MAFUNZO KWA VITENDO

Na Frank Philip


“Basi haya ndiyo mataifa ambao BWANA aliwaacha, ili awajaribu Israeli kwa hao, yaani, awajaribu hao wote ambao hawakuvijua vita vyote vya Kanaani; ili kwamba vizazi vya wana wa Israeli wapate kujua ili kuwafundisha vita, HASA wao ambao hawakujua vita kabla ya wakati ule; aliwaacha wakuu watano wa Wafilisti, na Wakanaani wote, na Wasidoni, na Wahivi waliokaa katika kilima cha Lebanoni, toka mlima wa Baal-hermoni mpaka kuingia Hamathi. Naye aliwaacha ili awajaribu Israeli kwa hao, apate kujua kwamba watasikiliza amri za BWANA, alizowaamuru baba zao, kwa mkono wa Musa” (Waamuzi 3:1-4).

Mara nyingi watu wamejifunza Neno la Mungu, na kusikia KUBARIKIWA sana, hata na kutoa sadaka kwa ajili ya kumshukuru mtumishi fulani aliyewahubiria. Neno la Mungu halifundishwi ili liwe kumbukumbu kama picha ya ukutani; Neno la Mungu huja kwako ili UTENDE sawa na hilo Neno; na sio kila mara utafundishwa kila kitu, ila kila jambo huja kwa majira na msimu fulani kwa kusudi fulani.

Mara nyingi sana, ukisikia fundisho limekujia kwa namna ya msisitizo usio wa kawaida, ukasikia kama Mungu amesema na wewe, jua haishii hapo; kuna mtihani utafuata. Sasa, mitihani inaweza ikatofautiana kwa uzito, kulingana na mtu, na kusudi la Mungu kwa mtu husika, ila KILA mtu atapitia mafundisho kwa NADHARIA na kwa VITENDO.

Wana wa Israel waliagizwa kuwafundisha na kuwasimulia wana wao, habari za MATENDO makuu ya Mungu. Kwa lugha nyingine, wana wa Israel walijua VITA ambazo wenzao walipigana, ila kwa nadharia tu; Mungu akaamua kujisazia “maadui” kidogo kati yao ili kuwafundisha vita “kwa VITENDO”, wale ambao hawakuwepo wakati wenzao wanabeba upanga kupigana vita. Lengo la Mungu kuacha maadui kati yao ilikuwa ili “WAJUE kupigana vita kwa vitendo”, na sio kwa KUSIKIA tu.

Mara nyingi sana watu hudhani kwamba mambo MAGUMU yanayokuja mbele yao ni Ibilisi tu. Hapana! Kuna mapito ambayo huja kwa MAKUSUDI ya kukufundisha VITA, ili UJUE uaminifua wa Mungu wako, ambaye jina lake ni MWOKOZI. Utakapomwona Mungu AKIKUOKOA katika mengi, ndipo utamjua ZAIDI kuliko ulivyosikia habari zake kwa wengine, kwenye mahubiri tu (kinadharia).

Paulo alijua habari ya KUMJUA Mungu kwa njia ya “kujifunza kwa vitendo”, ndipo akasema “ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu” (Wafilipi 3:10). Hii sio habari ya hadithi ya kinadharia, kwamba kuna “Roho wa Ufufuo, aliyemfufua Yesu”, au kwamba “yupo mtu aliyeitwa Yesu huko zamani”, Paulo anasema, hata saa, nataka NIMJUE yeye na UWEZA wa kufufuka kwake, hata na KUSHIRIKI mateso yake; akiutiisha mwili wake kukaza kutenda mapenzi ya BABA, haijalishi kama atapigwa mawe, kuchapwa viboko, kulala njaa, kutukanwa, nk. Anasema “nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu” (Wafilipi 3:14). Tena sio kukaza mwendo tu, Paulo anasema “kwa njia yoyote, huku akihesabu mambo yote aliyoyathamini kuwa kama mavi, kwa ajili ya uzuri ulipo katika Kristo”. Hii ni NIA ya dhati ya kusonga mbele, kwa vitendo.

Wakati BWANA alipokuwa duniani, akitembea huku na kule akifanya huduma. Wanafunzi wake waliona na kujifunza mengi, ila kwa NADHARIA tu. Hawakujua kwamba iko siku ya kufanya MAFUNZO kwa VITENDO; ndipo siku moja wakaagizwa kwenda kuhudumu peke yao; wakatoe pepo wachafu na kuwafungua watu (Mathayo 10:1-15). Bwana Yesu akabaki kusubiri ripoti baadae; Ndipo walipokuja na kushangilia jinsi pepo wachafu walivyowatii, na watu kufunguiwa. Hebu fikiri, wanafunzi wanamhadithia Yesu habari za pepo wachafu, na watu kufunguliwa, wakati Bwana alijua vyema kuliko wao! Hawakujua kwamba wako DARASANI kujifunza “kwa vitendo”, na Mwalimu alikua anangoja taarifa pale, Aone kama wameelea/wameweza. Kumbuka, walipofanya kwa VITENDO, hawakuwa kama walivyokuwa mwanzo, yaani kujua mambo kwa nadharia tu; walivuka hatua nyingine ya imani; yaani kwa kutenda wayajuayo.

Angalia jambo hili, BWANA anawaambia KUSUDI la wito wao mkuu, “msifurahi kwakuwa mapepo yanawatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni”. Angalia tena kitu Paulo anasema, “ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu”. LENGO sio kufanya huduma, kugaragaza watu chini, kushambulia mapepo, na kufungua watu, kisha kujikusanyia makundi huku na kule, lengo ni “kufikilia kiyama ya wafu/uzima wa milele”; Paulo akiisha KUMJUA Mungu na nguvu zake, kwa vitendo kabisa, mwishoni aweze kuingia mbinguni; Jina lake liwemo siku ile watakatifu wakiitwa kuurithi uzima wa milele! Je! Hili silo jambo ambalo BWANA aliwaambia wanafunzi waangalie zaidi? yaani kufurahi kwa sababu majina yao yameandikwa Mbinguni, na sio wagonjwa kufunguliwa, miujiza, na mapepo kuwatii.

Frank Philip.

Comments