HAKIKISHA UKO NURUNI NA SIO GIZANI.


BWANA YESU asifiwe.
Karibu katika fundisho muhimu sana kujua kwa kila mwanadamu.
Leo tunaangalia tofauti ya nuru na giza.
Mwanzo 1::4 ''MUNGU akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza. ''.
Nuru ni tofauti na giza.Nuru ni kinyume cha giza.
Popote penye giza ukiweka tu nuru lazima giza liongoke yaani hutaliona maana nuru imeingia.

Nakumbuka enzi nikiwa mdogo, kuna siku nilitoka kuchunga ng'ombe na mbuzi, nilipofika nyumbani niliagizwa na shangazi yangu kufuata mafuta ya taa, shangazi ambaye ndiye kama baba yangu baada ya baba mzazi kufariki nikiwa mdogo sana, nampenda sana shangazi yangu ambaye alichukua jukumu la kunilea tangu nikiwa mtoto mdogo wa kuoshwa, Siku hiyo nilikua nimechoka sana lakini ilibidi nichukue baiskeli na kufuata mafuta ya taa kwa sababu ni muhimu sana, mafuta ya taa yale yangeleta mwanga(nuru) na kwa sababu ya umuhimu wa nuru niliwahi haraka sana na kufuata mafuta ya taa.  Kwa siku ile ilikuwa ni faida sana kupatikana kwa mafuta ya taa ili giza liondoke ndani. Giza halikutakiwa kabisa. kwa muda mrefu MUNGU aliandaa mpango wa wokovu kwa wanadamu.

Hata sasa ndugu yangu baada ya kusoma somo hili najua hakika hutataka kuwa gizani tena.
Kwenye historia ya mwanadamu; Baada ya wakati wa kwanza kupita kupita ukaja wakati wa kuongozwa kwa dhamiri, baada ya wakati huo kupita ukaja wakati wa wazee, baada ya wakati huo kupita ukaja wakati wa agano la Sinai, baada ya hapo ukaja wakati wa Ahadi. Ahadi kuu ilisubiriwa na wanadamu, ni Ahadi ya kuwatoa gizani, ahadi hii ni nuru ''Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa BWANA umekuzukia. Maana, tazama, giza litaifunika dunia, Na giza kuu litazifunika kabila za watu; Bali BWANA atakuzukia wewe, Na utukufu wake utaonekana juu yako. -Isaya 60:1-2''
Inuka uangaze maana nuru yako imekuja, nuru ni BWANA YESU. Umepitia kwenye vipindi vingi, umepitia kwenye kufuata  mizimu, umepitia kwenye dhambi za kila aina, hayo yote ni matendo ya gizani. lakini sasa nuru imeingia yaani ili utoke gizani unahitaji nuru na nuru ni moja tu yaani BWANA YESU. BWANA YESU yeye mwenyewe anasema  katika Yohana 8:12 '' Basi YESU akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima. ''
Ndugu zangu giza halifai, matendo ya gizani ni mabaya. mkuu wa giza ni shetani na watoto wake hufanya matendo yao gizani, vikao vya wachawi hufanyika usiku gizani, maovu mengi hufanyika gizani ndiposa MUNGU kwa upendo wake wa ajabu anaileta Nuru ya ajabu ambayo ni YESU KRISTO. Ukimpokea YESU anakuondolea giza  na kukufanya kuwa nuru ulimwenguni  Mathayo 5:14 ''Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. ''

Ndugu zangu YESU akikuokoa anakuondolea giza na kukufanya nuru maana yeye ni nuru kuu. Ndugu yangu mpokee BWANA YESU ili akuondolee giza  na kila aina ya giza zinazokutesa , YESU atakuondolea giza magonjwa, YESU atakuondolea giza dhambi, giza madeni, giza mateso, giza laana na kila aina ya giza. kuompokea BWANA YESU ni faida kuu. 

1Petro 2:9-12  '' Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya MUNGU, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika NURU yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la MUNGU; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema. Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze MUNGU siku ya kujiliwa. ''
. Ndugu yangu ambaye hujampokea BWANA YESU tambua ya kwamba bado wewe uko gizani, unahitaji nuru hii ya ajabu na ya pekee ili utoke gizani na uje nuruni kwenye uzima. Kwa YESU ni kwenye uzima wa milele. YESU ni mabo yote ukimpata yeye umepata vyote , umepata ulinzi dhidi ya uchawi na majini, unakuwa umepata ukombozi wa mwili na roho yako, hakika kwa YESU ni raha.  Nuru hii ya ajabu ni muhimu sana kwa kila mtu. 1 Yohana 1:5-7 '' Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba MUNGU ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake. Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. ''
MUNGU ni nuru na watu wake wote wanatakiwa kuenenda nuruni, na Nuru ya kweli ni moja tu yaani kumpokea BWANA YESU. shetani giza na ndio maana kama kuna kitu anakiogopa basi ni nuru maana nuru ikiingia tu kwa mtu yeyote giza huondoka tena bila kuaga. Kama utaingia kwenye chumba ambacho kuna giza harafu ukawasha taa kubwa hakika giza hutaliona hata liliko, ndio inavyokuwa kwa mwanadamu anayempokea BWANA YESU. Waefeso 5:8-18  '' Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika BWANA; enendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo BWANA. Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee;
  kwa kuwa yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu hata kuyanena. Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru. Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na KRISTO atakuangaza. Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya BWANA. Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe ROHO; ''

Ndugu zangu wapo pia watu ambao zamani walikuwa nuruni yaani walikuwa na YESU maishani mwao lakini wakatamani giza kuliko nuru na sasa wako gizani ni hatari sana, ndugu heri kurudi nuruni. Wewe ni nyumba ya BWANA hivyo kama nyumba hiyo ambayo ni wewe harafu  imeme umekatika hakikisha umeme unawaka tena, usikubali kuwa giza na kuishi gizani. MUNGU anakupenda sana. Isaya 49:6-9  '' naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia. BWANA, mkombozi wa Israeli, Mtakatifu wake, amwambia hivi yeye anayedharauliwa na wanadamu; yeye anayechukiwa na taifa hili; yeye aliye mtumishi wao watawalao; Wafalme wataona, watasimama; wakuu nao watasujudu; kwa sababu ya BWANA aliye mwaminifu, Mtakatifu wa Israeli aliyekuchagua BWANA  asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. ''
Kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisha kanisani.
ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana
Ni mimi ndugu yako katika BWANA YESU.
Peter M Mabula
Maisha ya ushindi Ministry.
0714252292
Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments