UNAJUAJE KWAMBA UMEOMBA VYA KUTOSHA?

Na Frank Philip

Utasikia mara nyingi watu wakisema, “imetupasa kuomba bila kukoma”, sawa, BWANA alitufundisha hivyo pia kwamba “IMETUPASA kuomba bila kukoma”; kwa sababu kila siku tuna mahitaji yetu, na ya watu wengine pia.

Sasa, nataka ujifunze jambo hili, kuomba ni ishara ya UHUSIANO wako na Mungu, na sio tu kwa sababu ya mahitaji yako. Nitakupa mfano. Kama una uhusiano mbaya na baba yako mzazi, je! Utakuwa na UHURU na MSUKUMO kiasi gani kurudi-rudi kuomba mambo MENGI kila saa? Utagundua KIWANGO cha uhusiano wenu kinaPUNGUZA (limit) idadi ya kurudi-rudi, hasa kwa yale mambo ambayo unaweza KUVUMILIA tu yakapita. Lakini kama unaUHUSIANO wa KARIBU, ndipo kinatokea kitu kinachoitwa KUDEKA, yaani KILA kitu wewe unakimbia mara moja kwa baba yako na kusema/kuomba. Je! Mungu ni BABA yako wa karibu kiasi gani?

Umewahi kujiuliza kama ukiombea jambo fulani maalumu (specific) kwamba unaomba hadi lini? Utajuaje kwamba sasa imetosha? Hili ni swali la kujiuliza. Wengi watakuambia PUSH (Pray Until Something Happens), sawa, ni jambo zuri. Je! Unajua majibu ya maombi yako HUJA kwa MUDA wa Mungu na sio kwa muda wetu? Umewahi kujiuliza kama unaombea jambo ambalo MUDA wa hilo jambo kutokea ni miaka 30 mbele? Je! Utaendelea kuomba kwa miaka 30 juu ya hilo jambo “usiku na mchana bila kukoma” hadi litokee? Hebu fikiri, kila siku au kila mwaka una mambo MAPYA ya kuomba, ukipanga orodha ya mambo yote ambayo HAYAJATOKEA, je! Si imekupasa kuomba masaa 24 kwa siku bila hata kumaliza orodha yako ya mambo ya kuombea? Basi kama HAIWEZEKANI kuomba kwa namna hii, je! Utajuaje kwamba “jambo fulani” umeomba vya KUTOSHA na sasa unaliweka pembeni KWA MUDA?

Angalia hapa, “Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana. […..] Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za BWANA, Eli akamwangalia kinywa chake. Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa. [….] Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za BWANA. Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. Ndipo Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba. Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena” (1 Samweli 1:10, 12, 13, 15-18).

Angalia tena, Hana alikuwa na UCHUNGU rohoni mwake, (yaani, hali ya uzito na maumivu ya ndani ambayo hukaa kama fundo, mzigo au moto). Hii hali ya UZITO wa ndani ilimpekekea “kudumu kuomba mbele za BWANA” (kuomba bila kukoma). Sasa, zingatia jambo hili, “Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe”, haimaanishi kuomba kwa sauti ni makosa, ila hii ni ile hali ya KUNENA MOYONI mwako juu ya JAMBO FULANI, hata kama uko kwenye dala dala, ofisini, njiani, ukipika, nk. ukilisukuma jambo “hilo” mbele za BWANA bila KUKOMA. Hana akasema “katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa”; Jinsi ambavyo hali ya UCHUNGU na KUUGUA ndani ya Hana ilivyo dumu, NDIVYO alidumu katika kuomba. Hana alizidi KUDUMU katika maombi bila kukoma, ndio maana tunasoma, “ndivyo nilivyonena hata sasa”; hii inaonesha MWENDELEZO wa maombi ya mfululizo, hadi hali ya ndani ya moyo wake ilipobadilika. Kumbuka, Hana alikuwa anaombea jambo maalum (specific), ambalo ni mtoto, au hali ya utasa wake.

Hana alijuaje kwamba amevuka? Angalia hapa, “Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena”. Hapa inaonesha ule UCHUNGU na MZIGO aliokuwa anabeba MOYONI ulipelekea uso wake kukunjamana. Jinsi nafsi yake ilivyoinama, na sura yake ilikunjamana kwa sababu ya yale MAUMIVU. Kipimo cha maombi yake ilikuwa MZIGO UONDOKE ndani, yaani yale MAUMIVU na UCHUNGU viondoke; mzigo ulipoondoka, Ghafla! Uso wake ukatakata.

Nataka uone jambo hili, Hana aliacha kuomba kabla hajapata mimba. Ile hali ya ndani ya moyo wake ilimthibitishia “kwa IMANI” kwamba, lile jambo aliloomba amepokea, (sio atapokea), na hilo jambo LITAkuwa lake. Kithibitisho cha KUTOSHELEZA kwa KIWANGO cha maombi ni KUONDOKA kwa ule mzigo ndani ya moyo wake.

Kama kuna jambo ZITO ndani yako, jambo ambalo linaleta MSUKUMO fulani au MAUMIVU/UCHUNGU ndani ya moyo wako, jua ni saa ya kulishughulikia na KIPIMO cha maombi ni kuondoka kwa huo MZIGO/UCHUNGU ndani yako. Utajikuta ghafla! Ukilitafakari hilo jambo, inakuja amani kama maji ya baridi, basi ujue umevuka au umefikisha kiwango cha kutosha cha maombi juu ya jambo hilo, HATA KAMA HALIJATOKEA, hilo limejibiwa na BABA yako.

Najua kuna watu wanaona aibu kuomba TENA kama jambo walishaomba, na kushukuru. Sikilize, kama ukiwaza juu ya “hilo” jambo BADO unasikia UZITO fulani ndani yako, hata kama ulishukuru, anza tena kuomba HADI usikie hali ya WEPESI wa ndani. Kurudia-rudia kuomba sio ishara ya imani haba, ila ni uhusiano wa KARIBU na BABA yako, ambapo hata “swali la kijinga” huoni haya kurudi tena kuuliza; tena kwa kurudia-rudia.

Roho Mtakatifu ajuaye jinsi tusivyojua kuomba kama itupasavyo, naam, Yeye atuombeaye kwa UCHUNGU usioneneka, Azidi kutusaidia katika udhaifu wetu na kutufundisha kuomba, na kumsikia Akisema nasi KATIKA maombi yetu.

Frank Philip.

Comments