KAINI ALIPOTOKA MBELE ZA USO WA BWANA,AKAKAA KATIKA NCHI YA NODI,KAINI AKAMJUA MKEWE;SWALI HUYU MKE ALITOKA WAPI? AU JE KULIKUWA NA WANADAMU WENGINE WAKIISHI? Mwanzo 4:16-17.

jungle_trail
Na Mtumishi wa Mungu Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Nakusalimu ndugu mpendwa katika jina la Bwana Yesu. Awali ya yote nikuambie kwamba wewe usomaye ujumbe huu umebahatika kujifunza mambo makubwa mazuri ya kuzijua siri za ufalme wa Mungu kupitia mahali hapa.
Fundisho la leo limebeba moja ya swali linaloulizwa mara nyingi haswa kwa wakristo wasomao Biblia,sijui kama wewe ulishawahi kujiuliza swali hilo hapo juu,au kama ulishawahi kuulizwa.
Mimi binafsi nilishawahi kuulizwa mara tu nilipomaliza mkutano wa nje wa injili mkoani Tanga. Tulipokuwa katika mafundisho ya ndani ya kuwafundisha wale waliokoka mara ya kwanza,ndipo nilipoulizwa na mdada mmoja aliyeokoka katika moja ya siku ya mkutano. Aliniuliza hivi;
” Mtumishi,Biblia inasema Kaini alipotoka mbele za uso wa BWANA,akakaa katika nchi ya Nodi huko akaoa mke,sasa huyo mwanamke alitoka wapi,? Maana tunajua kwamba watu walikuwa ni Adamu na Hawa pamoja na yeye Kaini baada ya Abili kuuwawa sasa huyo mwanamke ametoka wapi?…”
Bwana Yesu asifiwe…
Nilichomjibu ndicho ninachokujibu wewe siku ya leo kwa ufupi sana.
• JIBU;
Ikumbukwe kuwa Adamu alikuwa na wana wengine wa kike na wakiume.
Hivyo,ni dhahili kabisa Kaini alikuja kumuoa mmoja wa ndugu yake( mmoja wa wadogo zake)

• Katika jamii ya zamani ya kiyahudi,wanawake walikuwa hawahesabiwi kama ikiwa si malango.
Mfano wa malango katika uzao wa Adamu;
Abili alikuwa ni lango,
Sethi alikuwa ni lango,
Enoshi naye ni lango,
Na hata pia Kaini alikuwa ni lango. Na wengine waliofuata.

• Lakini pia wanawake ambao ni malango,walitajwa Mfano akina Esta,Debora nabii mke,N.K
Hivyo Adamu alikuwa na watoto wengine wa kiume na wakike ambao si malango,wana wa aina hii hawakuhesabiwa au kutajwa.
• Malango ni vichwa vya kabila,familia au ukoo au vichwa katika uzao vyenye uwezo wa kupitisha mambo mazuri au mabaya katika ukoo,mfano mzuri ni katika kile kilichoandikwa katika kitabu cha Hesabu 13:3.

Bwana Yesu asifiwe…
Biblia inasema;
” Siku za Adamu baada ya kumzaa Sethi zilikuwa miaka mia nane, akazaa wana, waume na wake. ” Mwanzo 5:4

Watoto waliozaliwa hawakutajwa kwa majina yao katika huo mstari,ikionesha kwamba hawakuwa malango.
Hivyo;
Mara nyingi Biblia haipangi vizazi kwa mfuatano bali kwa kuangalia malango ya familia,maana kama ingelipanga kufuata vizazi kama vizazi basi tusingejiuliza swali la namna hiyo maana tungeliona labda baada ya kuzaliwa Kaini na Abili,papo hapo wangelitajwa na vizazi vyote kwa mfululizo. Labda tuliangalie jambo hili kiundani kidogo, tazama kizazi cha Nuhu.

Ukisoma katika kitabu cha Mwanzo 5: 32,imeandikwa;
“Nuhu alikuwa mwenye miaka mia tano, Nuhu akawazaa Shemu, na Hamu, na Yafethi. “

Hapo unaweza kudhani ya kwamba Shemu alikuwa ni mtoto wa kwanza wa Nuhu,akifuatiwa na Hamu mtoto wa pili na akifuatiwa na Yafethi mtoto wa mwisho wa Nuhu,kumbe! SIVYO!
• Mtoto wa kwanza wa Nuhu ni Yafethi,ingawa katika kutajwa amewekwa mwisho sababu ya suala la MALANGO.
Naipenda Biblia ya amplified bible,imeeleza vizuri mno,inaweka wazi kuwa Yafethi ni mkubwa wao,tazama inasema;

” To Shem also, the younger brother of Japheth and the ancestor of all the children of Eber [including the Hebrews], children were born.”
” the younger brother of Japheth” Maana yake Shemu ni mdogo wa Jafethi. Hivyo Kama Biblia ingelikuwa inataja vizazi kama vizazi vya kawaida, Basi angeliandikwa hivi,
Watoto wa Nuhu ni, Yafethi,Shemu na Hamu,badala ya Shemu Hamu na Yafethi,Hii yote ni kwa sababu ya suala la malango. Hamu ni mdogo wa wote,
Imeandikwa ya kwamba Hamu ndie aliyemchungulia baba yao Nuhu,

” Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea. ” Mwanzo 9:24
Hivyo yatupasa kuyaelewa hayo pindi tusomapo Biblia. Biblia ni kitabu kilichotaja malango ndio maana kama hukujua malango ni nini inaweza kukupa taabu kidogo.
Bwana Yesu asifiwe,…
Alikadhalika, Adamu alikuwa na watoto wengine waliokuwa hawakutajwa. Hivyo Kaini alioa mmoja wa ndugu yake.
Kama ndivyo hivyo,basi ikumbukwe kuwa Kaini ndio mtu wa kwanza kabisa kuoa ndugu yake. Ndoa za ndugu kwa ndugu ziliruhusiwa kipindi hicho.

Na ikumbukwe kuwa ndoa zaidi ya mke mmoja ilianzia kwa kizazi cha Kaini. Iliruhusiwa kwa muda huo mpaka Yesu alipokuja na kuilekebisha.
Tazama habari ya ndoa ya kaini na kizazi chake.
Kizazi cha Kaini kile kizazi sita ukianzia Kaini,Henoko,Iradi,Mehuyaeli,Methushaeli na Lameki ( Mwanzo 4:17-18) Katika kizazi cha sita,kizazi cha Lameki ndipo muingiliano wa ndoa za wake wawili zinaanza,tazama;

” Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila. ” Mwanzo 4:19.
Sasa;
Ukoo wa Kaini ukatoka nje ya mpango wa Mungu,kwao wakazaliwa wana wa wanadamu. Hapo ndipo asili ya uovu wa kwanza chini ya jua hili,na kulepelekea gharika. Pale tusomapo ” wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wowote waliowachagua.” Mwanzo 6:2

Kizazi cha Sethi kiliwakilisha wana wa Mungu,wakati wana wa wanadamu walikuwa ni kizazi cha Kaini. Hata hivyo haisemekani kuwa kizazi chote cha Kaini kilikuwa ni kiovu,maana neema ya Bwana ni kuu mno.
Ni hayo tu kwa ufupi,
• Ikiwa hujampa maisha Bwana Yesu,ali awe Bwana na mwokozi wako,yaani bado hujaokoka, basi usisite kunipigia kwa namba yangu hii ili Bwana Mungu akuhudumie sasa;
Piga sasa kwa namba iliyopo hapo juu.

UBARIKIWE


Na Mtumishi wa Mungu Gasper Madumla.
.

Comments