NENO LA MUNGU NI NINI?

Na Nyandula Mwaijande.

Ni mbegu inayoota na kuzaa matunda, Ni waraka, barua au ujumbe kutoka kwa Mungu kuja kwa wanadamu. Neno la Mungu ni moto unaoteketeza kila kilichokuwa si sahihi. Neno la Mungu ni nyundo linagawa nafsi. Neno la Mungu ndiyo kweli inayodumu milele (Yohana 17:17) Uwatakase na ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Neno la Mungu linatuweka huru (Yohana 8:32) tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.
Neno la Mungu ndilo linalompa mtu uhakika wa jambo ambalo hauwezi kuyumbishwa na kitu chochote. Neno la Mungu moyoni mwako ndilo linalokupa uhakika wa mambo yako yote; (wokovu, uponyaji, ushindi katika majaribu, mamlaka yako juu ya shetani na kazi zake, uzima wa milele n.k.). Neno la Mungu linapokuwa limefika mahali lazima litaleta mabadiliko.
Neno la Mungu lina nguvu sana kiasi cha kutenganisha roho, na nafsi na mwili! Pia mawazo na makusudi ya moyo yanakuwa wazi mbele zake huyo aliye na neno la Mungu ndani yake (Waebrania 4:12) Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
NENO LA MUNGU LIMEKUWA MSAADA MKUBWA SANA KWETU KWASABABU ZIFUATAZO;
• Si roho zote zimetokana na Mungu
1Yohana 4:1 Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.
• Kuna roho zidanganyazo
1Timotheo 4:1 Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani.
• Kuna wapinga Kristo katikati ya watu wa Mungu
1Yohana 2:18-19 Watoto ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu.
• Kuna walimu wa uongo
2Petro 2:1 Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia.
• Kuna wajiingizao kwa siri, au kwa hila katikati ya wakristo
Yuda 1:3-4, 12-13 Wapenzi nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo. Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung’olewa kabisa; ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele.
Neno la Mungu ni msaada mkubwa kwa mtu yeyote anayetaka kukua na kudumu katika maisha ya kiroho, hawezi kudanganywa wala kupotea maana ndani yako una Neno la kutosha hivyo chochote utakachofanya au kuamua utasikiliza uongozi wa Roho Mtakatifu, maana Roho Mtakatifu siku zote anazungumza sawasawa na Neno la Mungu hata siku moja hawezi kukuongoza tofauti na Neno la Mungu. Hivyo mimi na wewe kama watu tunaomuamini Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yetu kuna umuhimu wa kujua Neno la Mungu kwa undani maana litatupa uwezo wa kutafsiri na kukipima kile ambacho tumekiona au kukisikia katika ulimwengu wa roho kwa sababu ya kuomba au mafundisho ya Neno la Mungu.
Shetani anafanya kazi usiku na mchana kupitia walimu wa uongo, ili ukose kuijua kweli hivyo ni vema moyoni mwako uliweke Neno la Mungu na ndilo litakalokusaidia kujua kwamba kile unachofunuliwa katika maombi au unachofundishwa kinatoka kwa Mungu au la.
Zaburi 119:105 Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.
Zaburi 119:11 Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.
MUNGU AWABARIKI SANA NA ATUSAIDIE TUWEZE KUSOMA NA KUTAFAKARI NENO LAKE KILA WAKATI MAANA NDILO LINALOTUPA USHINDI DHIDI YA SHETANI.

By  Nyandula Mwaijande.

Comments