SHETANI NI NANI?


- Ni roho iliyoasi, ambayo haina mwili, ingawa wakati mwingine anajivika umbo Fulani la kitu kujionyesha kuwa siyo yeye, kumbe ndani ni yeye halisi.
Mwanzo 3:1-5 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.
Ayubu 1:6 Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao. Ayubu 2:1 Tena kulikuwa na siku hao wana wa Mungu walipokwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao, ili kujihudhurisha mbele za BWANA.
- Ni roho iliyoasi na ina uwezo wa kuzunguka na kuingia popote kwa vile haina mwili
1 Petro 5:8 Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama samba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.
- Ni adui yetu na amejiandaa vema na vita Ufunuo 12:7-9
Shetani maana yake ni mshindani, pia ni joka na ibilisi.
TABIA ZA IBILISI/SHETANI
i. Yeye hapumziki (1Petro 5:8)
ii. Yeye halali
iii. Siyo kama bundi anayesinzia (yeye hasinzii)
iv. Yeye siyo mvivu
v. Wakati wote amevaa silaha za vita na anazitumia vema kwa kadri ya mahitaji yake
vi. Hafanyi kazi kimazoea
vii. Ni mbunifu
viii. Anawaza vita muda wote
ix. Anajifunza jinsi ya kutumia silaha wakati wote
x. Hana likizo ya uzazi wala ya kazi
xi. Ni fundi mzuri wa kulipiza kisasi
xii. Ni kama panya anayevizia kutoboa sanduku na akipata nafasi kidogo ya kuingia ataharibu kila kitu
xiii. Ni baba wa uongo (Yohana 8:44) Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tama za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.
xiv. Ni mdanganyifu mkubwa (Ufunuo 12:9) Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye ibilisi na shetani audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.
xv. Ni mpambaji mzuri wa maneno yake (Mwanzo 3:1-5)
xvi. Hachoki kutafuta habari mpya
xvii. Ni mwivi (Yohana 10:10a) Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu;
xviii. Yeye ni mwuaji (Yohana 8:44)
JINSI YA KUMSHINDA/KUPIGANA NA IBILISI/SHETANI
• Kumtangazia shetani kuwa mtu aliye ndani ya Yesu Kristo ana nguvu kubwa kuliko yeye (shetani)
• Ili uweze kumshinda/kupigana na Ibilisi ni lazima uende kiroho kama yeye alivyo katika roho iliyoasi. Ndani ya miili hii ya kibinadamu, tujawe Roho Mtakatifu, tuvikwe ule utukufu wa Mungu na hatimaye tuwe tayari kupigana. Tunapaswa kwenda kinyume na hizo tabia zake, na hapo itakuwa rahisi kumshinda. Luka 4:1-13, 1Yohana 2:13-14
• Yeye hapumziki, sisi tusipumzike wala tusilale (1Wathesalonike 5:6-7)
• Yeye siyo mvivu – Tunatakiwa tuwe hodari zaidi yake. Tusiwe wavivu wa sala, maombi, kusoma Neno la Mungu. Kudumu katika sala, maombi na kusoma neno la mungu ndiyo njia pekee ya kumshinda shetani.
• Tuvae silaha za Kristo na tuzitumie kama inavyotakiwa. Waefeso 6:10-18
Kuwa na silaha za kiroho ni muhimu sana katika maisha ya kiroho.
WAKRISTO WA SASA
- Hatuna ile kweli iliyo moyoni ya kuishi maisha ya wokovu, haki na ukweli.
- Hatutumii ule upanga wa Roho Mtakatifu ambao ni Neno la Mungu kama Yesu alivyotumia na kumshinda adui yake.
- Zaidi ya yote hatudumu katika maombi, hata tukifanya ni kwa kiasi kidogo.
- Hatuna ule utayari wa kupeleka Injili.
• Maisha ya kiroho hayana likizo mpaka pale utakapokufa (2Timotheo 4:7) Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda.
• Shetani ni mwongo na mdanganyifu, sisi tuwe wakweli na waaminifu.
• Shetani ni fundi wa kutengeneza urafiki kama alivyofanya kwa Eva. Hivyo tusimpe nafasi katika maisha yetu kwa jinsi yo yote na wala tusiwe na urafiki naye. (Yakobo 4:7) Basi mtiini Mungu, Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.
MUNGU AWABARIKI SANA KWA KUJIFUNZA SOMO HILI NI JUKUMU LAKO KULIWEKA KATIKA MATENDO ILI UWEZE KUISHI MAISHA YA USHINDI DHIDI YA SHETANI.

By Nyandula Mwaijande.

Comments