WAO WENYEWE HAWAPO! Hii huwa haifai.

Angalia usiwe kama Akani mwana wa Karmi, aliyeiba vitu vilivyowekwa wakfu, na kuvificha hemani mwake; kisha akadhani Mungu ataendelea kumpigania tu kama zamani! Ghafla tu, mambo yakabadilika, hapo nyuma mambo yalikuwa marahisi walipokuwa katika kusudi la BWANA, sasa mambo yamekuwa Magumu ghafla tu, Israel wamepigwa na Ai kaliko kataifa kadogo tu; ndipo Joshua mwana wa Nuni alipoutafuta uso wa Mungu; BWANA akasema “mimi sitakuwa pamoja nanyi tena, msipokiharibu kitu kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu” (Yoshua 7:10). Wana wa Israel walijaribu kupambana wakati UWEPO umeondoka, Kumbe! Kuna dhambi katikati yao. Angalia, imekupasa KUWEPO unapoita UWEPO wa Mungu.

Je! Waweza KUMTUMA BWANA akatende mambo yako wakati wewe mwenyewe haupo?

Frank Philip.

Comments