KUJITENGA NA MUUNGANIKO WA MADHABAHU YA KIPEPO.

Na mtumishi wa MUNGU Gasper Madumla

Chakula cha leo ni chakula kigumu,lakini kinakufaa kabisa,haya tuanze kula kwa pamoja maana Imeandikwa ;
" Na katika habari za kuzaliwa kwako, siku ile uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuoshwa kwa maji usafishwe; hukutiwa chumvi hata kidogo, wala hukutiwa katika nguo kabisa.
Hapana jicho lililokuhurumia, ili kukutendea lo lote la mambo hayo kwa kukuhurumia; lakini ulitupwa nje uwandani, kwa kuwa nafsi yako ilichukiwa,
katika siku ile uliyozaliwa.
Nami nilipopita karibu nawe, nikakuona ukigaagaa katika damu yako, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai; naam, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai. " Ezekieli 16:4-6

Bwana Yesu asifiwe...
Siku ya leo ni siku ya kufanya maombi mimi na wewe ndugu msomaji wangu haswa wewe unayesoma fundisho hili. Najua umekwishawahi kujifunza mafundisho mengi sana kwa nyakati tofauti tofauti,na kwa kupitia watumishi tofauti tofauti lakini nakuambia kupitia fundisho hili;tutafanya maombi ya kina,kisha maombi hayo yatakupeleka katika kiwango cha juu cha maisha yako.
Maandiko hayo hapo juu tuliyoyasoma hivi sasa ( Ezekieli 16:4-6 ) yanatupa mafundisho mengi mno,lakini siku ya leo tunakwenda kujifunza kwa ufupi juu ya kujitenga na nguvu za madhabahu ya kipepo yaliyotoka kwa wazazi wako kupitia muunganiko wa kitovu chako.
Si mara nyingi hukute fundisho hili likifundishwa,sababu kwanza haliwapendezi wengi,tena ni fundisho gumu kueleweka,lakini naomba unielewe kwa uweza wa jina la Yesu Kristo.
Imefika wakati sasa wa kuyafahamu mambo haya kiundani,na kuyafanyia kazi pia. Wakati wa kujitenga na kila aina ya madhabahu ya kipepo ndio sasa.
Biblia inasema " Na katika habari za kuzaliwa kwako, siku ile uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa,..." Ezekieli 16:4
Hii ina maana kwamba wakati wa kuzaliwa kwako,kulikuwa na muunganiko wa tabia na mambo yatokayo kwa mama yako,na hata baba yako pia.

Kitovu kutokatwa...
Ni ishara ya kuwepo mambo endelevu yatokayo kwa wazazi wako. Lakini mambo haya tunayaangalia kama mambo ya kimadhabahu au kama mambo yenye kukudai hatma ya maisha yako kwa ujumla.

Haleluya...
Mimi sio mwana baiolojia kuhusu mfumo wa uzazi,ila kile kidogo ninachokifahamu mimi ni hiki;
Mtoto mdogo awapo tumboni,huungana na mama yake kwa njia ya mlija/ utumbo. Kupitia utumbo/mlija huo,mtoto aweza kupokea chukula, utumbo/mlija huu ulioungamana katika sehemu ya kitovu chake mtoto. Kwa lugha nyingine ni kwamba,mama akiwa anakula,ndicho mtoto naye hula kupitia kitovu chake.

Sasa;
Ikiwa kitovu cha mtoto hakikukatwa,hii ina maana kwamba mtoto bado ameungamana na mama.

Kitika ulimwengu wa kiroho,vipo vitovu vilivyokatwa na vipo vitovu visivyokatwa.
Vitovu vilivyokatwa ni kutokuwa na muunganiko wowote ule kwako wewe na madhabahu ya miungu ya baba zako na mama zako.
Vitovu visivyokatwa ni kuwa na miunganiko ya madhabahu ya miungu ya kwenu.

Hakuna kitu kinachofuatilia kizazi hadi kizazi kama madhabahu. Madhabahu yoyote ile,iwe ya ki-Mungu au ya kipepo,kazi yake ni kufuatilia au kutembea katika kizazi kimoja hadi kingine.Mfano mzuri mtizame Ibrahimu, madhabahu aliyokuwa akimfanyia Mungu ndio ilitembea kwa kizazi chake,Ibrahimu alipomzaa Isaaka,Isaaka naye alijikuta akimuabudu Mungu huyo huyo Mungu wa kweli,Mungu wa Ibrahimu babake,alikadhalika Isaaka alipomzaa Yakobo,mambo yakawa ni vile vile.
Biblia inaposema ;
" Na katika habari za kuzaliwa kwako, siku ile uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa,..." ina maana kwako wewe bado ulikuwa na muunganiko wa kiroho na mama yako. Sasa ikiwa mama yako alikuwa akiabudu miungu mingine,basi ujue automatically na wewe unahusika katika miungu hiyo.

Yale aliyokuwa akiyafanya baba na mama yako,ndio hayo hayo wewe utafanya,hata kama kuna laana za wazazi basi ujue zinapita,sababu ya kuwepo na muunganiko huo.
Tazama hilo andiko hapo juu,Biblia inaanza kwa kukupa habari kwamba," Asili yako na kuzaliwa kwako kwatoka katika nchi ya Mkanaani; Mwamori alikuwa baba yako, na mama yako alikuwa Mhiti. " ( Ezekieli 16:3 ).

Biblia inakuambia kwamba wazazi wako walikuwa ni waabudu miungu,watu wenye madhabahu za kipepo. Sasa si rahisi kujitenga na madhabahu hizo kama ujapata ufahamu huu. Maana unaweza ukawa umeshaongozwa sala ya toba,lakini bado pakawa na mambo yanayokufuatilia. Yakupasa ufanye jambo la ziada.
Ndugu,nisemapo ya kwamba kitovu chako hakijakatwa nina maana kwamba upo muunganiko wa madhabahu ya kipepo baina yako wewe na mababa zako wa awali.
Unisikilize;
Wapo watu walipozaliwa tu,kitovu chao kilikatwa na kupelekwa katika matambiko. Wengine walipokuwa wamezaliwa,vitovu vyao vilipelekwa vijijini katika mizimu ya ukoo ya kwao.

Sasa mambo kama haya ndio " kitovu chako hakijakatwa " maana yake bado umeungamanishwa na mizimu kama hujasimama imara katika maisha ya wokovu,ujue utaendelea kuwa chini ya madhabahu ya kipepo ingawa unakwendaga kanisani jumapili kwa jumapili. Suala sio kwenda kanisani jumapili hadi jumapili,suala ni KUOKOKA kisha na kufanyiwa maombi lasmi ya kukata kitovu cha madhabahu ya kipepo.
Bwana Yesu asifiwe...
Wapo watu ambao nafsi zao zilichukuliwa wakati walipozaliwa. Maana imeandikwa;
" Hapana jicho lililokuhurumia, ili kukutendea lo lote la mambo hayo kwa kukuhurumia; lakini ulitupwa nje uwandani, kwa kuwa nafsi yako ilichukiwa, katika siku ile uliyozaliwa. " Ezekieli 16:5
Waweza kujiuliza kwamba;
*Sasa nitajuaje kwamba nafsi yangu ilichukuliwa?
Au
*Nitajuaje kwa habari ya kitovu changu?

Hayo ni maswali muhimu sana.
JIBU:
Ukiona kuna upinzani mkubwa katika yote uyafanyayo haswa mambo ya ki-Mungu. Mfano;Pale utakapo kumuabudu Mungu wa kweli,lakini unakuta upinzani mkubwa sana basi ujue ipo vita juu ya nafsi yako.
Au
Ukiona majanga yanayokufuatilia miaka hadi miaka. Mfano yawezekana ikawa ni magonjwa,au laana,au mikosi fulani. N.K
Na mambo kama hayo.

Ok,
Sikia hii kidogo;
Yesu Kristo alipozaliwa,mama jusi waliweza kuifuatilia nyota. Na walipomfikia walijua ya kuwa ni mfalme,sasa swali;
Walijuaje ya kuwa Yesu ni mfalme hali ni mtoto mdogo,na wao hata hawakuambiwa?( Mathayo 2:7-12)

Hapo ndiposa utajua ya kwamba shetani anaweza jua nyota yako yaani mafanikio yako yajayo. Ikiwa kitovu chako kitapelekwa kwa miungu katika madhabahu zao,wao pia wanao uwezo kuijua nyota yako/ mafanikio yako ingawa wewe mwenyewe hujijui kipindi hicho.
Namna ya kujitenga na madhabahu ya kipepo ni KUOKOKA kisha kuombewa maombi ya kukata kitovu.
Yote haya yanawezekana tena nimekueleza habari hiyo kwa ufupi sana,tena sana.
Yote yanawezekana kwa Bwana Yesu,ikiwa unaamini hayo na ikiwa kama umenielewa nipigie kwa namba yangu iliyopo chini hapo,nikueleze sana na maombi pia.
Piga;
0655-111149.

UBARIKIWE.

Comments

Unknown said…
Ahsznte mtumish na Mungu akubariki na uzid kutupa maarifa na ujuzi zaid