JE WEWE NI MTUMISHI WA MUNGU ALIYE HAI?


BWANA YESU asifiwe na kutukuzwa ndugu zangu.
Karibu katika kujifunza.
Leo tunamzungumzia mtumishi wa MUNGU aliye hai.

Mtumishi Ni Neno Linalotokana Na Neno "TUMIKA" Na Utatumika Kama Tu Kuna Unaowatumikia. 
Mtumishi Kama Hana Anaowatumikia Huyo Sio Mtumishi. Mtumishi Wa MUNGU Ni Mtu Aliyetokana Na MUNGU Na Ametumwa Na MUNGU. 
 Mtumishi haanzi tu kujiita kwamba yeye ni mtumishi ila watu wakiona utumishi ndani yake na akitumika watamwita tu ''Mtumishi'' 
Marko 16:15-20 ''Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.
Basi BWANA YESU, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa MUNGU. Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, BWANA akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.
'' .
Watumishi wa MUNGU aliye hai ni watumishi wa KRISTO,
Na wameitwa na MUNGU ili watumike.

SIFA SABA(7) ZA MTUMISHI WA MUNGU ALIYE HAI NI:

1. Anamhubiri KRISTO maana hakuna uzima wa milele kwingine nje na KRISTO (Yohana 14:6, Matendo 4:12).

2. Anakemea dhambi zote bila kuangalia anamkemea Mwanadamu nani.

3. Ameweka tumaini lake kwa MUNGU  na sio kwa wanadamu.

4. Anafundisha mafundisho sahihi ya Biblia.

5 . Anamtii ROHO MTAKATIFU maana asiye na Roho wa KRISTO huyo sio wake (Warumi 8:9)

6. Anaenenda kwa Roho wala sio kwa Mwili.

7. Anampa MUNGU utukufu wote sio kujipa utukufu yeye.


 Matendo  13:2-3 “…..nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia
-Watumishi wa MUNGU huitwa na kupewa jukumu. 
Ona hapo juu ambapo MUNGU mwenyewe anawaambia Mitume kwamba wawatenge pembeni Barnaba na Paulo kwa sababu kuna kazi ambayo kwayo MUNGU amewaita.
-Hata wewe ndugu kama tu YESU amekuokoa basi tambua kwamba kuna kazi amekuitia. .
-Ndugu Yangu Hujaokolewa Kwenda Mbinguni Bali Umeokolewa Kwenda Duniani Kuhakikisha Ndugu Na Marafiki Zako Wote Wanaokoka, Ungeokolewa Kwenda Mbinguni Ungekuwa Umeshaondoka Lakini Umeokoka Uende Duniani, Mbinguni Utaenda Tu Maana Ni Haki Yako siku kazi yako aliyokuitia MUNGU ikiisha au ukimaliza.
 
Warumi 12:1-2 ( Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake MUNGU, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza MUNGU, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya MUNGU )
-Walioitwa kujitoa kabisa ili watumike. 
-Walioitwa wala hawaogopi makwazo ya wanadamu.
-Walioitwa humtii KRISTO.
-Walioitwa ni waaminifu kwa MUNGU.
-Walioitwa huvumilia yote.
-Walioitwa hata wakipigwa na kutukanwa kazi ya MUNGU kwao huendelea.
Yeremia anasema ''Utanyamazaje ikiwa BWANA amekupa agizo?''

 MUNGU anamuitaje mtu ?
- Ingawa MUNGU huwa anaita watu kwa namna tofauti lakini anatumia njia moja ya mawasiliano kwa kila muitwaji. MUNGU huwasiliana na mwanadamu kwa njia ya sita ya ufahamu ya mtu(fourth dimension), namaanisha MUNGU hutumia MAONO, NDOTO, MASIKIO YA NDANI, MACHO YA NDANI.

 Utumishi ni Wito
-Wito ni kitendo cha kumsikia MUNGU akitoa majukumu ya utumishi wako.
YEREMIA 1:5, ISAYA 42:6-7.
-Kama kweli umeitwa wala hutasikiliza wanadamu wanasema nini ila utasikiliza MUNGU anasema nini.
-Kama umeitwa lazima tu utaenda kule alikokutuma BWANA.
- Wengine walikataa kumtumikia MUNGU na kuishia pabaya.
-Ndugu tutumike maana BWANA ametuita tumtumikie.
-Mtumishi hafuati mapato ya aibu.
-Mtumishi hatakiwi kupendelea watu.
-Mtumishi halegezi kamba za kuonya watu kwa sababu tu ya vipato vyao.

  Wafilipi 3:7-11 ( Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya KRISTO. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua KRISTO YESU, BWANA wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate KRISTO; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika KRISTO, haki ile itokayo kwa MUNGU, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu. )..
Siku moja nilipata ufunuo ukisema Kwamba '' Mtumishi ambaye mafundisho yake hayana lengo la kuwafanya watu wampokee BWANA YESU na kuokoka, huyo sio mtumishi sahihi.''
Ndugu yangu na mtumishi mwenzangu hakikisha hata kama siku hiyo unahubiri utoaji hakikisha na KRISTO unamhubiri kwenye ujumbe wako, tena hakuna fundisho, somo au ujumbe ambayo YESU hahusiki hivyo hakikisha unamhubiri BWANA YESU ndani ya ujumbe wako hata kama hauhusu Wokovu lakini kama ujumbe huo umeutoa Kwenye Biblia basi YESU anahusika. 
-Watumishi wengine huwafariji watu kwamba kuna njia nyingi za kwenda uzimani huo ni uongo mkubwa na upotoshaji mkuu, Njia ni moja tu ya kwenda uzimani yaani YESU KRISTO(Yohana 14:6, Warumi 10:13, Matendo 4:12, Warumi 10:10-10)
Ndio maana mkazo wa mahubiri yetu yote lazima tumhubiri KRISTO anayeokoa.
-Matendo mema tu bila YESU hayawezi kumpoleka mtu uzima wa milele 
-Kuwa dhehebu fulani tu bila kuwa na KRISTO ndani yake hakutoshi kumpeleka mtu uzima wa milele.
-Kuwa mtu wa dini fulani tu bila KRISTO ni sifuri/Zero  tena nyeusi
- Kuhubiri upendo tu bila KRISTO ndani hatuwezi kuingia uzimani.
-Tunamhitaji YESU ili tupone. 
Luka 10:16 ''Halafu akasema, "Anayewasikiliza ninyi, ananisikiliza mimi; na anayekataa kuwapokea ninyi, anakataa kunipokea mimi. Yeyote anayekataa kunipokea, anakataa kumpokea yule aliyenituma." 
-Ndugu yangu haijalishi upokewaji wa neno unalowaambia watu ni mbaya lakini fata agizo la BWANA tu, waeleze maana neno hilo unaweza ukawaeleza leo na wakakutukana sana lakini MUNGU atawafanya miezi michache ijayo walikumbuke na kujuta na kuokoka.
-Kazi ya kuokoa sio yako ila ni ya MUNGU, wewe kazi yako ni kueleza tu. 

 Yeremia 51:20-23 ''Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;  na kwa wewe nitawavunja-vunja mwanamume na mwanamke; na kwa wewe nitawavunja-vunja mzee na mtoto; na kwa wewe nitawavunja-vunja kijana mwanamume na kijana mwanamke; na kwa wewe nitamvunja-vunja mchungaji na kundi lake; na kwa wewe nitamvunja-vunja mkulima na jozi yake ya ng'ombe; na kwa wewe nitawavunja-vunja maliwali na maakida. 
''
-Mtumishi wa MUNGU ni silaha ya BWANA ya kuwaharibu mawakala wote wa shetani.
-Mtumishi wa MUNGU hutumia mamlaka ya KRISTO iliyoko ndani yake ili kunyamazisha kila ushetani unaotesa watu.
-Mtumishi wa MUNGU huomba maombi kupitia jina la YESU KRISTO tu.
-MUNGU anaupatanisha ulimwengu kupitia watumishi wake waaminifu.
-Sisi watumishi ni rungu la BWANA YESU na ni silaha za vita vyake maana kwa sisi wachawi watakimbia, majini watarudi kuzimu, waganga wa kienyeji wala hawataonekana ''maana  BWANA YESU alidhihilishwa ili azivunje kazi za shetani- 1 Yohana 3:8b''
-Mtumishi Hutumika Katika Hali Zote Ndio Maana BWANA YESU Anawaambia Watumishi Wake "Uwe Tayari Wakati Wote, wakati unaofaa na wakati usiofaa''
-Tumeitwa na BWANA YESU ili tutangaze habari njema za ufalme wa MUNGU.
-Tumeitwa ili kuwaambia wanadamu wote kwamba ''YESU KRISTO anaokoa, wakiamini wanaokoka''

 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.


                     MUNGU akubariki sana .
                      Ni mimi ndugu yako
                       Peter M Mabula
                 Maisha ya Ushindi Ministry.
                           0714252292
 

              mabula1986@gmail.com
  MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
  MUNGU Akubariki.

Comments