SIO KILA AHADI YA MUNGU NI YAKO

Na Frank Philip


“Ndipo ilipoonekana mikondo ya maji, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Ee BWANA, kwa kukemea kwako, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwako. Alipeleka kutoka juu akanishika, Na kunitoa katika maji mengi. Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia, Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi. Walinikabili siku ya msiba wangu, Lakini BWANA alikuwa tegemeo langu. Akanitoa akanipeleka panapo nafasi, Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami. BWANA alinitendea sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu akanilipa. Maana nimezishika njia za BWANA, Wala sikumwasi Mungu wangu. Hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu, Wala amri zake sikujiepusha nazo. Nami nalikuwa mkamilifu mbele zake, Nikajilinda na uovu wangu. Mradi BWANA amenilipa sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake. Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili; Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu; Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi. Maana Wewe utawaokoa watu wanaoonewa, Na macho ya kiburi utayadhili” (Zaburi 18:15-27).

Ni rahisi sana kuchukua msitari kwenye biblia na kuanza kuung'ang'ania, na KUMDAI Mungu afanye kama alivyosema. Umewahi kujiuliza kama UNASTAHILI kudai unachodai? Najua hili ni swali gumu, ila wengi watakuja na majibu mepesi. Mmoja atasema, “mimi ni mtoto wa Mungu, na ahadi hizi zote ni zangu”, Sawa, Je! unajua “aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi”? 1 (Yohana 1-5). Je! utadai ahadi za Mungu wakati unajua kabisa kwamba UMEMKATAA Mungu kwa matendo yako machafu yale utendayo kwa SIRI? Je! Mungu ataangalia tu maneno yako na kuacha kuuchunguza moyo wako na kiuno chako? Je! Matendo yako hayatangulii mbele za Mungu kabla ya maombi na dua zako? Mbona hukuanza na kudai kuwa kufunga na kuomba kwamba “aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi”, na unamsihi Mungu akusaidie kuvuka hapo? Badala yake unadai tu baraka na mafanikio hasa kupata mali na utajiri?

Daudi anasema, “Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili; Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu; Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi. Maana Wewe utawaokoa watu wanaoonewa, Na macho ya kiburi utayadhili” Je! Bwana Yesu hakutufundisha pia? Angalia tena hapa, “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao” (Mathayo 5:3-10). Kuna HALI/TABIA zingine katika MAISHA yako, zitaleta tu MATOKEO fulani, haijalishi unaomba nini. Kwa mfano, kama wewe una rehema au kufadhili watu, kabla hujaomba na kufunga ili watu wakurehemu na kukufadhili, watakuja tu, ole wake MPOTOVU kwa maana Mungu atajionesha MKAIDI kwake, hata kama anakiri ahadi zote za kwenye biblia na kukesha hekaluni.

Ukitaka kudai ahadi za BABA, hakikisha wewe ni MTOTO wake wa HALALI. Tafuta kukubaliwa Naye, sio kwa KUMTUMIKIA tu, bali kwa UHUSIANO wako naye; kisha OMBA lolote kwa Jina la Yesu UTAPEWA.

Frank Philip.

Comments