MATENDO MEMA NI AKIBA

Na Frank Philip


“Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikilia watu usiowajua tangu hapo. BWANA akujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake” (Ruthu 2:11, 12).

Naomi alikuwa ameolewa na Elimeleki, wote wawili ni Waizraeli; wakajaliwa watoto wawili wa kiume. Kukawa na njaa katika nchi, basi wakahamia Moabi. Huko Moabi, watoto wote wawili wakaoa wake wa Kimoabi, Orpa na Ruthu.

Kitambo kidogo, Elimeleki na watoto wake wawili wakafa, nyumba yake ikabaki na wajane watatu, Naomi, Orpa na Ruthu. Katika hali ya njaa, uhitaji na taabu nyingi, hawa mabinti wajane wakaambatana na “mama mkwe” wao, ambaye pia ni mjane. Wakapendana na kushikamana sana.

Angalia jambo hili, Naomi akawatizama hawa wajane wawili, bado umri wao ni mdogo tu, hawana watoto, akawahurumia na kuwapa kibali WAONDOKE waendelee na maisha yao, waolewe wakafurahi na waume zao. Orpa akakubali, Ruthu akakataa.

Pamoja na kwamba Naomi alikiri kwamba “mkono wa Mungu umeondoka juu yake” (Ruthu 1:13), ila BADO Mungu alikuwa Mungu wake. Haijalishi SHIDA na MATATIZO aliyopitia, alijua yeye ni wa Nani. Ruth akijua jambo hili, bado akakaza kusema, “Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa;BWANA anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami” (Ruthu 1:16, 17). Ruthu akaambatana na Naomi, wakarudi katika nchi ya Israel. Sasa angalia kitu Boazi anamwambia Ruthu, “Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikilia watu usiowajua tangu hapo. BWANA akujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake”. Matendo mema hayaozi, hata kama hakuna aliyeona, Mungu huona, na kuyahesabu, na kukuwekea akiba.

Angalia jambo hili, yale MATENDO MEMA Ruthu aliyomfanyia mama mkwe wake, yaani Naomi, na mumewe, hayakupotea, yalikuwa AKIBA iliyomsaidia huku mbele, na sasa ANALIPWA kwa kadri ya matendo yake! Ruthu akatendewa mema na moyo wake ukaburudishwa (Ruth 2:13).

Mara nyingi tunasahau kwamba “yale tuwatendeayo watu, hayo hayo nasi tutatendewa; mizani ile ile tuwapimiayo wengine, nasi tutapimiwa kwayo”, Ukichagua kutendea watu UOVU, jua umejichagulia kutendewa UOVU pia. Sio kwa sababu kuna mtu amekuona, ILA Mungu ameona, na ndio maana MALIPO huja kupitia mtu mwingine yeyote! Ndio maana BWANA wetu akatufundisha kuwa na rehema kwa wenzetu, kwa sababu tutavuna rehema pia (Mathayo 5:7). Ukimrehemu mtu, jua umeweka akiba tu, siku moja utakutana na rehema. Kanuni ya kupanda na kuvuna ipo siku zote, naam, hakuna apandaye zabibu na kuvuna tunu, kwa sababu Mungu hadhihakiwi, kile mkono wako upandacho hicho hicho utavuna (Wagalatia 6:7).

Basi jueni neno hili, kama watu hawata waamini kwa maneno yenu kwa habari ya Kristo, matendo yenu na yawe Injili itakayowafanya WAMWONE Mungu wenu, nao wataamini japo kwa matendo yenu. Je! Matendo si zaidi ya maneno? Na imani je? Utaitwa mwenye imani bila kuionesha kwa matendo yako?

Neema na amani ya Kristo vizidi kwenu.

Frank Philip.

Comments