MUNGU ANAPOMWACHA MTU APIGWE NA ADUI ZAKE

Na Frank Philip


“Wakamwacha BWANA, wakamtumikia Baali na Maashtorethi. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao. Kila walikokwenda mkono wa BWANA ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama BWANA alivyosema, na kama BWANA alivyowaapia; nao wakafadhaika sana. Kisha BWANA akawainua waamuzi, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara. Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za BWANA bali wao hawakufanya hivyo. Na wakati BWANA alipowainulia waamuzi, ndipo BWANA alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana BWANA alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua” (Waamuzi 2:13-18).

Maisha ya mkristo ni maisha ya ushindi; lakini ni maisha ya “ukristo” na sio jina tu la kikristo. Ili ufaidi ushindi, inaanza kwa “kuishi maisha ya mkristo” na sio maisha ya kipagani, huku unadai ushindi usiokustahili. Watu wengi wanadai “ushindi wa wana wa Mungu” (watu wanaoishi maisha ya Kristo), japo wanaishi kama wamataifa. Jina lako la kikristo sio kibali au sababu ya Mungu kukupigania, ila maisha yako ambayo ni matokeo ya uhusiano MZURI na Mungu.

Kusudi la Mungu kuja na kujidhihirisha kwa wana wa Israel kule Misri, ilikuwa ni Yeye Mungu kukaa katikati yao na kuwa Mungu wao. Sasa, Mungu ni mtakatifu; huwezi kumfukuza Mungu kwa kumkemea, ILA kwa kutenda mambo kinyume Naye. Kimsingi, kila niliposoma jinsi Mungu alipojiweka mbali na wana wa Israel, ni pale walipotenda machukizo, na sasa anajiweka mbali ili asiwaangamize kwa hasira! Je! Huu nao sio upendo na rehema tu za Mungu? Ndio maana tunasoma “ni kwa rehema tu za Mungu hatuangamii”. Sasa, kumbuka, Mungu kwa kuwarehemu hawa wana wa Israel, ilimpasa kukaa mbali nao kwa sababu ya dhambi zao, hapo ndipo maadui zao walipopata nguvu na kuwasumbua.

Sasa nisikilize vizuri. Mungu ni baba yetu, hata tukimkasirisha, bado ni baba yetu, na Yeye hutuhurumia hata katika hasira zake. Kumbuka siku zote, Mungu anapokasirika, hakuachi tu uangamie, ila atakufundisha UJUE kosa lako, ili utubu. Ukishupaza shingo, bado ataleta na mtu mwingine tena kukusaidia ujue makosa yako ili usiangamie; ukizidi kushupaza shingo sana, basi shingo huvunjika na hupati dawa. Sasa kumbuka, huyu sio Ibilisi anakushughulikia, ila ni Mungu; na Mungu akifanya jambo juu yako, je! Ni nani awezaye kukuokoa kutoka mikononi mwa Mungu aliye hai? Mungu akikuonya mara nyingi juu ya jambo, chukua tahadhari kwa maana shingo yako ikivunjika hakuna wa kukuokoa.

Nikisema nameno haya, imekupasa kujua, sio kila jambo ni la kukemea kwa sababu sio kila jambo BAYA linatoka kwa Ibilisi (Waamuzi 2:15); yapo mambo ambayo Mungu anaruhusu maishani mwetu, ili tupate kujua makosa yetu na kumgeukia Mungu kwa toba ya kweli. Sasa nakupa njia nyingine ya kupona katika majanga yako, sio kukemea pepo wa chafu tu, ila kumrudia Mungu, na Mungu atashughulika na adui zako kwa sababu hao adui zako hawakuja kwa sababu ni Ibilisi aliwaleta, bali kuna wakati mwingine huwa ni Mungu amewaruhusu. Ukiangalia huduma ya BWANA Yesu duniani, utaona kuna wakati ALISEMEHE tu mtu badala ya kukemea ugonjwa, na akasema “enenda zako, na usitende dhambi tena, yasije yakakukuta yaliyo mabaya zaidi” ghafla! Mtu anafunguliwa na kuwa mzima (Luka 5:20).

Uonapo wewe ni mkosaji sana, mchafu sana na asiyestahili kabisa, jua ni wakati muafaka wa kumrudia Mungu, maana Mungu anapendezwa na watu wamrudiapo hata kama dhambi zako ni nyekudu kama damu; Yeye huwasafisha, na utakuwa mweupe kama dheluji.

Mungu hufurahia tunapoishi maisha ya ushindi, lakini kumbuka, hutaishi maisha ya ushindi bila Mungu/mungu, jaribu uone [Mungu ni BWANA; na mungu ni miungu mingine, mfano nguvu za giza, uchawi, rushwa, nk.] Na ni mbaya ZAIDI kwa mtu anayemjua Mungu akirudi nyuma, ni aheri yule asiyemjua Mungu kabisa, (fuatlia somo lenye kichwa “TOFAUTI ya NEEMA na NEEMA” ). Kumbuka hatujaahidiwa kuishi maisha bila TUFANI, ila katika tufani hatuangamii. Tukiwa na BWANA tuko salama. Ole wake yule aliyegeuka na kumwacha BWANA, nani atamuokoa sikua ya tufani ipigapo au adui wazongapo?

Frank Philip.

Comments