MAWAZO YAKO

Na Frank Philip

Kile ukionacho/sikiacho ndicho ukiwazacho/semacho kwa kuwa kitaujaza moyo wako; na hicho huwa matokeo maishani mwako. Ukikaa na vitu/watu hasi (NEGATIVE thinkers), watakujaza vitu hasi, hizo zitakuwa ndio MATOKEO maishani mwako. Hali kadhalika, ukikaa na watu chanya (POSITIVE thinkers) watakubadilisha mtazamo wako na namna ya kufikiri, na utakuwa mtu wa kufanikiwa.

Kumbe! Mafanikio y
ako huanza na kufikiri mafanikio? Ndio, yaani mawazo tu! kisha mambo mengine hufuata. Je! umejiuliza ni kwanini IMEKUPASA kusoma na kutafakari Neno la Mungu kila siku? Ona hapa, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza” (Yohana 1:1-5). Yaani pasipo Neno, hakikufanyika chochote kilichofanyika! Hata leo, pasipo Neno, hakuna chochote kitu kitafanyika.

Daudi akijua siri hii, alianza kuandika Zaburi ya kwanza na kusema SIRI ya mafanikio yake; ni KUTAFAKARI NENO usiku na mchana, kisha akasema, mtu wa namna hiyo atakuwa “kama mti uliopandwa kwandokando ya vijito vya maji, uzaao matunda yake kwa majira yake, wala jani lake halinyauki na KILA ALITENDALO LITAFANIKIWA”! Ona tena Mungu akimwagiza Yoshua wakati akimkabidhi majukumu ambayo Musa alifanya, akasema, “Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana” (Yoshua 1:7, 8).

Kusudi la kukwambia siri hii sio kukufundisha kukimbia watu, ila ujue unapokea kitu gani kutoka kwao, na kujilinda na mambo/mawazo madhaifu au haribifu. “Usidanganyike, maneno mabaya huharibu tabia njema”. Usifikiri ni maneno tu, kesho-kutwa hayo maneno yatakuwa ndio tabia yako! Kumbe, hukujua kwamba unabadilika kadri usikiavyo vitu vya aina fulani, ghafla unajikuta na wewe unavitenda au kuvitamani, kwa sababu VITAUJAZA moyo wako! Na kwa kuwa umeviwaza/tafakari, vimekuwa na nguvu kwako.

Ukijua siri hii, ndipo utajua kwamba Ibilisi/mtu akitaka kukukosesha katika njia za Mungu, hakutakii MEMA. Kumbuka, hatuishii KUSOMA na KUTAFAKARI, bali KUTENDA sawa na hilo Neno. Ukitaka kuona siku njema kila uchwao, jifunze kukaa katika Neno, soma SANA na tafakari hilo, HAKIKA hutakuwa kama ulivyo. Miaka yako itakuwa heri na uzao wako utaitwa uliobarikiwa.

Frank Philip.

Comments