KUMJUA MUNGU

Na Frank Philip.


“Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu (Goliath); mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake. Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai. Daudi akasema, BWANA aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na BWANA atakuwa pamoja nawe” (1 Samweli 17:32-37).

Nimekutana na watu wengi wanasema “wanamjua Mungu”, hakika wapo watu wanamjua Mungu, ila kwa viwango tofauti. Sio kila mtu mwenye TAARIFA za Mungu ANAMJUA Mungu. Kuna tofauti kubwa sana kati ya TAARIFA (kufahamu) na KUMJUA Mungu. Kwa lugha ya kigeni tunasema EXPERIENCE with God. Sio kila mtu anayesikia habari za Mungu amemjua kwa experience. Daudi alifikia kiwango cha kumjua Mungu zaidi ya watu wengi wa wakati wake kwa sababu ALIPITISHWA mahali ambapo ALIJUA kwamba “huyu ni Mungu” ameniokoa/saidia na sio mwanadamu.

Sijui kama unajua MAJIBU ya maombi yako ya kutaka kumjua Mungu yanajibiwaje? Mungu humfundisha mtu KUMJUA kwa VITENDO na sio kwa NADHARIA tu. Sasa, unapomwomba Mungu, na kusema, “Mungu nataka nikujue”, kaa tayari anapokufundisha kwamba yeye ni nani. Akitaka kujifunua kwako kama BWANA wa vita, kaa tayari kupambana. Akitaka kujifunua kwako kama mponyaji, kaa tayari kuletewa wagonjwa/ugonjwa na wewe kuwawekea mikono na Bwana akaponya, nk. Ukivuka mambo ya namna hii, utagundua kwamba kiwango chako cha KUMJUA Mungu kimeongezeka zaidi ya ULIVYOSIKIA habari zake.

Haikumtosha Daudi kujua habari za Mungu; kila mtu alijua yuko Mungu wa Israel, ila wote walikwama kwa siku 40, wanatukanwa tu na Mfilisti asiyetahiriwa, kutwa mara 2. Hadi alipokuja mtu ambaye anaUZOEFU na Mungu kwa namna ya VITENDO, huko katika MAPITO yake, Daudi mwana wa Yese, ndipo ghafla! AKAJUA kwamba Goliath sio kitu kikubwa cha kusumbua mtu namna hii. Kumbuka, sio habari za Mungu, ila experience na Mungu huko kwa dubu na simba (changamoto za maisha).

Ukiona mambo MAGUMU yanakujia, usikimbilie kukemea tu, na kuteremkia Misri, hiyo ni nafasi nyingine ya KUMJUA Mungu wako. Kadri unavyofanikiwa KUSHINDA changamoto mbalimbali kwa KUMWAMINI na KUMTEGEMEA Mungu, na kutumia MBINU za Kimungu, ndivyo unaongezeka katika KUMJUA Mungu.

Frank Philip.

Comments