UNAFANYAJE UNAPOKUTANA NA JAMBO USILOTARAJIA?

Na Frank Philip

“Naye Yeftha akamwekea BWANA nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli, ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha BWANA, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa […..] Binti yake akamwambia, Baba yangu, wewe umemfunulia BWANA kinywa chako; basi unifanyie sawasawa na hayo yaliyotoka kinywani mwako; kwa kuwa yeye BWANA amekulipia kisasi juu ya adui zako, hao wana wa Amoni” (Waamuzi 11:30, 31, 36).

Yefta alikuwa na binti mmoja, ambaye ni mtoto wake wa pekee. Siku moja akaweka nadhiri ya kumtolea BWANA sadaka ya kutekekezwa, ya kitu kitakachotoka mlangoni mwake kumlaki, ikiwa Bwana atampigania dhidi ya adui zake, na akirudi kwa amani kutoka vitani.

BILA KUTARAJIA, Ndipo binti yake, akajikusanyia watu, na kufanya mapokezi ya heshima ya baba yake alipokuwa akirudi kutoka vitani. Yeftha alipoona hilo, alijua IMEMPASA kutimiza nadhiri yake kwa BWANA.

Tazama jambo hili, na binti yake alipojua kwamba baba yake atakwenda kumtoa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA, haikumsumbua kwa maana alimjua Mungu wa baba yake. Binti aliomba udhuru akajiombolezee kwa miezi miwili. Akafanya hivyo, kisha akarudi kukabidhi shingo yake achinjwe, ili baba yake ASIMKOSEE Mungu wake.

Nilipotazama mistari hii nilijiuliza maswali mengi sana. Je! Tupo wangapi ambao katika shida zetu tunamwahidi Mungu mambo mbali mbali, kwa kusema au katika nafsi zetu; lakini BWANA akiisha kutuvusha katika TAABU zetu, huanza kuona tuliahidi jambo KUBWA sana au GHALI kulitimiza, kisha kuomba msamaha, kuahirisha-ahirisha au kuacha tu kwa maana hakuna ajuaye ila wewe na Mungu?

Jiulize mwenyewe. Unapaokutana na jambo usilotarajia katika maisha yako, jambo la gharama KUBWA, unafanyaje? Je! Unamwacha Mungu kwa ajili ya hiyo gharama? Je! Unatafuta njia ya mkato au nyingine (alternatives), ili usifanye MAPENZI ya Mungu? Zidi kujiuliza, unapokuwa na matarajio fulani kwenye NDOA yako, kazi yako, biashara yako, watoto, nk., na sasa mambo yanatokea KINYUME na matarajio yako, je! Unaamua kufanya nini? Je! Utazidi kumpenda Mungu na kumtii hata kama mambo yanatokea kinyume na matarajio yako?

Sikujua kama yupo aliyeenda mbele zaidi ya Ibrahim, kwa habari ya kumchinja mtoto wa viuno vyake mwenyewe kama sadaka kwa BWANA; Yeftha alivuka hatua hii, akamtolea BWANA mtoto wake wa pekee sadaka, ilimradi asimkosee Mungu. Ni mara ngapi tumeharibu ushuhuda kwa sababu tumeona kumfuata Bwana ni njia ya kupanda wakati kuna mteremko? Je! Mbinguni sio juu na kuzimu chini? Sasa mbona ikifika wakati wa KUPANDA kilima tu, tunaona shida na kuangalia njia za kushuka mteremko? Je! Si kwa BWANA tunafanya haya?

Kumbuka, kama Ayubu na haki zake zote alipitishwa mitihani migumu, mimi na wewe tutapanda cheo bure tu? Kama BWANA wetu alijaribiwa na Ibilisi, wewe ni nani hata usijaribiwe? Kama akina Daniel, Shedrak, Meshak na Abednego, na uelekevu wao wote, walipita njia zao zikiwa na miiba mingi na vilima vilivyoinuka, wewe ni nani upite sakafuni tu, mteremko na kujisifia vitu/mali za dunia hii (magari, nyumba, pesa, elimu, nk.) na kuviita baraka! Kweli ni Baraka za BWANA, ila Je! Yusufu alipotupwa shimoni, kisha kuuzwa kama bidhaa, kuwa mtumwa wa Wamisri, kufungwa gerezani kwa miaka kadhaa, nk., hakuwa amebarikiwa pia? Kumbuka, hata katika moto, maji mengi, njia zenye miiba, jangwa lenye kitisho na nyoka za moto, wewe umebarikiwa. Mambo hayo YOTE hutokea ili kukujaribu na kukutweza, ILI Mungu ajue KAMA wewe unampenda, naye atakupa mwisho mwema, kama ukizidi kumtii na kumheshimu katika taabu zako.

Ukitizama mitihani katika njia zako za Mungu, ukaogopa, na kisha ukajitafutia miungu mingine na kuiabudu, jua neno hili, haijalishi unaitwa kwa jina gani, mwisho wako sio mzuri.

Jifunze kujua njia za BWANA, sio kila siku utakaa na kustarehe, zipo siku za taabu na vita. Jipange vizuri, BWANA akiisha kukuvusha, nawe ukampendeza katika yote, ndipo utastareheshwa kwa sababu Mungu hapendi kusikia vilio vya watoto wake, hasa waonewapo na adui zao.

Frank Philip.

Comments