ROHO NYUMA YA MAFANIKIO YAKO - I

Na Frank Philip.

“Kuna nini basi, chini ya mkono wako? Nipe mkononi mwangu mikate mitano, au cho chote ulicho nacho hapa. Yule kuhani akamjibu Daudi, akasema, Hapana mikate ya sikuzote chini ya mkono wangu, ila mikate mitakatifu; ikiwa wale vijana wamejitenga na wanawake. Naye Daudi akamjibu kuhani, akamwambia, Hakika tumejitenga na wanawake siku hizi tatu; napo nilipotoka, vyombo
vya vijana hawa vilikuwa vitakatifu, ingawa ilikuwa safari ya sikuzote; basi leo je! Vyombo vyetu havitakuwa vitakatifu zaidi? Ndipo kuhani akampa ile mikate mitakatifu; kwa maana hapakuwa na mikate ila ile ya Wonyesho, nayo imekwisha kuondolewa mbele za BWANA, ili itiwe mikate ya moto siku ile ilipoondolewa” (1Samweli 21:3-6).

Nimejaribu kufuatilia sana mafanikio ya Mfalme Daudi, na kuna mambo kadhaa ambayo nitakuwa nayataja moja baada ya jingine katika masomo mbali mbali. Moja ya jambo ambalo nimejifunza kama SIRI ya mafanikio ya Daudi ni KUJITENGA.

Kazi ya Daudi ilikuwa ni kuchunga kondoo za baba yake. Katika watoto nane (8) wa mzee Yese, Daudi alikaa peke yake (kutengwa) akikaa na vijakazi tu, kondeni wakilisha kundi. Huko kondeni, Daudi alijifunza kutumia silaha zake, na kupiga kinubi (muziki). Mungu alimpitisha katika shule yake ya kumwandaa kuwa JEMADARI, KIONGOZI na MWIMBAJI (mwana muziki) kwa VITENDO.

Wakati bado akiwa machungani, mazoezi ya kivita yalianza na simba na dubu, kisha baadae akahitimu kwa kumtandika Goliath. Hii ilimfanya KILA mtu katika Israel AJUE kwamba yuko JEMEDARI katikati yao, ila ilimchukua muda. Wakati Daudi anaendelea na kazi yake ya kukaa kondeni na kondoo, alipata kazi nyingine (part time job), ambayo ilikuwa ni kumpigia kinubi mfalme Sauli. Hebu fikiri, je! Mfalme atatafuta mtu asiye HODARI katika muziki kumpigia muziki? Bila shaka Daudi alikomaa sana kama mwana muziki kabla hajapata kazi ya kumpigia kinubi mfalme ikulu. Angalia, kufanya kazi kwa bidii, ni ishara tu ya mafanikio ya mtu. Angalia tena, mambo uyafanyayo ukiwa PEKE YAKO (sirini), ndiyo yatakayo KUSIMAMISHA au KUKUANGUSHA ukiwa hadharani.

Kwa sababu ya umaarufu wake, baada ya kumshughulikia Goliath, haikuwa rahisi tena kwa Daudi KUJITENGA. Hapo bado Mungu alikuwa anamfundisha hatua zingine za kuwa mtu bora na mkuu zaidi. Kila Sauli alipoona jinsi Daudi anafanya kazi kwa bidii, hekima na busara, huku akikubalika sana na watu wa CHINI (sio wakuu tu) (1 Samweli 18:5-9), WIVU wa Sauli juu ya Daudi uliwaka kama moto. Ndipo Sauli akaadhimia kumuua Daudi. Sasa, ukiangalia CHUKI ya Sauli kwa Daudi, utaona kama ilikuwa ni kitu KIBAYA, ila ilikuwa ni NAFASI tena ya Daudi KUJITENGA na KUJITAKASA zaidi. Kwa mfano, angalia 1 Samweli 21:3-6, wakati Daudi anamkiambia Sauli, alijitakasa (tengwa) kwa kiwango cha kula mikate ya WONYESHO bila kupata madhara! Mikate ya wonyesho walikula makuhani tu, tena wakiwa wamejitenga na DHAMBI na kila kitu najisi, la sivyo, mtu asiye msafi akila hufa. Ona jambo hili, Daudi alikuwa amjiweka safi mbele za Mungu muda wa kupanda kuelekea mafanikio yake.

Kipindi cha kujitenga kwake, ndipo Daudi alimjua Mungu kwa kiwango kingine. Katika mateso yake, Daudi aliimba, hata akisema “BWANA ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu” (Zab. 23), anajua maana yake; alifika mahali pa kuanguka kwa njaa na kuhitaji kipande cha mkate (1Samweli 21:3-6). Akisema, “nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti” (Zab.23), anazungumzia uzeofu (experience) na sio hadithi za watumishi wengine au za kwenye maandiko. Ilifika mahali Daudi akaona sasa ana hatua moja tu kati yake na mauti (1 Samweli 20:3). Aliposema “nitayainua macho nitazame milima, msaada wangu watoka wapi?” kisha anajijibu mweneywe, “msaada wangu utatoka kwa BWANA, aliyeziumba mbingu nan chi” (Zab.121), Aliona jinsi ambavyo alibaki na mtu mmoja tu, Jonathan, ambaye pia ni mwana wa Adui yake! Ilibidi ajitahidi kumwamini kwa sababu ya viapo vyao walivyoapiana mara mbili! Laa sivyo, Daudi haoni mtu, ila milima tu, mauti na hofu ziko kila upande. Alikuwa a AMETENGWA! Katika kutengwa kwake, hakwenda kulala na makahaba wa Kifilisti kama Samsoni, yeye alimtafuta BWANA wa Majeshi. Daudi mwana wa Yese, hadi sasa jina lake ni kuu mno japo amekusanywa na baba zake.

Ona jambo hili, ukiona mtu anamtenda Mungu dhambi, eti, kwa sababu AMETESEKA vya kutosha, na sasa anasema “hata WATU watanielewa” kwa sababu ameteswa sana, huyo hajui asemacho, kwa maana adui anakatilia mbali NDOTO zake na MAFANIKO yake ya baadae bila yeye kujua! Akidhani ni mambo ya muda tu, kumbe! Kila hatua inahesabu uendako. Mapito ni ya kila mtu, jichunge usiwe mjinga upitishwapo kwenye “bonde la uvuli wa mauti”, hapo ndipo Mungu alikoamua kukupitisha kabla ya kukuweka “juu ya vilele”; hapo ulapo chakula chako, ndipo “WATESI wako walipo”, naam, ndio, BWANA anajua kwamba ndipo pa kuinukia kwako, mtazame Mungu nawe utaishi. Kula kwa amani huku adui zako wakikukodolea macho kwa maana punde tu, watajua UKUU wa Mungu wako.

Nataka uone jambo hili, Sauli alipozidi kumwonea wivu Daudi, alimshusha kikazi (alimpa demotion), kutoka ikulu, kutoka nafasi ya mtu wa karibu na mfalme hadi kuwa akida (1 Samweli 18:12-14). Sauli hakujua kwamba hii ilikuwa NAFASI nyingine ya Daudi KUJITENGA na kukaa karibu na Mungu zaidi. Kule akiwa akida, Mungu alimfundisha mambo ya UONGOZI, UTAWALA na KUHESHIMU watu; watu wakampenda zaidi, na Sauli akamwogopa zaidi Daudi kwa mana aliona kwamba Mungu yuko pamoja naye.

Angalia hapa, ukiona watu wanapenda sana KUJISOGEZA mbele (kukaa viti vya mbele), na wasipotambulishwa katika mikutano ya watu, wanajisikia vibaya, ni dalili tu ya roho mbaya ambayo inamnyima mtu FARAGHA na Mungu. Kama unadhani ni mimi nimesema, kumbuka BWANA alisemaje juu ya mahali pa kukaa mtu aalikwapo karamuni; kumbuka habari ya matumizi ya chumba cha ndani, huko sirini ambapo BABA huona. Ukijikuta unatafuta kwa BIDII kuonekana hadharani (public), kuliko kuonekana kwa BWANA, huko sirini katika maombi, kujifunza na kusikiliza, jua kuna jambo sio sawa. Mungu huinua watu kutoka mavumbini, ILA kwa wakati wa Mungu; hata kama uko machungani, hakuna mtu anajua kwamba upo, wewe fanya kazi zako kwa bidii, uaminifu, na JITENGE na uovu, siku moja utaketi na wakuu katika ngazi mbali mbali za wito wako. Najua sana umuhimu wa kujitangaza (MARKETING), ila jiulize unafanya kwa UMAARUFU wa nani? Kama ni kwa BWANA, songa mbele, ila kama unajijengea JINA kuu, bila KUMJALI na KUMHESHIMU Bwana, kumbuka mnara wa Babeli.

Basi nikisema haya, tusisahau KUJINYENYEKEZA chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, TUKISUBIRI kwa saburi kuinuliwa kwa wakati wa Bwana.

Amani, rehema, neema na Baraka za Bwana wetu Yesu, ziwe juu yenu tangu sasa na hata milele.

Frank Philip.

Comments