JIWE LA KUNOLEA

Na Frank Philip


“Akapanda chomboni, wanafunzi wake wakamfuata. Kukawa msukosuko mkuu baharini, hata chombo kikafunikizwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu” (Mathayo 8:23-26).

Huwezi kunoa upanga kwa kutumia mti au kitu laini tu; upanga hunolewa kwa kitu KIGUMU kama jiwe au chuma fulani maalumu.

Maisha ya watu wengi yamekuwa na kitu KIGUMU na cha kusumbua sana. Vitu vya namna hii tunaviita kwa jina moja “changamoto”, na hapa mimi naita “jiwe la kunolea”. Kuna tofauti ya jiwe na jiwe, ila nakuhakikishia kwamba katika maisha yako LAZIMA kutakuwa na mawe KADHAA ya kunolea, ambayo yatajitokeza katika misimu mbalimbali. Wewe kama upanga, makali yako yanahitaji jiwe la kukunoa ili uweze kuwa na makali. Kumbuka, ubora wa upanga upo katika makali yake. Ukiona mtu hapendi changamoto, jua huyo hapendi kunolewa, na pia hawezi kuwa mtu wa maana sana katika jamii.

Nimekutana na mama mmoja, akaniambia, “NDOA yangu ina changamoto, ILA nimegundua Mungu ananiandaa kwa HUDUMA ya wamama”. Kumbuka, huyu mama hakunieleza changamoto zake, na mateso anayopitia katika ndoa yake, wala KUMLAUMU mumewe kwa kuwa kitu KIGUMU (jiwe); yeye haoni kitu kigumu, anaona KINOLEO. Huu mtazamo wa huyu mama ulinifanya nijifunze jambo jipya.

Hebu fikiri ni watu wangapi wanapiga kelele juu ya waume/wake zao, mabosi wao kazini, jamaa wanaowasumbua mtaani, majaribu ya kwenye biashara zao, majaribu katika shule zao, nk. Hawaoni changamoto kama JIWE la KUNOLEA! Wengi wao wametafuta njia mbadala (za kibinadamu) za KUKWEPA jiwe, kumbe! hawajui kuna KUSUDI la Mungu katika kila jambo, hawana makali tena, wamekuwa upanga butu lisilo na makali kabisa, na sasa, majaribu kidogo tu wanakwenda kama bendera fuata upepo, wanaanguka tu kama watu ambao hawajawahi kumjua BWANA, kumbe! wakati wa kunolewa hawakujua, wamekuwa dhaifu wa imani.

Jifunze kusimama kwa imani (kutumia Neno ulilofundishwa/jifunza) kupambana na mazingira na changamoto zako, kwa maana hizo huja KUKUNOA ili uwe chombo kizuri zaidi. Angalia, katika dhoruba na changamoto za maisha, wengi wamemtenda Mungu dhambi, kwa sababu wamekuwa walegevu katika KUMTII Mungu wao, na hawakuwa na BIDII kusikiliza sauti yake, na KUTAFUTA kutenda mapenzi Yake.

Frank Philip.

Comments