USHIRIKINA

Na Frank Philip


“Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia BWANA kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee BWANA mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti. Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia BWANA peke yake” (1 Samweli 7:3,4).

Taf
akari neno hili, “mkamtengenezee BWANA mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake”.

Mara nyingi watu wamefikiri kumtumikia Mungu kwa AKILI zote, MOYO wote na kwa NGUVU zote, ni kuacha kufanya MAJUKUMU ya kila siku ya kuingiza KIPATO na kujikita katika kazi ya HUDUMA peke yake. Hii sio sawa.

Pamoja na majukumu ya kila siku, kazi tufanyazo katika nafasi zetu mbali mbali, jiulize tu, Je! unapita katika njia za Mungu? Je! unatenda haki kwa watu katika nafasi yako? Je! unafanya kazi yako kwa uaminifu KAMA KWA BWANA? Je! watu wanamtukuza Mungu kwa sababu ya USHUHUDA wako hapo kazini kwako? na je! UNAFANYA ushirikina?

Ushirikina ni hali ya KUMSHIRIKISHA Mungu na miungu mingine. Kila KITU ambacho unakitegemea SANA kwa kiasi cha kukiabudu, au kuona kwamba huwezi kufanikiwa bila hicho, hicho kitu hugeuka na kuwa mungu kwako.

Watu wengi hunyooshea vidole waendao kwa waganga wa kienyeji, na kusahu kwamba kuna kundi kubwa sana la watu ambao UZINZI na UASHERATI ni mungu wao! (Wakolosai 3:5) Je! hujui kwamba wapo watu wanaishi mjini kwa KIBURI cha uzuri wao, huku “wakitumainia” MIILI yao kupata NAFASI za kikazi, na MAHITAJI yao, SHULE, nk., kwa kujitoa miili yao kwa WENYE MAMLAKA na WAKUU wa dunia hii? Je! hawakumtumaini mungu wao uzinzi na uasherati kupata faida na kufanikiwa katika mambo yao? Hata lini watu wataabudu sanamu kwa kiasi hiki, na kuleta mshahara wa mbwa kwa BWANA (Kumbukumbu la Torati 23:17,18) huku wakidhani wanamtolea sadaka?

Je! mnadhani Shetani alipoamwambia BWANA Yesu, “akimsujudu atampa milki za dunia”, unafikiri hata leo Shetani hasemi na kuwajaribu watu namna hii? Ukijiinamisha (sujudu) mbele ya wenye mamlaka, utapata kila kitu, naam, hata ulimwengu wote, ila je! ukipoteza nafsi yako utapata faida gani? itakufaa nini kuwa MSHIRIKINA, huku umebeba jina la kuwa hai? Je! Jina la BWANA likufuriwe na kutukanwa kwa ajili yako hadi lini? Kwanini uwalishe wanao chakula cha laana?

Basi imempasa kila mtu kutafakari sana njia zake, na kuona mambo yaliyositirika sana, na kuomba rehema kwa BWANA, kwa maana siku inakuja ambayo BWANA atahukumu siri za wanadamu.

Mungu atupe rehema na neema ya kujua yatupasayo kufanya, ILI tukiisha kuondoa miungu kati yetu, tuweze kutengeneza mioyo yetu, na kumwabudu yeye peke yake.

Frank Philip.

Comments