TULIA KWA BWANA,WAKATI WAKO UKIFIKA MWENZI WAKO ATAKUJA MWENYEWE.

Na Mtumishi wa MUNGU Gasper Madumla
Bwana Yesu asifiwe...
Alipo Bwana yote yanawezekana,tena yanawezekana kwa viwango vya hali ya juu sana. Ndani ya utulivu kwa Bwana ndipo mahali ambapo kuna mafanikio yote.
Leo nataka nizungumze na binti na kijana mmoja asomaye ujumbe huu kuhusu mahusiano tu, jambo ambalo halizungumziwi sana na watumishi wa Mungu na hatimaye kusababisha waamini wengi wakijikuta wakitumbukia katika mahusiano ya kimapenzi pasipo tahadhari yoyote,na hata pasipo kujijua.
Kinachosababisha haya yote ni kwamba;
• Vijana wamekosa utulivu kwa Bwana
• Mahusiano hayazungumziwi vya kutosha huko makanisani.

Kanisa likishindwa kuzungumza kuhusu mahusiano ya kimapenzi kwa vijana wao wanaochipukia,husababisha vijana hao kwenda kujifunza nje ya kanisa kwa watu wa mataifa,ambapo huko ndio ni hatari na haifai kabisa maana wawapo kwa watu wa mataifa ni lazima watauacha upendo wa Kristo Yesu na kisha kujichafua miili yao kwa uzinzi na uesharati.
Ninafahamu fika kiu iliyopo kwa vijina wa kike na wa kiume wa siku ya leo;kiu yao kubwa ni kuoa au kuolewa. Hata mimi pia nilikuwa ninakiu hiyo hiyo kabla ya kuoa,hivyo ninafahamu mambo haya kiundani sana. Kila mmoja hupenda awe na familia yake binafsi,yaani kila mmoja hupenda siku moja aitwe baba fulani,au aitwe mama fulani.
Katika maombi;
Ninaamini ukiwakusanya mabinti wapatao ishirini pamoja na wavulana ishirini hivi.Kisha uwape karatasi nyeupe na peni iliyojaa wino,alafu uwatenge mbali mbali kama vile wanafanya mtihani wa taifa na uwaambie kila mmoja aandike jambo moja la msingi ambalo anahitaji Mungu amfanyie kwanza.
Utakuta nusu yao wanaweza wakaandika jambo la kwanza ni KUOA au KUOLEWA,maana ndio kitu kilichokamata mioyo yao.

Sasa kiu hii ya KUOA au KUOLEWA inapozidi kumtawala mtu,mtu hujikuta akimwacha Mungu wake hata kama alikuwa ameokoka tena na kusahau vyote alivyofanyiwa na Bwana Mungu wake,jinsi alivyotolewa huko Misri,mtu huyu akizidi kutawaliwa na mawazo ya kuoa au kuolewa mara nyingi huwa mtumwa wa dhambi ya uesharati.
Maana kila mwanaume atakaye kuja kwa gia ya KUOA basi ni ruksa kulala naye! kisa tu mwanaume kamwambia " nitakuoa" hii ni hatari sana.

Hata wanaume hudondoka katika dhambi hii mara nyingi sana kuliko unavyofikiria,eti kisa tu binti kamwambia kuwa " wewe ndio my husband " huku kabinti ako kakiwa kanaigiza sauti yake kwa kuibana!hii ni hatari sana. Ni roho ya uesharati na uzinzi,ISHINDWE KWA JINA LA YESU KRISTO.
Ikumbukwe;
Dhambi zote ziko sawa,yaani hakuna dhambi kubwa wala dhambi ndogo. Lakini matokeo ya kila dhambi hutofautiana sana. Yapo matokeo makubwa na yapo matokeo madogo kulingana na dhambi ya namna gani.

Mfano;
Matokeo ya dhambi ya wizi ni tofauti na matokeo ya dhambi ya uzinzi na uesharati. Hii ni kwa sababu dhambi ya uesharati ni dhambi inayohusisha AGANO wakati dhambi ya wizi inaweza isihusishe agano.Yaani yeye aziniye uungana na yule aliyezini naye. Ukizini na kahaba,umeungamana naye,nawe umekuwa mwili mmoja. Biblia inasema;

" Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. " 1 Wakorintho 6:16
• NDUGU,TULIA KWA BWANA.
Ukitaka kupata mwenzi bora aliyebeba hatma ya maisha yako,basi huna budi kutulia kwa Bwana. Kutulia kwa Bwana inamaana kuendelea kutumika kwa kazi ya Bwana Mungu kwa moyo wote pasipo kukamatwa na roho ya kuoa na kuolewa.

Kumbuka hili;
• Chombo kinachotumiwa sana,ndicho kinachosafishwa sana.
Kikombe unachokitumia sana ndicho hukisafisha sana kuliko vyoote.
Vivyo hivyo,ukitumika kwa kazi ya Mungu sana basi ndivyo utakavyokirimiwa sana. Mwenzi wako atavutwa kokote kule alipo,haijalishi yupo mkoa gani,wala hajilishi yupo taifa gani bali atakuja kwako sababu wewe unamtumikia vyema Mungu wako,na wala si kwa sababu unaomba sana maombi ya kuoa na kuolewa.

Ninao ushuhuda wa mama mmoja aliyekuwa hajaolewa ila katika pita pita yake huko ujanani alikutana na mwanaume mmoja akazaa naye mtoto. Huyu mama alitamani aolewe na yule mwanaume,lakini kumbe yule mwanaume alikuwa amekwishaoa tayari. Kilichotokea;
Huyu mama akajibidiisha kwa kazi ya Mungu sana,kisha Bwana Mungu akajua hitaji lake,akamjibu na akampatia mume wa kulea yule kijana na kulea watoto wengine watakao barikiwa na Mungu.

Kumbe katika kutulia yapo mafanikio ya kumpata mwenzi bora atokaye kwa Bwana Mungu mwenyewe.
Achana na yale maombi ya kila siku ya kuomba uolewe tu,maana kama kuomba umeomba sana,sasa unahitajika kubadili staili/ mfumo wote wa maombi na kugeukia katika kufanya kazi ya Mungu kwa usahihi zaidi,yaani kutumika zaidi mahali unapoabudu. Kama ulikuwa haupo katika kwaya basi jiunge kwaya umwimbie Bwana kwa moyo wako wote,na kwa akili na nguvu yako yote.

Au
Kama wewe si mmoja wa watenda kazi hapo unapoabudu basi jiunge na kundi la watenda kazi. Au la! nenda basi hata kusafisha vyoo vya kanisa na upangaji wa viti na usafi kwa ujumla,kwa moyo mmoja wa kumpenda Bwana Mungu wala sio kwa ajili ya kutaka kuoa au kuolewa.Fanya hivyo kisha uone kama Bwana Mungu ajakutetea kwa kila jambo.Usikae pasipo kuifanya kazi ya Bwana Mungu.

• Kuna watu kanisani si wanamombi,wala si viongozi,wala si wanakwaya,wala si watenda kazi yoyote ile,yaani hawaeleweki ni waamini wa namna gani? Kazi yao ni kuja kanisani na kuondoka kama walivyokuja huku wakingangana kwa Bwana kwa vijimaombi vyao vya kutaka kuolewa au kuoa.
Kuolewa/Kuoa ndio maombi yao ya kila siku kama wimbo wa taifa usiobadilika,wakati kuna mambo makubwa ya kiroho yanayohitajika kuomba. Staili hii ya maombi ni UTOTO WA KIROHO.
Mimi ninawashangaaga watu waliokosa mambo ya kuomba, maana mambo ya kuombea yapo mengi mno. Tusigande kungangana kwa maombi ya kuoa na kuolewa tu.
Imefika wakati sasa wa kuyabadili maombi ya namna hii na kuelekea katika kutenda kazi ya Bwana kwa mikono yetu wenyewe huku tukizidi sana kuomba mambo ya kiroho.
Fanya kazi ya Mungu ili Mungu afanye kazi yako. Tumika katika ufalme wake Mungu,kisha Mungu atakuletea yule aliye sahihi katika maisha yako.

Mahusiano ni jambo kubwa sana lenye kuchukua nafasi kubwa sana katika kanisa. Haipaswi kuingia katika mahusiano ya kimapenzi kabisa isipokuwa hali ya uchumba usiohusisha kujamiaana. Uchumba safi ni ruksa kwa kanisa.
Tusiige watu wa mataifa wanaoitana " boy friend,& girl friend " huku wakilala pamoja kama mke na mume, HII NI DHAMBI!
Masuala haya ni ya watu wa mataifa,hayahitajiki kabisa kanisani.
Ndani ya kanisa,mahusiano ya uchumba hakuna KUONJANA,mtaonjana na kujuana mkishaoana.

Tena;
Ukimpenda mtu,basi fuata taratibu zote za kanisa. Usipige kona kona,NI DHAMBI!
Tulia kwa Bwana,Bwana akutendee.

Kwa huduma ya maombi na maombezi,usisite kunipigia kwa namba yangu hii;
0655-111149.

UBARIKIWE.

Comments