MADHABAHU YA KUSHINDWA

Na Mchungaji  ADRIANO MAKAZI, Ufufuo na Uzima,Tanganyika parkers Kawe

Madhabahu ni eneo linalojengwa na mtu au watu kwa ajili ya kutolea kafara.  Kafara hii yaweza kuwa mbuzi, ng’ombe au mwanadamu. Ziko madhabahu  maeneo mbalimbali zilizojengwa ili kila jambo atakalolifanya mtu fulani lisifanikiwe. Mtu anaweza kufungua duka halafu baada ya muda akalifunga kwasababu ya kutokufanikiwa kinyume na matarajio yake. Kila analolifanya linashindikana, anakuwa mtu wa kushidwa shindwa. Mtu wa aina hii anatakiwa kutambua kuwa kuna madhabahu ya kushindwa aliyotengenezewa. Madhabahu inaweza kuwaleta watu pamoja, kumwabudu  na kusema na Mungu wa mbinguni au shetani. Unaweza kufika madhabahuni pa BWANA ukiwa mgonjwa lakini ukaondoka mahali hapo ukiwa mzima. Na hii ni kwa kuwa, madhabahu ni daraja la kumkutanisha Mungu na mwanadamu.

 WATU WALIOMJENGEA MUNGU MADHABAHU KATIKA BIBLIA

IBRAHIMU

Ibrahimu, baba wa imani aliambiwa na Mungu atoke katika nchi aliyozaliwa ya uru wa wakaldayo na aende katika nchi ya mbali BWANA atakayomuonyesha, na amjengee BWANA madhabahu huko. Ibrahimu  alitii neno la BWANA na akamjengea  madhabahu. Imeandikwa;

 Bwana akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea.
8 Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea Bwana madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana.
Mwanzo 12:7-8

Kupitia madhabahu hii aliyoagizwa kujenga Ibrahimu aliweza kuwasiliana na Mungu.

 Imeandikwa;

 Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Mwanzo 22:9

Ibrahimu alikuwa mtu aliyefanikiwa sana kutokana na madhabahu aliyoijenga. Kumbe madhabahu ni kiunganishi cha Baraka kutoka kwa Mungu anayeabudiwa kwenye madhabahu husika mpaka kwa anayeabudu. Hivyo ni dhahiri kuwa mikosi, balaa na matatizo mengine pia yana chanzo chake kutokea kwenye madhabahu. Kwa akili yako unaweza kuhisi kuwa kushindwa kwako ni kwasababu ya elimu yako ulionayo, au mtaji kidogo ulionao. Mawazo yako sio kweli wala sio sahihi, tambua kuwa kuna madhabahu imejengwa inayofanya kazi ya kupolomosha mambo yako. Leo kwa jina la Yesu tunabomoa kila madhabahu ya kushindwa kwako.

Katia nyakati tulizonazo leo, watu wanamjengea shetani madhabahu kwenye magari yao, ofisi zao na hata nyumba zao. Kutokana na madhabahu hizi, waweza kuona mtu anapandishwa cheo bila kustahili; wakati yule aliyestahili anahamishwa ofisi ghafla au anakufa. Ni madhabahu ya kushindwa imefanya kazi.

Bwana akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu.
Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko.
Mwanzo26:24-25.

Utaona Isaka kama ilivyokuwa kwa baba yake, yeye pia anamjengea MUNGU Yehovah madhabahu. Ili uweze kuwa na uhusiano wa kudumu Mungu uweze lazima umjengee  madhabahu. Pia tunaona kuwa anachokifanya baba mara nyingi mtoto naye hukifanya; hivyo aliyeabudiwa na baba mara nyingi ndiye ambaye huabudiwa na mwana.

Madhabahu inaweza kuwa chanzo cha Baraka zako au shida yako. Hivyo madhabahu zilizojengwa na wazazi wako au watu wa kale katika ukoo wako yaweza kuwa ndio chanzo cha Baraka au kushindwa kwako leo. Mfano Gideoni, alikuwa amekuwa mtu dhaifu kwa sababu alikuwa ameteswa na madhabahu ya kishetani  iliyokuwa imejengwa na baba yake.

Kila madhabahu inayojengwa hujengwa kwa sababu maalum. Ipo madhabahu imejengwa mahali kwa jina lako ili ushindwe na kufa katika matatizo uliyonayo. Unyonge wako ni kwasababu ya madhabahu iliyojengwa  ili ikutese. Leo tutawaagiza malaika wa BWANA wazisake madhabahu za kushindwa   zilizokufunga  kwa muda mrefu sana.

   UKIRI: MIMI NI SHUJAA WA BWANA, KWA MSAADA WA BWANA NALIENDEA JESHI NA KULIKANYAGA. NALIPONDA NA KULIONDOSHA  KWA JINA LA YESU.

NUHU

 Nuhu mara baada ya kutoka kwenye safina alimjengea BWANA madhabahu na kuweka sadaka mbele zake. Unapotaka kumtolea Mungu unapashwa kumtolea kilichosafi. Ili madhabahu iwe na nguvu lazima kuwepo sadaka juu yake tena iliyosafi. Mfano Habili alimtolea Mungu sadaka nono na yakupendeza na Mungu akapendezwa nayo. Ni vizuri kujiuliza kwanza kabla ya kumtolea Mungu sadaka kuwa unatoa nini mbele za BWANA?

Mara baada ya sadaka ya Nuhu mbele za BWANA, Mungu akafanya agano na Nuhu kuwa hataiangamiza tena nchi kwa gharika kama lile, na akaweka ishara ya upinde wa mvua. Imeandikwa:

 Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.Mwanzo 8:20

Unaweza kutafuta kwa taabu sana, hali ikawa nzuri baada ya taabu kubwa lakini kama kuna madhabahu ya kushindwa imejengwa kwa ajili yako utaishia kufa mara tu baada ya kupata. Tambua kuwa unapaswa kupigana na kushindana ndio amani ya maisha yako iweze kupatikana. Usisubiri kufarijiwa, faraja unatakiwa kuitafuta wewe mwenyewe kwa kupigana na kushindana juu ya ufalme wa giza. Imeandikwa:

Kwa maana kushindana kwetu sio juu ya damu na nyama…. Waefeso6:12

Tunatakiwa kushindana siku zote bila kuzimia mioyo. Wale waliokujengea madhabahu ya kushindwa wao pia hawakati tamaa. Hata pale wanapoona umeanza kuwa na bidii ya kuomba na kuhudhuria ibada. Wao pia huzidi kuimarisha madhabahu kwa kuzidi kutoa kafara ili kuendelea kukuweka katika hali ya kushindwa. Imeandikwa:

Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki.   2Wafalme3:26

UKIRI: Nakataa  kushindwa, nakataa kukata tamaa kwa jina la Yesu. Kila madhabahu ya kushindwa iliyojengwa  kwa jina langu naibomoa kwa jina la Yesu, kila madhabahu iliyojengwa angani, baharini, ufukweni au bondeni  ili mimi nishindwe, leo naibomoa kwa jina la Yesu. Kila madhabahu ya kukataliwa, kuonewa naibomoa kwa damu  ya Yesu. Amen.

Zamani watu walikuwa wanatoa kafara ili washinde vita, hata ulimwengu wa sasa watu wengine wanatoa kafara kwa mashetani ili waweze kushinda katika nafasi za ushindani kama vile biashara, utawala, vyeo maofisini, au kataika kutafuta kazi. Nawe pia lazima uingie katika ulimwengu wa kushindana na upate kushinda. Lakini ushindani wako wewe ni kinyume na wao, yakupasa kushindana kwa Jina la Yesu. Mtu anapokushinda, ujue amekutolea kafara kwenye madhabahu ya kishetani. Lakini neno la Mungu linatuonyesha kuwa Yesu alitoa kafara ya damu yake yenye thamani kuliko damu zote ili tupate kushinda siku zote.  Imeandikwa:   

Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. Ufunuo 12:11
Kafara ya Madhabahu

Kafara hii mara nyingi huwa ni damu inayomwagika juu ya madhabahu husika. Ukiharibu damu iliyo kwenye madhabahu, madhabahu haina nguvu tena. Kafara inayo mwagwa juu ya madhabahu ya mashetani ndiyo inayowapa nguvu ya kutenda jambo lolote la uharibifu juu ya wanadamu. Waganga na wachawi wanapotaka ushindwe, ukataliwe, uwe mgonjwa au upatwe na tatizo lolote; kafara ya damu ndiyo inayotumiwa kutenda kazi.


UKIRI:  Leo kwa jina la yesu kila damu inayonifanya nisishinde, niwe mgonjwa, nionewe, nainyamazisha kwa jina la Yesu.

Imeandikwa :

 Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Mwanzo 4:10

Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Mambo ya walawi 17:10

Kumbe basi kama damu inaweza kulia, vivyo hivyo yaweza kuongea. Hivyo kwa kadri ile damu iliyomwagwa juu ya madhabahu ya kushindwa inazidi kunena ndivyo na wewe unavyozidi kuwa mtu wa kushindwa. Hii ndiyo sababu Mungu alikataza tusile damu, maana ndimo ulimo uhai.

UKIRI: Kila aliyetoa kafara kuharibu ndoa yangu, damu iliyotolewa juu ya madhabahu ilitolewa ili mimi nishindwe na kuangamia, leo naiponda damu hiyo na kuisambarataisha kwa jina la Yesu. AMEN
 
MAOMBI:

Katika jina la Yesu Mungu baba naomba msamaha kwa kila dhambi niliyokutenda kwa kujua au kutokujua. Naomba unisamehe uovu wangu na unitakase kwa ajili ya vita. maana imeandikwa Daudi akivitakasa vita. Naomba unitakase na unisafishe kwa ajili ya vita. Amen

Kila madhabahu ya kushindwa iliyojengwa juu ya ukoo wetu ili uwe ukoo wa kushindwa au kufakufa, madhabahu iliyojengwa angani, mabondeni au milimani leo naibomoa kwa jina la Yesu.

Wewe uliyejenga madhabahu ya kukataliwa juu ya maisha yangu naiangusha leo kwa jina la Yesu. Imeandikwa: Nao wakamshinda kwa damu ya mwanakondoo na neno la ushuhuda wao. Ewe madhabahu nakushinda kwa jina la Yesu.  Wewe uliyenitesa kwa madhabahu yako leo nakupasua na naipasua na kafara yako kwa jina la Yesu. Kwa maana imeandikwa: Nimekuweka juu ya mataifa na juu ya falme ili kubomoa na kuvunja na kuharibu na kuangamiza katika jina la Yesu.

Kila madhabahu iliyojengwa ili niwe mtu wa kushindwa; kushindwa kwa familia, kushindwa kwa taifa langu ,ndoa yangu, masomo yangu  naibomoa kwa jina la Yesu. Nakuamuru kwa jina la Yesu toka ndani yangu, achia akili yangu, achia ufahamu wangu, achia  moyo wangu kwa jina la Yesu.

Kila madhabahu iliyojengwa juu ya familia ili tushindwe na kukataliwa naiangusha kwa jina la Yesu. Madhabahu iliyojengwa juu ya nchi yangu Tanzania naiangusha kwa jina la Yesu. Naamuru madhabahu ya kushindwa ipasuke kwa jina la Yesu na kafara ya madhabahu imwagike katika jina la Yesu.

Madhabahu zote njia panda, chini ya milima, mabondeni, nchi kavu naamuru zianguke  katika jina la yesu. Madhabahu iliyojengwa ili mimi niwe wa kupoteza, kuchanganyikiwa, maskini naivunja leo kwa jina la Yesu. Imendikwa: Mimi ni rungu la Bwana na silaha za BWANA za vita; naivunja madhabahu iliyojengwa juu ya mafanikio yangu, juu ya huduma yangu, madhabahu iliyojengwa ili nitumikishwe na mashetani au familia yangu naibomoa kwa jina la Yesu.

Madhabahu iliyojengwa kwenye mtaa wangu, kwenye ukoo wangu, kwenye mji wangu, kwenye nchi yangu naivunja na kuibomoa kwa jina la Yesu. Naipasua na kuiangamiza kwa jina la Yesu.

AMEN.

Comments