KUTENGENEZA

Na Frank Philip


“Lakini mmeniacha mimi, na kuitumikia miungu mingine; basi kwa ajili ya hayo mimi sitawaokoa tena. Haya, endeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua; na hiyo iwaokoe wakati wa kusumbuka kwenu. Wana wa Israeli wakamwambia BWANA Tumefanya dhambi; utufanyie yote uyaonayo kuwa ni mema; lakini tuokoe, twakusihi, siku hii ya leo, haya tu. Nao wakaiondoa hiyo miungu ya kigeni iliyokuwa kati yao, nao wakamtumikia BWANA; na roho yake ilihuzunika kwa sababu ya msiba wa Israeli” (Waamuzi 10:13-16).

Hakuna mwanadamu awezaye kujisifu kwamba HAKUTENDA dhambi, naam, hata watakatifu pia wametenda dhambi, na utakatifu wao sio wao wenyewe, ila wao ni watakatifu kwa sababu Mungu wao ni Mtakatifu. KILA mtu ametenda dhambi na anaweza kutenda dhambi, ILA kuna tofauti katika kutenda dhambi. Wapo watendao dhambi huku hawajui (kwa kutokujua maandiko/wasioamini), na wapo watendao dhambi kwa kujua (kwa makusudi kwa sababu wanajua Neno/waaminio). Wale wasiojua huitwa WAJINGA. Kuna neema juu ya wajinga, na ndipo Mungu anasema “alijifanya hazioni dhambi zao” (Matendo 17:30,31), Akawahurumia tu wasiangamie.

Kundi la pili ni watendao dhambi kwa makusudi. Kundi hili linaitwa la WAPUMBAVU. Hawa wanajua cha kufanya kama Neno la Mungu linavyowaagiza, lakini kwa makusudi kabisa wameamua kufanya yaliyo maovu. Sasa naweza pia kuligawa kundi la wapumbavu katika makundi mawili: Wapo watendao dhambi, kwa sababu iwayo yote, lakini HUGEUKA na KUTUBU, na wapo walioamua KUIISHI dhambi fulani kwa sababu iwayo yote. Hili kundi la WALIOAMUA kuiishi dhambi, hujikuta wanatubia dhambi moja kila siku na kuirudia kila siku tu.

Sasa nisikilize, kwa MJINGA huwa haiji adhabu kwanza, Mungu huleta SHULE ili ajue cha kufanya, ndipo anasema, “nyakati za ujinga alijifanya hazioni dhambi zenu, lakini sasa anaagiza watu wote watubu”, kwa sababu SASA wanajua makosa yao, IMEWAPASA kutubu (Matendo 17:30,31).

Sasa, kwa huruma za Mungu, huwa wapumbavu hawaangamii moja kwa moja tu. KWANZA, Mungu huleta mtu wa KUWAONYA, na kisha ataleta na mwingine na mwingine, hadi wawe wengi. Huyu Mpumbavu AKIONYWA “mara nyingi” asiposikia, shingo yake huvunjika, na hapati dawa. Mpumbavu akifika mahali amekwama, na kumlilia Mungu, ndipo utasikia Mungu anasema “Haya, endeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua; na hiyo iwaokoe wakati wa kusumbuka kwenu”. Ila akitubu Mungu ni wa rehema. Iko Damu ya Yesu inenayo mema kuliko ya Habili, ndio maana hakuna mtu atakimbia kwa ajili yako, kwa mfano wa Musa na makuhani wa zamani, ili kukutetea usipigwe; ile Damu ya Yesu ipo kukupatanisha, KAMA ukikubali na kutii.

Sijui kama unafahamu kwamba yule Mungu aliyeshusha moto, na kuangamiza manabii wa Baali ni yeye yule jana, leo na milele? Sijui kama unataarifa kwamba yule Mungu aliyewapiga wana wa Israeli kwa tauni, na hata wengine kumezwa na ardhi, ni huyu Mungu unayesema unamwabudu? Wakati ule, kabla ya Agano jipya, uovu ukiingia katikati ya wana wa Israel, ghafla tu walianza kuona ugonjwa unakula watu, au maadui wanainuka kufanya vita nao, na kuwasumbua, nk. Mara zote makuhani, waamuzi au manabii, walikimbia kuomba TOBA na UPATANISHO pamoja na KUTENGENEZA, ili mambo yakae sawa tena.

Njia rahisi ya Mungu kutowapiga watu ilikuwa kujificha mbali nao. Ukisikia jicho au sikio la Mungu halioni/halisikii kwa sababu ya dhambi za watu (Isaya 59:1-3), sio kwamba dhambi zako zina nguvu kumzuia Mungu asikuone au asikusikie, la hasha, Mungu anaamua kukaa mbali ili asikuangamize; ndio sasa, adui zako hupata nafasi ya kukusumbua kwa sababu Mkono wa Mungu umeondoka maishani mwako. Ukisoma habari za Joshua utaona walivyoshindwa na adui zao, kumbe! Kuna KITU KIOVU katikati yao; Mungu akaondoka katikati yao ili kuwapigania, wakapigwa na adui zao (Yoshua 8).

Watu wengi sana wanajua KUTUBU, ila ni wagumu KUTENGENEZA. Ukitaka kumwona Mungu TENA, jifunze siri hii: TUBU, MGEUKIE BWANA, na kisha ONDOA KITU KIOVU KATIKATI YAKO. Angalia tena hapa, “Nao wakaiondoa hiyo miungu ya kigeni iliyokuwa kati yao, nao wakamtumikia BWANA; na roho yake ilihuzunika kwa sababu ya msiba wa Israeli”. Kama umetubu na kumrudia Bwana, hiyo madhabahu za miungu mingine ni za nini? Kama umeachana na hayo maisha ya kale, mbona unazidi kujihusisha tena na hivyo vitu au watu waliokupeleka njia za miungu yao hata ukamkosea Mungu wako? Je! Unajua Mungu hachanganywi na miungu mingine? Je! Unajua hupati FAIDA bila kukubali kupata HASARA ya mambo yote, kama Mtume Paulo alivyofanya?

Neema na amani ya Yesu Kristo ikawe nawe tangu sasa na hata milele.

Frank Philip.

Comments