DHAMBI YA MAKUSUDI

Na Frank Philip

“BWANA akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha. Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli katika habari za nyumba yake, tangu mwanzo hata mwisho. Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye
hakuwazuia. Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele.” (1 Samweli 3:11-13).

Nimetazama mistari hii nikajiuliza ni kwanini HASIRA ya Mungu ilikuwa kali kiasi hiki? Kwani tofauti ya hii dhambi ya hawa wana wa Eli, ambao walikuwa makuhani, na dhambi za watu wengine waliopata rehema ilikuwaje? Angalia mwenyewe hii hasira, “Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele”. Mungu alikasirika na kuhukumu nyumba nzima ya Eli, na kufuta baraka, na ahadi zake alizowapa, hata milele! (1 Samweli 2:30).

Nikisoma naona mahali ambapo kuhani Eli akijitahidi kwa namna fulani kuwaonya watoto wake, ona hapa “Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote. Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa BWANA. Mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa BWANA, ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu BWANA amekusudia kuwaua” (1 Samweli 2:23-25). Kama aliwaonya, shida ilikuwa wapi? Katika kutafuta jambo la zaidi ya KUONYA, nikaona neno hili “nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia”. Sasa kuna tofauti ya KUONYA na KUZUIA uovu usitokee. Kosa la Eli, aliwaonya ila HAKUWAZUIA wasifanye machukizo kwa BWANA.

Nikifuatilia habari za Musa, na manabii wengine waliotangulia, naona jinsi hasira ya BWANA ilivyotulia/poozwa. Kwa mfano, Haruni alipotoa kibali cha kutengeneza “mungu ndama” wa dhahabu, na watu wakaiabudu KINYUME na Mungu wao; Musa hakuonya na kukemea tu, ila alivunja yule ndama na kumsaga-saga. Kuna mifano mingi ya namna hii. Sasa sikurudishi kwenye Torati ambapo uovu ulilipizwa kwa sharia (jino kwa jino), ila jiulize, katika UOVU wako binafsi, na wa nyumba yako, je! umefanya nini zaidi ya kuonya? Sasa angalia usimtende BWANA dhambi ukijitahidi kuzuia uovu, ila nenda mbele za BWANA kwa ajili ya uovu wako binafsi, au watu wa nyumbani mwako, ili iwepo Neema ya kuwasaidia kuwaepusha na laana.

Sasa nataka ujue kwamba kila mtu anatenda dhambi, ila kuna tofauti ya kutenda dhambi kwa makusudi, na kutenda dhambi kwa kujikwaa. Yohana anasema, “Twajua ya kuwa KILA mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi” (1 Yohana 5:18). Sasa usidhani sijui kazi ya Neema, je! Unajilinda? Angalia neno hili, kujilinda ni zaidi ya kujua hatari (maonyo); ni HATUA ambazo mtu anachukua kuepuka uovu. Je! Umechukua hatua zipi KUJILINDA ili usitende dhambi? Ukiona mtu anatenda dhambi ile ile, mwaka mzima, na mwaka ujao tena, huyo hajikwai, ila AMEAMUA kutenda “hiyo” dhambi kwa makusudi. Ukikutana na mtu wa sampuli hii muulize, je! Amechukua HATUA gani za kujilinda ili asitende “hiyo” dhambi? Au ulidhani NEEMA maana yake ni Yesu kuja kukufunga miguu na mikono ili usimtende Mungu dhambi? Kama ingekuwa hivyo, basi angeanza na hawa Finehasi na Hofni, wana wa Eli, kwa maana walimchukiza sana BWANA kwa uovu wao mkuu (1 Samweli 2:17). Mungu akamwambia Eli, “HUKUWAZUIA kufanya huo uovu”! na hiyo ikawa dhambi kubwa kwa ajili ya Eli na nyumba yake yote.

Nitakuonesha jambo, hasa kwa mabinti/wanawake ambao wanabeba jina la kuwa hai lakini wamekufa. Ona hii nia iliyokwa ndani ya Naomi, “Kisha Naomi akamwambia mkwewe (Ruthu), Je! Mwanangu, si vizuri nikutafutie raha, ili upate mema?” (Ruthu 3:1). Kumbuka, hapo kabla, kwenye Ruth 1:8 na 9, Naomi alimshauri Ruthu na mjane mwenzake, warudi kwao wakaolewe na wanaume wengine, ila Ruthu alikataa. Ruthu hakuwa na NIA ya kutafuta mwanaume, aliamua kukaa na kutulia. Angalia jambo hili ambalo Naomi anamshauri huyu binti akafanye, “Tazama, usiku wa leo atakuwa akipepeta shayiri pale ugani. Basi wewe oga, ujipake mafuta ujivike mavazi yako, kisha uende kwenye uga; walakini usijionyeshe kwake mtu yule, ila atakapokwisha kula na kunywa. Nayo itakuwa wakati atakapolala, utapaangalia mahali alalapo, nawe uingie, uifunue miguu yake ujilaze hapo; na YEYE ATAKUAMBIA UTAKALOFANYA. Akamwambia, Hayo yote unenayo mimi nitayafanya” (Ruth3:2b-4). Je! Hivi sivyo na Ibilisi anavyowashawishi watu wengi, kutenda kwa hila, huku wakijua mioyoni mwao “kitakachotokea” mbele, nao wakaenda kwa miguu yao wenyewe?

Ona huu mtego, Naomi anamwambia huyu mwanamke Ruthu, jinsi ya KUMTEGA Boazi, ili AZINI naye. Sasa nataka ujue jambo hili, Naomi alimwambia Ruthu aende WAKATI wa usiku, sio nyumbani kwa Boazi ambapo kuna mkewe na wanawe, la! Amfuate Ugani; kisha asubiri ALE na KUNYWA, yamkini ilikuwa pombe, yaani asubiri hadi Boazi ALEWE. Ruthu akaambiwa AJIFICHE, ila achunguze Boazi alalapo, na kisha ajilaze miguuni pa Boazi, umeona jambo hili? Yaani, huko usiku wa manena, Boazi akijinyoosha miguu yake agundue anakanyaga mtu, astuke! Binti kaoga, kajipaka mafuta, kavaa nguo rasmi, anang’aa! Ona jambo hili. Je! Hayo hayapo katikati yetu hadi leo? Utaona binti/mwanamke ANAJUA nafsini mwake kwamba LITATOKEA “jambo”, ila anakwenda akiwa AMEJIANDAA kabisa! Huku akijifariji kwamba “mimi sikukubaliana naye hili jambo, ila amenistukiza na kunitenza kwa nguvu”! Angalia tena hii akili ya Naomi, “uifunue miguu yake ujilaze hapo; na YEYE ATAKUAMBIA UTAKALOFANYA”. Hata mnyama akiletewa jike, huwa ANAJUA cha kufanya, haambiwi kitu. Usimlaumu DUME, laumu huyu aliyepelekea JIKE kwa dume, au jike LILILOJIPELEKA kwa dume. Kwa mtizamo wangu, hii ni DHAMBI ya MAKUSUDI kabisa. Hata kama hukupewa taarifa, mkakubaliana na kupanga, hii haiitwi KUJIKWAA, hii ni dhambi ya MAKUSUDI kabisa.

Sasa nakuagiza katika Roho Mtakatifu, kama unamcha BWANA, na umeamua kumfuata, una jina la kuwa hai, chagua hivi leo. Mungu sio mwanadamu hata umtende kwa HILA. Acha mara moja TABIA hii ya KUFANYA dhambi na kuweka LAWAMA kwa wengine, usipoacha hakika tabia hiyo itakuangamiza. Ukisikia “aonywaye mara nyingi, akishupaza shingo, atavunjika shingo na hapati dawa”, usidhani ni utani, imetokea kwa Eli; hii dhambi ya wanae, walionywa hawakusikia, wakashupaza shingo, na sasa, hakuna dawa hata milele; ona tena, “nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele”, shingo zao hazikupata dawa hata leo.

Jilinde, mtafute BWANA katika majaribu yako kwa maana LAZIMA utajaribiwa tu, omba msaada wa maombi ukiona unaelemewa, usiache kukusanyika na waaminio, dumu katika Neno na Sala, utashinda na utapona katika mengi.

Frank Philip.

Comments