KUKOSA TUMAINI LA MAISHA YAKO NI UGONJWA MBAYA SANA

Na Mwinjilisti John Chinyuli

Kukosa tumaini na mwelekeo wa maisha yako ni mbaya kuliko hali iliyosababisha ukakosa matumaini. Unapochagua kuishi maisha ya kukata tamaa huwezi kupata suluhisho la mahitaji yako, hali hiyo inaendelea kuathiri maisha yako, ndoa yako, afya, biashara yako n.k, matokeo yake hali inazidi kuwa mbaya na kusababisha matatizo mengine kuibuka. Wengi hufikia hatua ya kujiua, kuwa na tabia sugu, kujikataa n.k. Leo ninayo habari njema kwa anayepitia hali kama hii kwamba unaweza kuishi kwa matumaini na ukawa mwenye furaha tena. Zaburi 51:8 “Unifanye kusikia furaha na shangwe, mifupa uliyoiponda ifurahi”
Mwamini Mungu, usifikirie sana kuhusu matatizo yako maana hakuna anayeweza kukusaidia kuliko Mungu, yaone matatizo yako ni madogo sana kwa Mungu yeye ndiye anayeweza kukusaidia, mtwike yeye mzigo wako atakusadia. Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo. Nami nitawapumzisha”
Muombe Mungu. Uombapo usifikirie Mungu atajibu vipi au usiwaze njia gani atatumia kukujibu, njia za Mungu hazichunguziki, atajibu kwa jinsi usivyoweza kudhania, yeye anatengeneza njia pasipokua na njia, atakutengenezea njia yako. Maana ukijua Mungu atajibu vipi, utajisifu umetumia nguvu na akili zako, Abraham kama mwanadamu alitumia akili zake kumpata Ishmail japo aliamini lakini hakujua ni kwa jinsi gani Mungu angempatia mtoto. Lakini katika uzee wake akampata Isack kwa jinsi ambavyo kwa akili ya mwanadamu haikuweza kufikiri.…Lakini hatimaye akampata Isaka, usiwazie njia za mkato, msubiri Mungu!
Omba kwa kunena kwa Lugha, Jizoeze kuomba kwa Roho! Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba kwa jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombeakwa kuugua kusikoweza kutamkwa” Unapoomba kwa Roho, hukusaidia kutamka majibu yako, hutamka ni kwa jinsi gani maombi yako yatajibiwa, unapoomba kwa Roho anakutia nguvu, bubujiko na hatimaye unaona raha moyoni mwako!
Anaachilia muujiza wako, hujenga imani yako, amani ya Kristo inakaa ndani yako, unakuwa mwenye furaha tena, mashaka yote yanaondoka. TUMAINI hujengeka ndani yako, japokuwa unapita kwenye magumu, ni kawaida kwa kila mtu sio wewe peke yako 1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lie jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili” ukiwa unasubiri muujiza wako. Mungu anakupa wepesi wa kupita hatimaye muujiza wako hutokea! Maana umevumilia na kuamini Mungu amefanya!
Ni maombi yangu umtumainie Mungu kwenye shida yako, ikiwa hujaokoka ungependa kumpokea Yesu awe Bwana na mwokozi wako sema sala hii fupi kwa kumaanisha;-
Bwana Yesu, mimi ni mwenye dhambi ninakuja kwako, naamini ulikufa na kuteswa kwa ajili ya dhambi zangu, naomba unisamehe sitarudia tena, unioshe kwa damu yako niwe safi, Naomba unisaidie kuishi maisha ya kukutumaini wewe, asante kwa kuyaokoa maisha yangu, naomba unipe na Roho wako Mtakatifu anisaidie, jina la Yesu ninaomba. Amen
 By Mwinjilisti John Chinyuli.
  0767 592989/0712 592989

Comments