NEEMA NA AMANI IWE KWAKO.

Na mtumishi wa MUNGU Gasper Madumla
Imeandikwa;
" Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. " Waefeso 1:2

Bwana Yesu asifiwe...
Nakusalimu ndugu mpendwa katika Kristo Yesu maana siku ya leo nakutakia neema na amani ya Kristo itawale maisha yako.Si mara nyingi ukutane na mtu kisha aanze kukutakia amani ya namna hii.
Andiko hilo hapo juu linatuonesha wazi wazi kabisa kwamba NEEMA na AMANI hutoka kwake MUNGU Baba na wala si pengine popote pale,sababu huwezi kuinunua neema wala amani,bali hupatikana kwa Mungu tu.
Neema inayoelezewa hapo,ni ule upendeleo wa Kiungu apewayo mtu pasipo hata kuomba. Mfano,tazama sisi tuliokuwa wadhambi wa kutupwa lakini leo tumeokoka kwa neema yaani pasipo kuomba,hii ni NEEMA ya kipekee.
Unaweza kujiuliza kwamba kwa nini Paulo alikuwa akiwatakia neema na amani ya Kristo hawa ndugu wa Efeso?
Sababu angeliweza kuwatakia wafanikiwe kwa habari ya pesa,lakini tunaona sivyo alivyokuwa akiomba Paulo kwa Efeso.

• Kuna nini basi ndani ya NEEMA na AMANI ya KRISTO?
Ok,
Paulo alijua kwamba ndani ya neema ya wokovu na amani ndipo mahali sahihi ya mambo yote anayohitaji mwanadamu chini ya jua hili.

Jambo moja la msingi katika maisha ya mwanadamu analolihitaji sio pesa bali kila mwanadamu anahitaji kuwa na AMANI ndani ya moyo wake maana pesa bila amani si kitu. Paulo anawatakia amani efeso,amani ile itokayo kwa MUNGU Baba. Kwa lugha nyingine Paulo anawasii wana wa Efeso wampokee Yesu ambaye yeye ni mfalme wa amani.
Bwana Yesu asifiwe...
Ipo tofauti ya maneno haya NEEMA na AMANI vile jinsi ilivyoelezewa kimaandiko,biblia inatuambia kwa habari ya AMANI kwamba amani ni ya kutafutwa,tunasoma;
" Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; " Waebrania 11:14

• Katika andiko hilo hapo juu tunaambiwa tutafute amani kwa bidii kwa watu wote,kumbe amani ni ya kutafutwa.
Hii ina maana kuwa yeye mwenye amani ni yule mwenye kuwapenda watu wote,pasipo kuangalia mapungufu yao. Mungu hakutuagiza tuwapende wanaotupenda tu bali tuwapende wote zaidi sana wale watuchukiao.

• Unapomtakia mtu neema na amani kwake ni kama vile unamvuta na kumsogeza kwa Kristo Yesu maana Yeye Bwana ndio mfalme wa neema na amani pia.
Hata kama mtu mbaya,amekuudhi wewe usimuombee mabaya,bali mtakie mema na amani pia zitokazo kwa Mungu Baba.

Najua wazi unaweza kuwa umekwazika mno,kiasi kwamba hata umemnenea mabaya mtu aliyekuuzi. Siku ya leo hupaswi kukaa na huo uchungu hata siku kuisha bali ni kumsamehe kwa lolote lile na pia kumtakia NEEMA na AMANI zitokazo kwa MUNGU BABA.
Unapomtakia mtu amani,ujue kwamba nawe utapokea mara mbili ya amani ile uliyomtakia. Hii ni kanuni ya kawaida kabisa isiyohitaji hata kwenda shule,kwamba utapata ulichokitoa. Hata maandiko yameelezea jambo hili;
Imeandikwa;
" Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. " Wagalatia 6:7

• Hivyo basi yeyote mwenye neema ya wokovu/ aliyeokoka safi huwa na amani moyoni mwake.
Ukihitaji amani ya moyo wako,basi mkabidhi Bwana Yesu maisha yako,kisha kaa magotini pake na hapo ndipo mwanzo wa amani.

Basi kwa maneno hayo machache napenda siku ya leo nikutakie NEEMA na AMANI ya Kristo ikae kwa wingi ndani yako.
• Kwa ibada ya maombi na maombezi,usisite kunipigia kwa namba yangu hii;
0655-111149.

UBARIKIWE.

Comments