JUA NAMNA YA KUMILIKI MAZINGIRA YAKO KIROHO

Na Nickson Mabena


Bwana Yesu asifiwe, karibu tujifunze pamoja somo hili la MAOMBI ambalo Roho Mtakatifu ameruhusu tulijue kwa wakati huu. Kwani hakuna namna yoyote tunaweza tukafanikiwa bila Maombi, na kwenye Maombi yanahitajika maarifa, kwani Mungu hawezi kusema na wewe nje ya Maarifa uliyonayo……..!!.

UTANGULIZI

Mazingira yanaweza yakambadilisha Mtu, kwa sababu hiyo watu wengi sana wamejikuta wamebadilishwa na mazingira yanayo wazunguka bila wao kujua!.
Watu wameshindwa kujua ni namna gani wanaweza wakayamiliki mazingira hayo, ngoja nikupe mfano kidogo ili ujue ninachomaanisha ninaposema mtu anabadilishwa na mazingira; Unaweza ukamkuta mtu akiwa katika maisha ya nyumbani anastawi vizuri tu kiroho, anafanya huduma kama kawaida au kanisani hakosi na anakuwa mstari wa mbele hata kuwahamasisha wengine kuhusu mambo ya Mungu, lakini cha ajabu mtu huyo huyo anayeyafanya hayo , siku akienda sehemu nyingine anajishangaa kwa nini hawezi tena kufanya kama alivyokuwa anafanya, yaani anajikuta haoni umuhimu tena wa kwenda kanisani au kufanya huduma, yaani anajikuta anashindwa kustawi kama mwanzo.

Wengine wamebadilishwa walipofika tu kwenye ofisi zao (Watu wanaopelekwa ofisi zingine kikazi).
Wewe mwenyewe unaweza ukawa shahidi, kuna watu walipofika chuoni/shuleni kwako walikuwa na moto wa Mungu, lakini baada ya mda kidogo tu anaanza kupoa taratibu mwisho wake anapotea kabisa.

Au Wasichana wanapata mimba wanapoenda mashuleni au vyuoni wakati nyumbani kwao wametoka ni waimba kwaya wazuri tu!,
Na wengine hufanya maamuzi ya kutoa mimba yenyewe kabisa, kwani akirudi likizo inabidi waingie studio kurekodi na wao ndiyo ma’solo’ wa nyimbo za kwaya yao!!.
Watu wa namna hiyo anakuwa wameshindwa kuyamiliki mazingira yao kiroho.
Kwani mtu aliyeokoka anatakiwa kuyabadilisha mazingira, na sio mazingira yambadilishe yeye!!.
SASA, ATAWEZAJE KUYAMILIKI!?, hebu kwanza tuzione sababu za kumiliki!....

ZIFUATAZO NI SABABU ZA KUMILIKI

1. NDANI YETU YUPO MUNGU ALIYE HAI

“Tena pana mapatano gani kati ya hekalu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.” 2KOR 6:16
Kwa kuwa Mungu mwenye nguvu anaishi ndani yetu, tena anatembea katikati yetu, basi tunaweza kuyamiliki mazingira yoyote yale tunayokutana nayo pasipo kubadilishwa nayo!.

2. TUMEFANYWA UPYA NIA ZETU

Maisha yetu yamebadilishwa, sio yale tuliyoyaishi mwanzo kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, haya yamefanywa upya na Yesu mwenyewe kwa Damu yake iliyomwagika pale msalabani, kwa sababu hiyo, tunaweza tukayamiliki mazingira kiroho.
Paulo aliwaandikia Warumi, alipotaka wayatawale na kuyamiliki mazingira yanayowazunguka, pamoja na kuwa Dunia ina namna yake inavyoenenda, katikati ya mazingira hayo hayo aliwaambia;

“Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu” RUMI 12:2
Ili usiifuatishe namna ya dunia hii, au usii ili uyajue mapenzi ya Mungu na kuyafanya, lazima ufanywe upya nia yako. Usinie kama zamani, usikusudie kama zamani bali “na mfanywe wapya katika roho na nia zenu” EFESO 4:23, Kwa Yesu tumefanywa upya, tutasitawi kiroho, kiuchumi hata kihuduma!.

3. KWA SABABU TUNALIITIA JINA LA BWANA

“Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa” MDO 2:21
Kwenye eneo lolote tunalofika, cha kwanza kabisa ni KULIITIA JINA LA BWANA, lazima tumiliki kwanza kwa jina la YESU……

Mtu mwingine anafika tu kwenye eneo Fulani, cha kwanza anaanza na mipango yake, bila kuliitia jina la Yesu, matokeo yake mambo baadae yanakuwa magumu, kwani hajui kwamba katika kila eneo yupo anayelimiliki kiroho, ndiyo maana ni lazima tuanze kwa kuliitia jina la Bwana Yesu, Mungu wa miungu.
Wanaofanya mikutano ya injili maeneo mbalimbali wanaelewa zaidi, kwani huwezi tu kuweka mkutano au semina mahali bila kuanza kwa kuliitia jina la Bwana!.

4. SISI NI UZAO MTEULE

Sisi sio watu wa kuyumbishwa na mazingira, au maisha flani.
Ona kile neno la Mungu linachokisema juu yetu
“Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kutangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu” 1PETRO 2:9

Usikubali kuyumbishwa ovyo wakati wewe ni Mteule, umachaguliwa na Mungu mwenyewe kama neno lale linavyosema, kwamba wewe ni mtu wa MILKI YA MUNGU.
Kanisa ni uzao wa Ibrahimu, ndiyo maana unapookoka unakuwa Myahudi wa kiroho. Kama sisi ni uzao wa Ibrahimu, Je! Ibrahimu aliambiwa nini!? Tusome wote
“BWANA akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu BWANA aliyemtokea” MWANZO 12:7

Pia ona “maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele” MWANZO 13:15
Ibrahimu aliahidiwa kumiliki eneo, yeye pamoja na uzao wake ambao ni kanisa la Bwana Yesu.
Mtumishi wa Mungu Musa, aliijua siri hii ya ajabu, Hasira ya Mungu ilipowaka juu ya wana wa Israeli, alimkumbusha Mungu

“Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kiazazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele” KUTOKA 32:13

Je! Wewe umeijua siri hii?, kumbuka tunajifunza juu ya kumiliki mazingira yako kiroho (NA SIO KUMILIKI MASHAMBA NA MAENEO).
Na wewe ni Uzao wa Ibrahimu, unaweza ukafanya kama alivyofanya Musa kwenye maombi, na utashangaa utakavyouona mkono wa Yesu.
Kwa nini ushindwe kuimiliki kiroho ofisi unayofanyia kazi!?, kwa ushindwe kumiliki eneo la Shule/Chuo kiroho?, hadi umekubali kubadilishwa na hayo mazingira?

Hata unakuwa na hofu, wala huna ujasiri tena wa kutangaza habari za Yesu!. Ni wakati wako sasa kuamka na kuamua kumiliki na kutawala kiroho, kwani Neno la Mungu linasema

“Kila mahali zitakapokanyaga nyayo za miguu yenu nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa” YOSHUA 1:3
Na Damu ya Yesu, iliyomwagika katika miguu yake inatupa uhalali huo.

5. KWA SABABU TUNAISHI MAISHA YA KUMPENDEZA MUNGU

“Wakati huo BWANA akamwambia Yoshua, haya, jifanyie visu vya mawe ya gumegume, watahiri tena wana wa Israeli mara ya pili. Basi Yoshua akajifanyia visu vya mawe ya gumegume, akawatahiri wana wa Israeli huko Gibea-haaralothi. Na sababu ya Yoshua kutahiri ni hii; watu wote waliotoka Misri, waliokuwa waume, hao watu waume wote waendao vitani walikufa katika bara njiani, baada ya wao kutoka Misri” YOSHUA 5:2-4

UFUNUO 5:10Waliofia njiani ni wale wasiotii sauti ya BWANA(YOSHUA 5:6).

Tohara ilikuwa ishara ya UTAKATIFU, kwani huwezi kumiliki bila ya kuwa Mtakatifu, na Utakatifu ni gharama kubwa ndiyo maana Yoshua aliwatahiri kwa MAWE!. Yoshua alifanya wenziwe wawe watakatifu yeye mwenyewe akaambiwa avue viatu vyake miguuni (YOSHUA 5:15).

Tunapokuwa watakatifu, tunaweza tukayamiliki na kuyatawala mazingira yoyote yale, kwani Mungu aliye Mtakatifu sana anakuwa upande wetu!.
Ishi maisha ya Utakatifu, utakuwa mshindi popote utakapokanyaga…….!!.

NAMNA YA KUMILIKI

Baada ya Kuona baadhi ya sababu za kutufanya tumiliki, hebu tumalizie kwa kuangalia namna ya kumiliki.
“ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi” UFUNUO 5:10

Yesu kwa DAMU yake ametufanya kuwa wafalme, na Mfalme lazima anakuwa na walinzi!, unatakiwa kutembea kifua mbele kwani wewe si mtu wa kawaida kwenye ulimwengu waroho………

Namna gani sasa utamiliki, ni kwa kufanya Maombi; na kwenye somo hili nakupa aina moja tu ya Maombi ambayo unaweza ukaifanya (INGAWA ROHO MTAKATIFU ANAWEZA AKAKUPA AINA ZINGINE).

FANYA MAOMBI YA KUMUWEKEA SHETANI MIPAKA

Ukuta wa Yeriko ulipobomoka, haukujengwa tena, kwa sababu Yoshua Mtumishi wa Mungu aliweka mipaka katika ulimwengu war oho;
“Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za BWANA mtu Yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake, kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na motto wake mwanamume aliye mdogo” YOSHUA 6:26

Baada ya Yoshua kuweka mpaka huo, katika ulimwengu wa roho, Je! Maneno yake yalitimia?

Neno la Mungu linasema
“Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.” 1WAFALME 16:34

Si umeona kilivyotimia alichokisema Mtumishi wa Mungu Yoshua, kwa kuweka mipaka katika ulimwengu wa roho!,

Na wewe ni Mtumishi wa Mungu,
hebu muwekee shetani mipaka kwenye ndoa yako, weka mipaka kwenye huduma yako ili asiichezee tena, muwekee mipaka katika Jina la Yesu, na wewe neno lako litatimia tu.

Mwambie uasherati basi, uzinzi basi, kudumaa kiroho basi, hakuwezi tena, amekurudisha nyuma vya kutosha sasa ni wakati wa kutawala na kumiliki!

Muwekee shetani mipaka kwenya Masomo yako, weka Mipaka kwenye Ofisi yako, kwenye UCHUMBA wako, kwenye ujana wako hata ubinti wako……!!

Roho Mtakatifu akusaidie ujue namna ya kuomba ipasavyo (RUMI 8:26).
NB: HUWEZI KUJUA KUOMBA, ISIPOKUWA UMEOMBA!

NAKUBARIKI KWA JINA LA YESU!
By Nickson Mabena.

Comments